June 5, 2018

UKWELI KUHUSU MAISHA YA MAPACHA MARIA NA CONSOLATA WAANIKWA NA MLEZI WAO WA KWANZA

Mlezi  wa  kwanza  wa Maria na  Consolata  Mwakikuti ,Bi Betina  Mbilinyi  akiwa katika mawazo mazito
Nyumba  waliyoishi mapacha Maria na Consolata Mwakikuti  wakiwa  wadogo  hadi  miaka  saba  iliyofika  nyumba hii ipo  Ikonda Makete
Na Matukiodaima Blog
WAKATI  mazishi  ya mapacha  waliokuwa  wameungana kiwili  wili  Maria  na  Consolata Mwakikuti yakitarajia kufanyika  kesho  katika  makaburi ya viongozi wa  dini ya  Romani Cathoric Tosamaganga wilaya ya  Iringa   mkoani  Iringa  mlezi  aliyewalea baada ya  kuzaliwa hadi  miaka 7 asema hajapata kuwaona ndugu  wa  kiume  wa mapacha hao.

Akizungumza na  matukiodaimaBlog   mlezi  huyo Betina  Mbilinyi (52)  mkazi  wa Ikonda wilayani Makete  mkoani Njombe alisema  kuwa toka  amepewa  jukumu la  kuwalea  mapacha hao  na  shirika la Misheni kwa   miaka  7  alioishinao  alipata  kukutana na ndugu  upande wa kike  pekee na  sio  upande wa  kiume .

“ Ila  nilisikia alipata  kuja  baba yao  mkubwa   akitokea  mkoani  Mbeya  ila  sikuweza  kukutana nae kwani  wakati  yeye  akija  nyumbani  kuwaona  watoto  mimi  nilikuwa  shamba  hivyo  niliambiwa  tu  kuwa  alikuja lakini  upande wa mama  walikuwa  wakija mara  kwa mara na kaka  yao  ambae  wameshirikiana  mama  alikuja  zaidi ya  mara  mbili ila nae  hakuja na kitu kwani  alikuwa akisoma wakati  huo  na  walikuwa  wakipendana  sana na kaka  yao ”  alisema  mlezi huyo .

Kuwa  kabla ya  kupewa  jukumu la  kuwalea  watoto hao  mara  baada ya  kuzaliwa katika  Hospitali ya misheni  Ikonda alikuwa  akifanya kazi ya  usafi katika  Hospitali  hiyo ya  Ikonda na uongozi wa Hospitali  hiyo  ulimpa jukumu la  kulea  watoto hao   na  kumtoa katika  kazi yake ya  awali ya  kufanya  usafi .

  Waliniomba  nifanye kazi ya  kuwalea  watoto hao  kutokana na  kuishi jirani na  Hospitali ya  Ikonda   na  walizaliwa mazingira ya Misheni hivyo  ilikuwa rahisi  kwangu  kuwapeleka  Hospitali  pale  walipohitajika na  kuwarudisha nyumbani  kwangu  kuishi nao  mimi  nina watoto  wawili ila  sina  mume  baada ya  kuachana nae  hata  kabla ya Maria na  Consolata  kuzaliwa “

Betina  alisema  aliwapenda  sana  watoto  Maria na  Consolata  kutokana na  kuwa na heshima  kubwa na  wasikivu  kwa  kila jambo  wanaloelezwa  na  walipendana  sana na  watoto  wake na  kuona kama  ni  sehemu ya  familia  yake .

“ Pamoja  na  kuishi nao kama  familia yangu  ila  nilikuwa  nikilipwa mshahara  na  misheni ila  ni mshahara ule  ambao  walikuwa  wakinilipa kwa kazi ya  kufanya  usafi  kutokana na  kunibadilishia kazi nilifurahia kuifanya kazi hii ya  kuwalea  Maria na  Consolata “

Alisema  kuwa kazi ya  kuwalea Maria  na  Consolata  ilikuwa na changamoto  kiasi  mwanzoni  wakiwa wadogo  ila  walipoendelea  kukua  kazi hiyo  haikuwa  ngumu  tena  ilikuwa ni kazi  rahisi  ambayo  alikuwa amekwisha  izoea  hivyo  aliweza  kufanya  shughuli  zake  nyingine .

“ Mshahara wangu  ulikuwa ni  ule  ule ambao nilikuwa nikilipwa japo  siwezi  kuutaja hapa ila ni  mshahara  ulionifaa na  ndio  ambao  nalipwa  hadi  sasa “

Baada  ya  kukaa nao kwa miaka saba na  walipofaulu  kujiunga na  elimu ya  sekondari walilazimika  kuondoka Makete na  kwenda  kuishi Wilaya ya  Kilolo  mkoani Iringa ambako  waliendelea na  elimu ya sekondari na ndipo  aliporejeshwa katika kazi yake ya  awali ya usafi anayoendelea nayo kuifanya hadi  sasa .

Betina  anasema  kutokana na  jinsi  alivyopata  kuishi na mapacha  hao  anajisikia simanzi muda  wote  kwani  tayari  walikuwa ni  sehemu ya  familia yake na  hata  wakati wa  likizo  yao walikuwa  wakirudi Makete  nyumbani kwake  kupumzika .

“ Wamekuwa  wakija  likizo na mara  yao ya  mwisho  ambayo  sitaisahau  walikuja mwezi wa nane mwaka jana na  hii ndio  likizo yao ya  mwisho  na tuliongea nao  mambo  mbali mbali na  kila ninapoyakumbuka baadhi ya malengo  yao ya  mbeleni  najisikia  kutokwa na machozi “

Alisema  wakati  wote  pamoja na  kuonyesha  furaha  ila  walikuwa  wakimsisitiza  sana  juu ya kuendelea  kuwaombea  kwa  Mungu  ili ndoto yao  iweze  kutimia na  mara  baada ya  ndoto  kutimia  na  iwapo  watapata kazi basi  watahakikisha  wanamsaidia kimaisha .

“ Ndoto  kubwa ilikuwa ni  kumaliza  chuo  na kuja kufanya kazi itakayowapatia  kipato  ambacho  wataniwezesha  na  mimi  na  familia  yangu  Tunaomba  mama tuombee  tuwe  wazima tukimaliza  chuo tutakulea na  wewe  mama  “ hii  ndio  ilikuwa ni kauli  yao  kwangu .

Hata  hivyo  alisema  enzi  za uhai wao  mapacha  hao  pamoja na mambo  mengine  hawakuweza  kuwekja  wazi kama  wanataraji  kuishi na  familia yao upande wa kike  wala wa  Kiume zaidi ya kuwapongeza masisita  wa Maria  Consolata   kwa  kuwawezesha  kufika hapo  walipofika .

  Hawa  mapacha  walikuwa ni watu wa aina yake  sana   pamoja na  ndugu  kufika  kuwajulia hali  hasa  upande wa kike na  kiume ila  hakuna  hata  siku  moja  walionyesha uhitaji wa  kuzungumzia  kwenda  kuishi na ndugu  zao  zaidi ya  kuomba  tuendelee  kuwaombea ndoto yao itimie “

Anasema  kuwa  sababu ya Maria na  Consolata  kwenda  kuishi  na  kusoma  Kilolo elimu ya  sekondari  ni  kutokana na shirika la Maria  Consolata  kumaliza  mkataba wake  wilaya ya Makete  na  kuwepo  wilaya ya  Kilolo  mkoani Iringa na ndio  sababu wakaamua  kupata  elimu yao ya  sekondari Kilolo.

Aidha  alisema pamoja na watoto hao  kuwa na furaha na kuonyesha  ucheshi  wakati  wote ila  walionekana kuchukizwa  sana na  wageni waliokuwa  wakiwashangaa na  kuwaona wa ajabu  pindi walipofika    kuwaona .

“ Hakika  ninaumia sana na  kifo cha Maria na  Consolata siwezi kuendelea  zaidi  nimepanga  kufika Iringa  kushiriki Mazishi  ya  Maria na Consolata  Mungu  azilaze  mahari pema roho  zao na kifo  chao kimetufunza  mengi sisi  tuliobaki”

Mkuu  wa  shule ya sekondari ya  Maria Consolata  iliyopo Kilolo  mkoani Iringa , Jefrod Kipindi  akiwaelezea  mapacha hao  alisema kwanza  hakuamini  aliposikia  taarifa  ya  kifo chao ila ilimlazimu  kuamini  baada ya  kusikia  salamu  za rambi  rambi za  Rais Dkt  John Magufuli  .

 Mwalimu  Kipindi alisema  kuwa  aliwapokea  Maria na Consolata   Januari mwaka 2011 wakitokea Ikonda wilayani Makete  na amepata  kuishi nao kwa  miaka saba  wakiwa  shuleni hapo  ambapo  pamoja na  kuiunga na  kidato  cha  sita  shule ya  sekondari  Udzungwa  bado makazi yao  yaliendelea  kuwa shuleni hapo  katika   nyumbani yao ya  Nyota  ya  Asubuhi .

Alisema  kuwa kati ya  wanafunzi  zaidi ya 163 waliokuwepo  wakati  wakijiunga na  kidato cha kwanza mwaka 2011  Maria  na  Consolata  walikuwa ni  wanafunzi  wa  kipekee  kwani  mbali ya hali  waliyokuwa nayo ila  walikuwa ni wanafunzi  watiifu na  wachangamfu  sana .

“ Awali  wanafunzi  hao  walikuwa  wakijaza  watu  shuleni na mitaani walikokuwa  wakipita  hasa  wanapokwenda  kanisani  kila mtu  alikuwa  akiwasogelea na kuwashangaa sana  ila  baada ya  kuzoeleka  hakuna  aliyewashangaa waliwachukulia kawaida  tu tofauti na  awali hadi  walimu  tulikuwa  tukiwashangaa sana  mimi  nilikuwa nikiamini ndoto yao itatimia ila  msiba  wao umetushitua  sana “

Mkuu  huyo alisema pamoja na kuwa  shule  imefunga  wamepanga  kufika  Iringa  kushiriki mazishi yao  kama  walimu na  watumishi  pamoja na  wanafunzi  wachache  waliobaki  shuleni hapo .
Kaka wa mapacha  hao  David Mwakikuti alisema   kuwa kifo  cha Maria na Sonsolata  kimempa  funzo kubwa katika maisha yake hapa duniani kwani hajawahi kuona watu wanaojimini na kusimamia haki kama walivyofanya  enzi za uhai wao 

David ambaye ni mtoto wa kwanza wa familia hiyo iliyobahatika kuwa na watoto watano alisema kuwa  kabla ya wadogo zake hao hawajaaga dunia walimwambia asiache kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu kwani hata wao walitamani kuja kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu kipindi cha uhai wao .

“Waliniambia kuwa pindi nitakapokuwa vizuri kiuchumi basi nisiache kumtegemea Mungu na niamini katika kile ninachokiamini na kukubaliana na hali halisi ya maisha halisi tuishiyo hapa duniani hivyo nitaendelea kuwajali watu wote na waina zote “

Alisema  kuwa  enzi  za  uhai  wao  alipata  kuwauliza maswali na miongoni mwa  swali alilowauliza kwanini  wanapenda kusoma  na  walimjibu  kuwa  wanatamani  kuja  kusaidia wengine  na kila  siku  hiyo ndio ilikuwa ndoto yao  na pale  waliposhindwa  kuelewa jambo hawakuishi bila  kuuliza

“Nimebahatika mara kwa mara kukutana na wadogo zangu hawa hata kipindi wanamaliza kidato cha nne niliweza kifika nikiwa kipindi hicho na soma walinipa moyo kwa kweli kwani hawakukata tamaa na walikuwa ni watu wakutaka kufanikiwa sasa nilijiuliza kama wao wanbajitahidi hivyo wakiwa na hali hiyo basi nami ilibidi nikaze buti sisi katika familia tulizaliwa watoto watano wakwanza akiwa ni yeye wapili ni Edith Mwakikuti anayesoma chuo cha sauti mwanza ,Maria na Consolata pamoja na mdogo wao wa mwisho Jaclini aliyeko  Dar es Salaam “

Wakati  kukiwa  na maswali  ya  ndugu  kutojulikana waliko ama  kuwa mbali na mapacha hao  enzi za uhai  wao Anna Fredrick Mushumbushi ni mama mkubwa wa mapacha hao alisema kuwa wao kama familia walikuwa bega kwa bega katika kusaidia watoto hao tangu walipozaliwa na wala hawakuwataenga watoto hao kama baadhi ya watu walivyokuwa wakisema 

Mshumbushi alisema kuwa taarifa za mapacha hao kuzaliwa alizipata kupitia vyombo vya habari baada ya siku saba  tangu kuzaliwa kwao na ndipo alipofunga safari kwenda Makete kwa ajili ya kuona watoto hao na tayari walikuwa wamesha kabidhiwa masisita hao kwa ajili ya kuwalea .

“Kwa hiyo baada ya kukuta wazazi wameshakabidhiwa kwa masisita hao kwa  ajili ya kumlea hawataka  kuwa na pingamizi na walitupatia  gari kwenda kwa mdogo wangu na tukawa tunakuja kuwaangalia na kurudi na ndugu wapo natulikuwa tunakuja kuwaangalia” alisema
Kuwa mara baada ya baba wa watoto hao kufariki dunia ilibidi baadhi ya watoto akiwemo kaka yao na Editha waliwachukua na kwenda nao  nyumbani Bukoba kwa babu yao na bibi yao na waliwasaidia kwa hali na mali kwa kuwasomesha mpaka hapo walipo

Hata hawa watoto walivyokuwa wamelazwa pale muhimbili nilikuwa mara kwa mara ninaenda na wakati mwigine kukiwa hakuna mtu wa kulala nao ninalala nao maana mpaka waliopoondoka kurudi Mkoani Iringa kupumzika .

Akitoa  taratibu za mazishi ya  mapacha  hao  kwa niaba ya  serikali ya  mkoa  wa  Iringa mkuu wa wilaya ya  Iringa Richard Kasesela  alisema  mazishi ya mapacha hao  yatafanyika  siku ya  jumatano kwenye makaburi ya viongozi wa RC  Tosamaganga  na kuwa  viongozi  mbali mbali  wanataraji  kushiriki  wakiwemo maaskofu  na viongozi wa  serikali  na kuwa hadi sasa  wanaendelea na utaratibu wa  kuandaa  mazishi na kuwa  watazikwa katika kaburi  moja  ila masanduku  mawili .

  Kila mmoja  atakuwa na  sanduku lakeila   hawatatengenishwa hivyo  litatengenezwa  sanduku  kubwa moja lenye  mwonekano  wa masanduku mawili  na  watazikwa kaburi  moja  tunaomba  wananchi  kujitokeza  kwa  wingi  kutoa heshima  za  mwisho”

Wakati jamii  ikiwa na  maswali  iweje  watoto  hao  wasitenganishwe  wakati wa mazishi yao  daktari    bingwa  wa  magonjwa ya  ndani  katika  Hospitali ya  Rufaa ya  mkoa wa  Iringa  Dkt  Fethy  Kundi kuwa  haoni sababu ya  kufanya  hivyo kwani  toka awali  hawakupenda  kutenganishwa .

Mlezi  mkuu wa  shirika la Maria Consolata Tanzania  Sisita Jane  Nyuti wao kama  shirika  walikuwa  wakiishi  vizuri na kwa amani na  mapacha hao  hivyo  kifo chao  ni  pigo kubwa kwa jamii na shirika.

“Watoto hao  walikuwa wa  kipekee  maana  vitu  mbali mbali  walivyokuwa  wakipewa  na  wasamaria  wema  walikuwa  wakivigawa kwa  watu  wenye  mahitaji kama  yatima  wanaowazunguka maeneo  yao “

Maria  na  Consolata   walizaliwa  mwaka  1996  katika   Hospitali ya  Misheni  Ikonda kijiji cha Ikonda wilaya ya  Makete  mkoani Njombe  kifo  chao  kilitokea  Juni 2 majira ya saa 2 usika  katika  Hospitali ya  Rufaa ya  mkoa wa Iringa  wakiwa katika matibabu .


0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE