June 6, 2018

MATUKIO KATIKA PICHA ZOEZI LA KUAGA MIILI YA MAPACHA MARIA NA CONSOLATA IRINGA

HUKU zoezi la  kuaga   na mazishi ya  mapacha  Maria na  Consolata  Mwakikuti yanafanyika  leo  katika  makaburi ya  viongozi wa  dini ya  Romani Katoliki  (RC)  Tosamaganga   kata ya Kalenga wilaya ya  Iringa  mkoani Iringa  wanawake  walioshiriki kuchimba  kaburi la mapacha hao lenye upana wa sentimita 180 na urefu  sentimita 200 wameomba  sanduku la mapacha hao  kubebwa na  wanawake   kabla ya  kuingizwa kaburini.

Huku  chifu wa  wahehe  mkoani  Iringa  wakitamani  mazishi  hayo yangefanyika  kichifu kama  alivyozikwa  chifu  Adam Sapi  Mkwawa kwa  kupiga  risasi  hewani na kaburini . 

Akizungumza  jana  makaburini  hapo kwa niaba ya  wanawake wa kata ya  Kalenga  Geogena   Sekitindi (57) alisema  kuwa  mbali ya  uchungu  waliokuwa nao  juu ya  vifo vya mapacha hao   ila  wangefurahi zaidi  iwapo  wangepewa jukumu  la  kubeba jeneza  lao  mara  baada ya  kufika eneo la  mazishi.

“ Pamoja na  kuwa  jukumu la  kuchimba  kaburi la watoto  hao  wamepewa vijana  wa waliopo katika  mashirika ya  kitume ya  RC  hapa  Tosamaganga   ila   mimi  kama  mwanamke na  binti  huyo  ambae alipata  kushiriki  semina na  mapacha hao  enzi za  uhai  wao  tumeona ni vema   tushiriki hata  zoezi la  uchimbaji wa kaburi  lao  ila ingependeza   leo  wakati wa mazishi  tupewe nafasi wanawake  kubeba jeneza lao”  alisema Sekitindi
Kuwa  heshima  kubwa  ambayo  Kalenga  imepewa ya mapacha hao  kuzikwa  Tosamanganga  ni  heshima  kubwa  iliyoambatana na huzuni kubwa  ila njia  pekee ya  kuenzi  heshima  hiyo juu ya  watoto hao  ni  ushiriki mkubwa wa  wanawake  katika mazishi  hayo  .

Kwani  alisema  ushiriki  wao  wanawake  ni sehemu ya  kuifuta machozi familia ya Mapacha hao  pamoja na  walezi  wa  shirika la Maria Consolata  ambao  waliwalea  mapacha hao  toka  utoto  wao.

 Aisha  Kibindo (16) ni mkazi wa kata ya Kalenga  ambae  amepata   kushiriki   mafunzo na marehemu hao  enzi za  uhai  wao alisema  kuwa kwa mara ya  kwanza alipata  kushiriki mafunzo  ya  kiroho ya mapacha hao  mafunzo yaliyokuwa  yameandaliwa na kanisa  na ndipo  alipokutana nao .

Kuwa  imani  yake  kuja  kuonana nao  katika mafunzo mengine  kwani  waliahidi  kuwa wataendelea  kushiriki mafunzo  mbali mbali na jamii ya  Iringa ikiwa ni pamoja na  kutoa ushauri  kwa  washiriki juu ya namna gani  wanaweza  kuishi   kama  mabinti  kwa  kujitunza  na kuzingatia masomo .

“  Tukiwa  katika mafunzo Maria na Consolata   walikuwa  wakitutia moyo  wa  kusonga  mbele  kimasomo  ya  kuwataka  wale  ambao  hawakubahatika   kufaulu    kutokata tamaa kwani  kuna maisha mengine  mazuri   nje ya  kufaulu  ila  iwapo  watakuwa  watii  na  wenye  heshima  kwa  wale  wanaoishi  nao”

Alisema  mafundisho  na  ushauri  wao  kwa washiriki wa warsha   hiyo ya  kiroho   yaliwagusa  mabinti   wengi  na baadhi ya  wale  ambao  hawakubahatika  kuendelea na  elimu  akiwemo yeye  wanaishi  kwa  kuzingatia  mafundisho  hayo na hadi  sasa  hajutii  kutofaulu  ila anajipanga  kuona  anatafuta  njia ya  kuendelea  kupambana na maisha kwa  kujiendeleza  zaidi  kielimu.

Wilbert  Kihwele ni  kiongozi  wa  vijana  wachimbaji na  wajenzi wa kaburi  la Maria  na Consolata anasema  kuwa  uchimbaji wa kaburi   hilo umeanza majira ya saa 2 asubuhi   hadi saa 7.20  mchana  na  kuwa ni moja kati ya  kaburi  ambalo  wamechimba kwa  muda  mrefu  ukilinganisha na makaburi  mengine  ambayo  wamepata  kuchimba katika  eneo  hilo .

Kihwele  alisema  kwa kawaida  kaburi   kawaida  huwa  linachukua kati ya saa 1.30 hadi saa 2 kutokana na aina ya  udongo  wanakutana  nao na upana wa kaburi  na kuwa udongo  wa  eneo  hilo ni wa kawaida  na makaburi  ambayo  huwa wanachimba ni   urefu  huwa sentimita   kati ya 95 hadi  100  na upana kati ya  sentimita 40 hadi  45  ila kaburi  hilo  limeweza  kuchukua muda  mwingi  kutokana na urefu  kuwa sentimita 200 na upana sentimita 180.

 Alisema   ukubwa  huo  unatokana na vipimo vya  Sanduku  ambavyo  walipewa  na  kuwa  Sanduku la Maria na Consolata lina upana wa  Sentimita  90 na  urefu  sentimita 160 na  kuwa kwa  upande wa kaburi  baadhi ya  sentimita  zimeongezwa kwa  ajili ya ujengaji wa kaburi .

Kiongozi  huyo  alisema  zoezi hilo la  kuchimba kaburi na kujenga  wanalifanya kwa  kujitolea na  hakuna malipo  yoyote  ambayo wao watalipwa na  hawana kawaida ya  kulipwa kwa kazi ya  kuchimba kaburi na  kuwa  wao  ni  vijana  wanaotoka ndani ya  mashirika na  jumuiya  za kanisa  na  hilo  ni  jukumu lao.

Akizungumza  kwaniaba ya chifu wa  wahehe Adam Abdu Sapi ambae  ni mwanafunzi kuhusiana na  uamuzi  wa familia  ,serikali na shirika la Maria  Consolata  la  kuwazika  mapacha hao katika  kata ya Kalenga  ambayo ni kata aliyozikwa chifu Mkwawa  mwakilishi wa chifu   huyo Gerald Malangalila pamoja na  kusikitishwa na  kifo  cha Mapacha hao ila  alisema  serikali ilipaswa kuwashirikisha  Machifu  katika vikao   hivyo .

“ Juu ya  vifo vya Mapacha hao tumesikia na  tumesikitishwa sana  kuondokewa na watoto hawa ambao  ni yatima na  baba yao alikuwa ni mwenyeji wa Mbeya na mama  Mwenyeji wa Bukoba  na sisi  sote ni  watanzania hatupaswi  kutengana uamuzi wa  kuwazika  Kalenga ni mzuri ila  ningeshirikishwa kama  Chifu katika vikao vya maandalizi tungewazika  kwa  heshima ya  chifu  wetu Mkwawa tungepiga  risasi kaburini na hewani  mimi na  wenzangu  tungepewa usafiri tungefika shida  usafiri  “

Alisema  chifu huyo  kuwa  iwapo   serikali ingewashirikisha katika  vikao  wangeweza  kushiriki  kikamilifu maana  msiba   huo ni mkubwa na  mazishi yanafanyika katika ardhi ya  chifu Mkwawa  hivyo  wangeweka utaratibu wa  kuwapa heshima  za  kichifu   watoto  hao ambao  wameondoka  ila  wameacha   historia  kubwa katika Taifa na  Kalenga .

Akizungumza  kwa njia ya  simu  akiwa  safarini  juu ya  madai ya  chifu wa wahehe  mkuu  wa  mkoa wa Iringa Amina Masenza  alisema  kuwa  mkoa umekuwa na ushirikiano mkubwa na machifu hao  pamoja na makundi  yote  yakiwemo yote   zikiwemo taasisi  za  dini ila katika  suala   hilo la mazishi  ya mapacha hao  yafanyike  wapi  ni suala la  kifamilia na kanisa  kupitia  shirika la Maria Consolata  sio   serikali  ila  serikali imeshirikishwa  tu." Hili ni suala la Kanisa  na familia  serikali  imeshirikishwa tu  hivyo  namba  kama ambavyo  watu  wengine  watakavyoshiriki tunaomba nao  waweze kushiriki kama  waombolezaji  wengine hatuwezi kuingilia maamuzi ya  kanisa “

Katika  mazishi  hayo   askofu  wa  jimbo la  Iringa Tarcisius Ngalalekumtwa ambae  ni Rais wa baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) anataraji  kuongoza mazishi  hayo huku  upande wa  serikali Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekanusha taarifa zilizoenea ya kuwa, Waziri wa Elimu Prof.Ndalichako anakusudiwa  kushiriki mazishi hayo  na viongozi  wengine  wengi  wakiwemo wakuu wa wilaya ya  Kilolo Asia Abdalah , mkuu wa  wilaya ya  Iringa Richard Kasesela na  mkuu wa  mkoa wa Iringa Amina Masenza .

Maria  na Consolata   walizaliwa  mwaka 1996 katika  kijiji cha Ikonda wilaya ya Makete  na walelelewa na shirika la Maria Consolata ,walisoma   shule ya  msingi  Ikonda Makete na  sekondari  walisoma  Kilolo mkoani  Iringa katika  shule ya Maria Consolata  na elimu yao ya  kidato cha  tano na  sita  waliipata  shule ya Udzungwa iliyopo wilaya ya  Kilolo mita chache  kutoka  shule ya  sekondari ya Maria Consolata  na  kituo  walichokuwa  wakiishi   cha Nyota ya  Asubuhi  kifo  chao  kilitokea Juni  3 mwaka  huu majira ya saa 2 usika katika  Hospitali ya  Rufaa ya  mkoa wa Iringa ambako  walikuwa  wakipatiwa matibabu 

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE