June 1, 2018

ASAS DAIRIES YAHAMASISHA UNYWAJI WA MAZIWA MASHULENI

Mkuu  wa  wilaya ya  Iringa Richard Kasesela  akigawa  maziwa  kwa  wanafunzi wa  shule  za  msingi  mbali mbali kata ya  Kihesa Manispaa ya  Iringa ,kushoto  ni  diwani wa Kihesa  Juli Sawani na kulia  ni mkurugenzi wa kampuni ya maziwa ya  Asas  Ahmed Asas
>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>
KATIKA  kuadhimisha  wiki ya  unywaji wa maziwa duniani  kampuni ya Maziwa ya Asas Dairies imegawa  maziwa kwa  wanafunzi wa  shule  mbali mbali za Manispaa ya Iringa, Mbeya na Dodoma .


Taarifa iliyotolewa  na Afisa Lishe wa Manispaa ya Iringa, Anzaely Msigwa kwenye kilele cha maadhimisho hayo yaliyofanyika kiwilaya katika viwanja vya shule ya msingi Ngome mjini Iringa  mapema leo imesema wanafunzi wameonesha kuyapenda maziwa Asas na kutamani kuyanywa kila siku.

“Jumla ya wanafunzi 30,134 na walimu 812 wa manispaa ya Iringa wamekuwa wakipata nusu lita ya maziwa toka maadhimisho hayo yaanze Mei 22, mwaka huu hadi leo Juni 1,” alisema.

Kwa kuzingatia mahitaji hayo, Msigwa aliomba kamati za shule zikae na wazazi na kujadili umuhimu wa kutoa maziwa kwa wanafunzi wakiwa shuleni.

Aidha aliiomba kampuni ya Asas itoe punguzo la bei ya maziwa hayo sambamba na kusogeza huduma hiyo jirani na shule hizo.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo  Ahmed Salim Abri alisema; “kwa kutambua umuhimu wa unywaji maziwa mashuleni, menejimenti iliamua kutenga lita 100,000 sawa na pakiti 400,000 za maziwa kuwahamasisha wanafunzi ikiamini kwa kufanya hivyo itahamasisha jamii nzima.”

"Na hilo ndilo lililotokea kwani awali tulipanga kutoa pakiti 120,000 kwa wanafunzi na walimu wa shule hizo za manispaa ya Iringa lakini ongezeko la mahitaji yake lilitulazimu kuongeza idadi," alisema.

Abri alisema kati ya pakiti hizo zenye thamani ya Sh Milioni 200, pakiti 200,000 ziligaiwa kwa wanafunzi na walimu wa shule za manispaa ya Iringa na 200,000 zilizobaki ziligawanywa katika mikoa ya Dodoma, Mbeya na Arusha ambako maadhimisho hayo yamefanyika kitaifa.

Ili kuongeza hamasa ya unywaji maziwa kwa jamii, alisema wameona kampeni ya unywaji wa maziwa wasiishie kuifanya kwenye wiki ya unywaji wa maziwa pekee na badala yake wataitanua katika wilaya zote za mkoa wa Iringa na nje ya mkoa huo.

Akinukuu taarifa ya Shirika la Afya Duniani Abri alisema kutokana na umuhimu wake mwilini, kila mtu anatakiwa kunywa wastani wa lita 200 za maziwa kwa mwaka lakini kwa bahati mbaya wapo baadhi ya watu ambao hawawezi kunywa hata robo ya maziwa kwa mwaka.

Akizungumzia umuhimu wa maziwa mwilini Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema maziwa ni lishe bora na serikali inatambua na kuwekeza katika lishe ili kufikia uchumi wa kati.

Kasesela alisema nchi haiwezi kufikia hatua hiyo ya kiuchumi kama watu wake watakuwa na matatizo ya akili ambayo chanzo chake ni ukosefu wa lishe bora yakiwemo maziwa ambayo mchango wake kwa mwili na akili ya binadamu unaeleweka.

Alisema takwimu mbalimbali zinaonesha hali ya lishe kwa wanafunzi na watoto walio chini ya miaka mitano katika manispaa ya Iringa sio ya kuridhisha.

Alisema takwimu zinaonesha asilimia 42 ya watoto chini ya miaka mitano wana udumavu huku asilimia 28 ya wanawake wajawazito wakiwa na upungufu wa damu, yote hiyo ikitokana na ukosefu lishe bora yakiwemo maziwa.

Mkuu wa wilaya aliziomba halmashauri za wilaya yake (Manispaa na Iringa Vijijini) kuangalia uwezekano wa kuwahamasisha wafanyabiashara wakiwemo wale wa vileo kufanya pia biashara ya maziwa katika maeneo yao.

"Na maziwa yanayotakiwa kuuzwa ni muhimu yakawa yale yaliyosindikwa ili kuwanusuru watumiaji na magonjwa yanayosababishwa na unywaji wa maziwa yasiosindikwa," alisema.

Katika kuchochea unywaji wa maziwa na kwa kuzingatia umuhimu wake huo, Kasesela aliwataka pia wazazi kubadili mitazamo pale wanapowakarimu wageni kwa kuwapa maziwa badala ya vinywaji walivyovizoea.

“Lakini nizihamasishe pia kamati za harusi na sherehe zingine mbalimbali kuweka maziwa katika sherehe zao kwani bei yake ni ndogo na mchango wake mwilini ni mkubwa kuliko vinywaji vingine vilivyozoeleka,” alisema na kutoa mfano war obo lita ya maziwa ya Asas yaliyosindikwa kuwa ni Sh 500 tu kiasi ambacho ni kidogo ikilinganishwa na bei ya vinywaji vingine

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE