May 11, 2018

SERIKALI YAWATAKA WARATIBU WA MASUALA YA VVU, UKIMWI NA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZWA (MSY) MAHALA PA KAZI KUTEKELEZA WAJIBU WAO KWA KUZINGATIA WELEDI


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Dorothy Mwaluko akiwa katika picha ya pamoja na Waratibu wanaosimamia masuala ya VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukizwa (MSY) katika taasisi za umma mara baada ya kufungua kikao kazi cha Waratibu hao mjini Morogoro.
Baadhi ya Waratibu wanaosimamia masuala ya VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukizwa (MSY) katika taasisi za umma wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Dorothy Mwaluko (hayupo pichani) akifungua kikao kazi cha Waratibu hao mjini Morogoro.
Serikali imewataka Waratibu wanaosimamia masuala ya VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukizwa (MSY) katika taasisi za umma kutekeleza wajibu wao ili kupata takwimu sahihi za watumishi wanaoishi na VVU, UKIMWI na wenye Magonjwa Yasiyoambukizwa (MSY) kwa lengo la kurahisisha  utekelezaji wa mpango wa kupambana na magonjwa hayo yanayoathiri utendaji kazi  wa watumishi kwa kiasi kikubwa.

Wito huo umetolewa leo mjini Morogoro na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Dorothy Mwaluko wakati akifungua kikao kazi cha siku mbili cha Waratibu wa VVU, UKIMWI na Magonjwa Yasiyoambukizwa (MSY) mahala pa kazi kutoka katika wizara mbalimbali nchini.

Bi. Mwaluko amesema, kukosekana kwa taarifa sahihi za watumishi wenye maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na UKIMWI, kumekwamisha mpango thabiti wa Serikali wa kukabiliana na changamoto ya maambukizi mapya kwa Watumishi wa Umma nchini.

Aidha, Bi. Mwaluko amehoji uhalisia wa takwimu zilizopo sasa za watumishi wa umma 1852 waliobainika kuishi na VVU/UKIMWI iwapo zinatoa taswira halisi ya tatizo lililopo.

Bi. Mwaluko ametoa angalizo kwa waratibu kusimamia vizuri suala la afya za watumishi kwani lina athari kubwa kiutendaji lisiposimamiwa vema.

Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Anuai za Jamii Ofisi ya Rais-Utumishi, Bi. Leila Mavika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Kitaifa inayosimamia utekelezaji wa shughuli za VVU, UKIMWI   na Magonjwa Sugu Yasiyoambukizwa (MSY) mahala pa kazi, amesema kuna mwitikio hafifu wa watumishi wa umma kupima afya zao kwa sababu ya hofu ya kunyanyapaliwa, hivyo amewataka waratibu kuweka mkakati madhubuti utakaowawezesha watumishi hao kuwa huru kujitokeza na kupima afya.

Naye, Katibu wa Kamati Tendaji ya Kitaifa ambaye pia ni Afisa Mwitikio wa taasisi za Umma kutoka TACAIDS, Dkt. Ameir Hafidh, amesema  kuwa Serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 asilimia tisini ya wanaoishi na VVU/UKIMWI watakuwa wametambua hali zao na kuanza kutumia dawa za kupunguza makali kwa usahihi.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE