May 3, 2018

RC TABORA : NI MARUFUKU KUWAKATISHA MASOMO WATOTO ILI WAKAVUNE MAZAO


Image result for RC Tabora 

NA TIGANYA VINCENT
RS TABORA

SERIKALI imesema itawachukulia hatua watu wote ambao watakutwa wakiwatumia watoto kuvuna pamba, tumbaku ,mpunga na mazao mengine jambo linalisababisha kuwa watoro na washindwe kuhudhuria masomo. 

Hatua hiyo imechukuliwa na uongozi wa Mkoa baada ya kutajwa  kuwa miongoni mwa vinara vya wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari wakati wa uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru na Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.

Kauli hiyo ilitolewa jana Wilayani Igunga na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati akionga na Maafisa Watendaji wa Kata, Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule na Walimu wakuu.

Alisema pamoja na sababu ikiwemo la ufugaji vitendo vya kuwatumia watoto kipindi hiki katika kazi mashambani limechangia Mkoa wa Tabora kuwa miongoni mwa maeneo hapa nchini yanayoongoza kwa utoro na mimba za utotoni.

Kufuatia kuwepo kwa vitendo vya utoro Mwanri aliwaagiza viongozi wote kuanzia ngazi za vitongoji kushirikiana na walimu kukabiliana na utoro ambao unarudisha nyuma maendeleo ya watoto na maendeleo ya Mkoa wa Tabora.

Mwanri alisema hatasita kumchukulia hatua kiongozi wa ngazi yoyote kuanzia Kijiji au kitongoji na walimu ambao watashindwa kutekeleza wajibu wao katika kukomesha utoro.

 “Kila mtu ni lazima asimame katika nafasi yake…ukiwa mwalimua hakikisha unafuatilia mahudhurio na kwa wale watoro majina yao yapelekwe kwa Mtendaji wa Kata kwa ajili ya kumchukulia hatua na nakala ya barua hiyo ipelekwe kwa Wakuu wa Wilaya” alisema Mwanri.

Alisema walimu wakuu na Wakuu wa Shule wanapaswa kuhakikisha kilaiku wanachukua orodha mahudhurio na kupeleka majina ya watoto watoro na wazazi wao kwa Watendaji wa Vijiji na Kata ili waweze kuchukuliwa hatua.

Mwanri alisema kwa Watendaji nao wanapaswa kufuatilia watoto ambao hawahudhuri shule na kuwapeleka Mahakamani Wazazi wao kama Waraka wa Elimu wa Mwaka 2002 unavyoagiza.

Naye Katibu Tawala Mkoa Msaidizi anayeshughulikia Elimu Suzan Nussu aliwataka Maafisa Elimu Kata na Wakuu wa Shule na Walimu Wakuu kuhakikisha wanafunzi wote waliondikishwa kujiunga na masomo wanafanya mitihani yao ya kuhitimu  Darsa la saba na wale wa Sekondari wanahitimu Kidato cha Nne.

Alisema hatua hiyo itausaidia Mkoa wa Tabora kuondokana na aibu ya kuwa miongoni mwa Mikoa inayoongoza kwa utoro.

Mthibiti Mkuu wa Ubora wa Shule Kanda ya Magharibi Alvini Mugasha aliwataka wanajamii wanapomuona mwanafunzi akiwa mazingira ya shule wakati wa masomo wamkemee.

Alisema kuwa ni jukumu la walimu kuhakikisha wanachukua orodha ya mahudhurio na kutoa taarifa katika Mamlaka husika ili wazazi wa watoro wachukuliwe hatua za kisheria.

Mapema mwezi uliopita Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizindua mbio za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa Magogo mkoani Geita aliitaja  mikoa ya Tabora, Geita, Mtwara na Shinyanga kuwa inaongoza kwa utoro wa wanafunzi wa sekondari.

Aliongeza kuwa mikoa ya Rukwa, Geita, Tabora, Singida na Simiyu kuwa inaongoza kwa utoro wa wanafunzi wa shule za msingi.
Mwisho

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE