April 2, 2018

RUSSIA KUHUSU KUKWAMA KOMBE LA DUNIA MWAKA HUU


  • Russia yaonya kuhusu njama za Magharibi za kukwamisha fainali za Kombe la Dunia 2018
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Russia, Maria Zakharova amesema kuwa nchi za Magharibi zinafanya jitihada za kuzuia kufanyika mashindano ya soka ya Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Russia na kwamba baadhi ya nchi hizo zinafanya kila liwezekanalo kufikia lengo hilo.
Tangazo hilo la Moscow linaonesha jinsi nchi za Magharibi zinavyofanya juu chini kuidhoofisha Russia. Kabla ya uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 18 mwezi uliopita wa Machi nchini Russia pia nchi za Magharibi zilifanya harakati kubwa za kuzusha machafuko na ukosefu wa amani na kutaka kuzusha hali ya kutoridhika baina ya raia wa nchi hiyo. Hata hivyo ushindi mkubwa wa Vladimir Putin katikia uchaguzi huo ambapo alipata karibu asilimia 77 ya kura zote zilizopigwa lilikuwa pigo kubwa na kufeli kwa njama hizo na propaganda chafu za Marekani, Uingereza na waitifaki wao. Sambamba na kufeli huko nchi za Magharibi zimeshikilia bango la kadhia eti ya kupewa sumu jasusi wa zamani wa Russia nchini Uingereza, Sergei Skripal na binti yake, Yulia.
Sergei Skripal na binti yake, Yulia
Kadhia hiyo inatumiwa kwa ajili ya kuanzisha wimbi kubwa la propaganda chafu dhidi ya Russia na kuifanya nchi hiyo itengwe kimataifa kwa kisingizio kwamba ilihusika katika jaribio la kukata kumuua jasusi huyo wa zamani. Maafisa wa Russia wanasisitiza kuwa, miongoni mwa malengo makuu ya wimbi hilo la propaganda chafu zinazofanyika sasa kabla ya mashindano ya Kombo la Dunia la soka mwaka 2018 nchini Russia ni kuzusha hali ya wasiwasi na hatimaye kutoa wito wa kususiwa mashindano hayo ya kimataifa ya mpira wa miguu. Uingereza ambayo ndiyo kinara wa propaganda hizo chafu dhidi ya Russia imechukua hatua kadhaa katika uwanja huo na kufuatwa na nchi kadhaa waitifaki.
Ni vyema pia kukumbusha kwamba, nchi za Poland, Iceland, Denmark, Sweden, Australia na Japan ambazo zimepata tiketi ya kushiriki katika mashindano hayo zimetangaza kuwa maafisa wao wataungana na Uingereza katika kususia mwaliko wa kushiriki katika sherehe za ufunguzi wa Kombe la Dunia.
Akijibu harakati za Uingereza za kuwataka washirika wake wasusie sherehe hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka la Russia, Nikita Simonyan amesema: "Wamagharibi walikuwa wakidai kuwa michezo inapaswa kutenganishwa na siasa lakini sasa wanatumia Kombe la Dunia la Soka kama silaha ya kisiasa na kipropaganda dhidi ya mataifa mengine."
Moscow inasisitiza kuwa, hadi sasa London imekataa kuonesha ushahidi wowote unaothibitisha kuwa Russia ilihusika katika jaribio la kutaka kumuua Sergei Sripal nchini Uingereza kwa eti kutumia sumu ya kemikali. Mtaalamu wa silaha za kemikali Leonid Rink anasema: Russia haina maslahi yoyote yakuifanya impe sumu Skripal. Katika upande mwingine Moscow isingeweza kuchukua hatua kama hiyo katika kipindi hiki muhimu na nyeti cha kukaribia michezo ya soka la Kombe la Dunia."
Pamoja na hayo inatazamiwa kuwa, hadi wakati wa kuanza mashindano ya mpira wa miguu ya Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Russia, nchi za Magharibi zitaendelea kufanya jitihada kubwa za kutaka kukwamisha au kuvuruga mashindano hayo. Hata hivyo Moscow inaamini kuwa, njama hizo zitafeli na mashindano hayo ya kimataifa yatafanyika kwa mafanikio makubwa.       

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE