March 29, 2018

MKUTANO MKUU WA YANGA KUFANYIKA MAY 5


IMG_8482

Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam
KLABU ya Yanga inatarajiwa kufanya Mkutano wake Mkuu wa mwaka Mei 5 mwaka huu katika ukumbi utakaotajwa baadaye mjini Dar es Salaam.
Mkutano huo ni matokeo ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya Yanga kilichofanyika Jumapili iliyopita mjini Dar es Salaam chini ya Kaimu Mwenyekiti, Clement Sanga ambacho kimewataka wanachama kujindaa kwa ajenda zitakazotangazwa baadaye.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa alipozungumza na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, Jangwani mjini Dar es Salaam.
Mkwasa, mchezaji na kocha wa zamani wa Yanga pamoja na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars amesema kwamba mkutano huo utakuwa maalum kwa wanachama kujadili masuala mbalimbali na kwa ujumla mustakabali wa klabu.
Mkwasa amesema kwamba wanachama wa Yanga wanapaswa kufanya maandalizi ya kuhudhuria mkutano huo sasa kwa kulipa ada za uanachama wao mapema, kwa sababu kwenye mkutano huo ukaguzi mkubwa utafanyika kabla ya watu kuingia ndani ya ukumbi.
“Mkutano utafanyika Mei 5 hapa Jijini Dar es Salaam, wanachama wenye kadi aina zote mbili wataruhusiwa kuingia ukumbuni, kwa maana ya wale wenye kadi za zamani na hizi zinazotolewa sasa kupitia benki ya posta,”amesema Mkwasa, aliyeongozana na Msemaji wa klabu, Dissmas Ten.
Ikumbukwe Yanga imekuwa chini ya Kaimu Mwenyekiti, Sanga kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti, Yussuf Manji Mei mwaka jana.
Kabla ya kufikia maamuzi haya, Manji alipitia kwenye misukosuko na Serikali kuanzia Januari hadi Aprili, kwanza akikamatwa na kuwekwa ndani kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na baadaye akidaiwa kumiliki pasipoti mbili.
Hali hiyo ilisababisha ashindwe kutekeleza majukumu yake ya kiufadhili Yanga na kufanya wachezaji wakose mishahara kwa kipindi chote hicho kabla ya viongozi wenzake kuanza kufanya jitihada za kulipa taratibu.
Lakini kwa ujumla ni udhamini wa SportPesa ndiyo umekuwa mkombozi wa tatizo la kiuchumi la Yanga baada ya Manji kuondoka, ingawa hali ya kifedha bado si nzuri klabu na hilo linatarajiwa kuwa miongoni mwa mambo yatakayajadiliwa Mei 5.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE