March 12, 2018

MBUNGE KUBENEA KWENDA NA HOJA BINAFSI BUNGENI

*TAARIFA KWA WAANDISHI WA HABARI:*

*Ndugu waandishi wa habari;*
Nimefanya haya kwa kutumia Kanuni ya 55 (1) na (2), pamoja na  Kanuni ya 54 (1) (2) na (3) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la Januari 2016.

Uchaguzi huru na haki, hauwezi kufanyika bila kuwapo na chombo huru cha kusimamia na kuendesha chaguzi hizo. Tume ya taifa ya uchaguzi (NEC), iliyopo sasa, siyo chombo huru cha kusimamia uchaguzi. NEC iliyopo sasa, ni janga kwenye nchi.

Na haya siyo maneno yangu pekee. Maneno haya yameelezwa vizuri na wanazuoni mbalimbali, ikiwamo Tume iliyoundwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, mwaka 1991 ili kuangalia mfumo bora wa siasa nchini. Tume hii iliongozwa na aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Francis Nyalali.

Tume ya Jaji Nyalali  ambayo ilikusanya maoni ya wananchi nchi nzima na taarifa yake kupendekeza kuanzishwa kwa demokrasia ya mfumo wa vyama vingi vya siasa, ilipendekeza pia kuanzishwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi.

Taarifa ya Tume ya Jaji Nyalali, ilitoa mifano ya nchi nyingi ambazo Tume zao za uchaguzi sio huru na jinsi ambavyo kukosekana kwa uhuru wa tume hizo, kulivyosababisha madhara makubwa ya mauaji, machafuko na kudidimia kwa ustawi wa nchi hizo.

Katika Ibara ya 591 ya ripoti yake, Tume ya Jaji Nyalali inasema, ni lazima Muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ubadilike ili kukidhi haja ya demokrasia ya vyama vingi na ikaonya watu wakijua kuwa chaguzi zinazofanywa nchini mwao ni za kughushi/bandia basi ni lazima kutatokea machafuko.

Aidha, mwaka 1999, Tume iliyoundwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kuratibu maoni ya wananchi kuhusu Katiba ilipigilia msumali mwingine kuhusu muundo wa sasa wa Tume ya Uchaguzi. Tume hiyo iliongozwa na Jaji Robert Kisanga.
Kwenye ripoti yake, Jaji Kisanga alisema, “hatua ya wajumbe wa Tume kuteuliwa na Rais ambaye pia aweza kuwa kiongozi wa chama cha siasa kinachotawala, katika utendaji wao wa kazi ama watakuwa na upendeleo kwa chama husika au watakuwa wanalipa fadhila kwa aliyewateuwa…”

*Ndugu waandishi wa habari;*
Vilevile, ripoti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyoongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba na hata Rasimu yenyewe ya Katiba iliyoandaliwa na tume hiyo, imeeleza kwa mapana umuhimu wa kubadili muundo wa sasa wa tume ya uchaguzi na kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi. Angalia Ibara ya 190 ya Rasimu ya Jaji Warioba.

Tume ya Jaji Warioba, ilifikia maamuzi hayo, pamoja na mengine, baada ya kumhoji na kumsikiliza kwa makini, aliyekuwa mwenyekiti wa NEC wakati huo, Jaji Damian Zefrin Lubuva.

Mbele ya Tume ya Jaji Warioba, Jaji Lubuva alikiri wakati akitoa maoni ya tume yake kwamba, tume yake siyo chombo huru. Akashauri katika mchakato wa kupata Katiba Mpya, iundwe TUME HURU YA UCHAGUZI ili chombo hicho kipate mwafaka wa kitaifa wa kusimamia mchakato mzima kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, chini ya Katiba Mpya.”

Tume ya Jaji Warioba ambayo iliundwa kwa kiasi kikubwa na watumishi waandamizi wa taasisi za  serikali,  imeeleza hata kwenye utafiti wake, kwamba imebaini kuwa mfumo wa uchaguzi ulipo sasa, pamoja na vyombo vya uchaguzi, vinapingwa au havikubaliki kwa wadau wakuu na muhimu wa uchaguzi.

Tume inasema, kuna kutokuaminiana kwa hali ya juu kuhusu sheria na mfumo mzima wa kitaasisi kwa taasisi zinazosimamia uchaguzi nchini Tanzania.
Utafiti huo umebainisha kwamba uendeshaji wa mifumo ya kiuchaguzi yenye tija inahitaji taasisi endelevu zenye uwakilishi wa kutosha, zenye kutenda haki, na zenye kujitegemea kimamlaka na kimaamuzi.

*Ndugu waandishi wa habari;*
Orodha ya tafiti ni nyingi. Rasimu ya Pili ya Katiba pamoja na Katiba Pendekezwa kwenye ibara za 190 na 211 kwa mfuatano huo, zinaongelea kuhusu kuundwa kwa Tume huru ya Uchaguzi, na jinsi tume hiyo itakavyopatikana.

Nayo taarifa ya awali kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Tanzania oktoba 2015, iliyotolewa na timu ya uangalizi wa uchaguzi ya TEMCO pamoja na ushauri mwingine ilisisitiza:

“…. NEC iliyopewa mamlaka ya kusimamia chaguzi za Jamhuri ya Muungano, wajumbe wake huteuliwa na rais na wanatekeleza majukumu yao kama inavyoelekezwa katika sheria za uchaguzi. Baadhi ya wadau wa uchaguzi hawaridhishwi na sheria zinazotawala chaguzi Tanzania. Kuna hisia na mashaka kuwa sheria zina mapungufu makubwa, zaidi ikiwa:

i. Tume haina mamlaka ya kutosha ya kutekeleza majukumu yake bila upendeleo. Mashaka haya yanatokana na ukweli kuwa Mwenyekiti wa Tume, Makamu wake, Makamishna, na Mkurugenzi wa uchaguzi, huteuliwa na rais ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha siasa na wakati mwingine mgombea katika nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano.

ii. Tume haina wafanyakazi na maafisa wake mahsusi ukiacha wale walioko makao makuu Dar es Salaam. Inategemea kiasi kikubwa wafanyakazi wa serikali ambao huwepo kwa ridhaa ya rais. Utii wa wafanyakazi hawa uko kwa mwajiri wao na sio kwa Tume.
Haya na mengine niliyoyataja, yanathibitisha kuwa Tume ya uchaguzi iliyopo sasa, ina mapungufu makubwa na inaweza kuwa chanzo cha kuingiza nchi kwenye machafuko. Kwamba NEC ya sasa ni janga kwa nchi.
Historia inaonyesha pale ambapo haki hakikutendeka katika chaguzi katika nchi mbalimbali duniani; nchi hizo zilikumbwa na machafuko ya kisiasa na ambayo yaliingiza nchi kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Hatutaki taifa letu lifike huko, ndio maana nimewasilisha hoja hii ya kutaka kuundwa chombo huru kitakachosimamia uchaguzi.

*Ndugu waandishi wa habari;*
Tatizo kubwa lililopo ni kwamba taifa letu liliingia kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa Julai 1992, bila kufanyika kwa mabadiliko makubwa ya Katiba.
Taifa liliingia kwenye mfumo wa vyama vingi kwa kutumia katiba ile ile ya chama kimoja, kwa kuowekewa “viraka” kupitia mabadiliko ya Nane ya Katiba. Eneo pekee lililoguswa kwenye mabadiliko haya, ni sura ya 3 ya Katiba ambako kulifutwa neno “mfumo wa siasa wa chama kimoja” na kuweka maneno “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni taifa linalofuata mfumo wa vyama vingi.” Basi!
Mabadiliko yakaishia kuundwa kwa Sheria Na. 5 ya Vyama vya  Siasa ya mwaka 1992, ili kuwezesha kuandikishwa kwa vyama vya siasa na kufanyia mabadiliko Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (Na.1 ya mwaka 1985), Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa,(Na. 4 ya mwaka 1979) na sheria zinazoendana na matakwa ya chama kimoja; na kuruhusu kufanyika kwa mchakato wa uchaguzi chini ya mfumo wa vyama vingi.

*Ndugu waandishi wa habari;*
Kwa mtazamo wangu na maandiko haya ya wanazuoni, mataifa mengi ambayo viongozi wake au vyama vinavyojitanabaisha kuwa vyama ukombozi wanatumia mbinu ya kutumia mabilioni ya shilingi za walipa kodi kwa ajili ya uchaguzi, huku kwa nyuma wakitumia vyombo vya dola kupanga matokeo.
Mifano mizuri ni uchaguzi wa urais wa mataifa ya Chile mwaka 1988, Poland mwaka 1989, Serbia mwaka 2000 na Ukraine mwaka 2004. Kwingine, ni Burundi, Zimbabwe, Uganda na hapa nchini katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 Tanzania Bara na tangu mwaka 1995, Tanzania Visiwani.

Ushahidi mwingine wa madai haya, ni kile kilichofanyika katika chaguzi ndogo za ubunge katika majimbo ya Kinondoni, Siha na Kata kadhaa nchini. Haya yote yanafanyika kutokana na udhaifu wa Tume zetu za uchaguzi na mfumo mzima wa wa usimamizi wa uchaguzi.

Mathalani, Ibara ya 74(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kwamba;
“Kutakuwa na Tume ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano ambayo itakuwa na wajumbe wafuatao watakaoteuliwa na Rais:-
(a) Jaji wa Mahakama Kuu au Jaji wa Mahakama ya Rufani, ambaye atakuwa mwenyekiti;
(b) Makamu Mwenyekiti ambaye atakuwa mtu anayeshika, aliyewahi kushika au anayestahili kuteuliwa kushika madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu au Jaji wa Mahakama ya Rufani;
(c) Wajumbe wengine watakaotajwa na sheria iliyotungwa na Bunge.

(2) Rais atamteua Makamu wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi kwa kufuata kanuni kwamba endapo Mwenyekiti ni mtu anayetoka sehemu moja ya Muungano, Makamu wake atakuwa ni mtu anayetoka sehemu ya pili ya Muungano.”

Ibara ya 74(7) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 na Kifungu cha 6(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (Na. 1 ya mwaka 1985 na kufanyiwa marejeo mwaka 2010), Mkurugenzi wa Uchaguzi ndiye Katibu wa Tume ambaye pia huteuliwa na Rais.

Sheria hii ya uchaguzi ni ya mwaka 1985, wakati huo Tanzania ilikuwa chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa na hivyo sheria hii ilikuwa mwafaka kwa mfumo wa chama kimoja cha siasa, na kwa mfumo wa sasa kifungu hiki kinatakiwa kibadilishwe ili kutoa uhuru kwa mtendaji huyo.

Kwa mujibu wa Ibara hiyo ya 74 (7) ya Katiba na sheria ya Taifa ya uchaguzi ni dhahiri kwamba Tume ya Uchaguzi iliyopo sasa, haiwezi kuwa huru kwani viongozi wake wakuu ni wateule wa Rais, kwa maana hiyo hata utendaji kazi wake unategemea matakwa ya mamlaka yao ya uteuzi.

Kitendo cha Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kuamua binafsi kufuta uchaguzi wa tarehe 25 Oktoba 2015, Visiwani na matokeo yake, hasa baada ya mgombea wa upinzani, Maalim Seif Sharif Hamad, kuonekana kushinda kwenye uchaguzi huo, ni uthibitisho tosha kuwa vyombo vinavyosimamia uchaguzi, vinaingiliwa na walioko madarakani na hivyo haviko huru.

Mfumo ambao Tume za Uchaguzi zinawajibika moja kwa moja kwa mamlaka za uteuzi, ni nadra sana kwa tume hizo kuwa huru, kwa maana nyingine ni kwamba maana halisi ya demokrasia itakuwa ni ndoto.  Ibara ya 74(14) ya katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema kwamba;
“Itakuwa ni marufuku kwa watu wanaohusika na uchaguzi kujiunga na chama chochote cha siasa, isipokuwa tu kwamba kila mmoja wao atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa katika Ibara ya 5 ya katiba hii.”
Aidha Ibara ya 74 (15) inasema kwamba;
“kwa madhumuni ya Ibara ndogo ya (14) watu wanaohusika na uchaguzi ni;- (e) Wasimamizi wote wa Uchaguzi katika miji na wilaya zote.”
Lakini kwa hali ilivyo sasa, ambapo wakurugenzi walioteuliwa na Mhe Rais ni makada walioshindwa katika kura za maoni ndani ya CCM na wengine ni wale walioshindwa kwenye uchaguzi kupitia CCM; kuwapa dhamana watu hao ambao ni wanachama wa CCM kusimamia uchaguzi, kunakwenda kinyume kabisa na matakwa ya ibara ya 74(14) inayopiga marufuku wasimamizi wa uchaguzi kuwa wanachama wa chama cha siasa.
Katika mazingira kama hayo, tume ya uchaguzi haiwezi kujidai kwamba iko huru kwa kuwa maafisa wake wana mafungamano na chama cha siasa – CCM.

*Ndugu waandishi wa habari;*
Tume ya uchaguzi ni chombo cha kufanya maamuzi. Kama ilivyo kwa mahakama, chombo hiki, huundwa kwa namna ambayo huaminiwa na wadau kuwa viko huru na haviwezi kuwa na upendeleo.

Kwa hivyo kigezo cha kwanza na cha msingi ni namna gani UTEUZI wao unafanyika. Mchakato wa uteuzi unatakiwa uwe huru na wa haki, wa wazi na ulio shirikishi.

Haiwezekani Mwenyekiti na Mtendaji wake Mkuu kuteuliwa kisirisiri na mtu mmoja tu na  ambaye naye ni mgombea mtarajiwa, na chama chake kina wagombea kwa chaguzi ngazi zote, halafu  tume ikatangaza kuwa yenyewe ni tume huru na kwamba haiingiliwi na mamlaka yoyote.

Hivyo kwa kuwa tume ya uchaguzi inaonekana kushindwa kutenda haki katika chaguzi ilizosimamia kutokana na kukosa uhuru wa kimamlaka na kifedha na kutokana na kuwapo kwa kuibuka kwa matukio ya  kiuhalifu wa kiuchaguzi (election fraud) - ambako imeshuhudiwa mgombea fulani anashinda uchaguzi, lakini anayetangazwa ni yule aliyeshindwa; au matokeo ya uchaguzi kutangazwa wakati bado kura zinahesabiwa, nataka kufanyike mambo matatu:

Kwanza, Bunge lijadili na kuazimia kwamba, serikali ilete bungeni Muswada wa Marekebisho ya Katiba ili kuruhusu kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi itakayoitwa, “Tume Huru ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Muswada wa Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi itakayoweka Muundo, Utaratibu wa Upatikanaji wa Wajumbe; Mamlaka ya Tume, Mipaka ya kazi na utaratibu mzima wa kuendesha chaguzi.

Pili, kuanzishwe kwa Mfuko wa Fedha wa Tume Huru ya  Uchaguzi (Tanzania Independent Electoral Commission Fund).

*Ndugu waandishi wa habari;*
Suala hili la Tume Huru ya Uchaguzi, ni kilio cha watu wengi, wakiwamo viongozi wakuu wa serikali, asasi za kiraia na vyama vya siasa. Ni matarajio yangu kuwa  watu wote wenye mapenzi mema na taifa hili, wataunga mkono hoja yangu na hivyo taifa hili kuweza kupata Tume Huru ya Uchaguzi kabla ya uchaguzi wa serikali za Mitaa, vijiji na vitongoji mwaka kesho na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Taifa linataka Tume ya Uchaguzi itakayoweza kusimamia usawa na haki kwa vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi ili kuepusha umwagikaji wa damu ambao unaweza kujitokeza kutokana na Tume kushindwa kusimamia misingi ya usawa katika uchaguzi.

 *Imetolewa leo tarehe 11/03/2018*
*NA:*

*SAED KUBENEA*

*Mbunge Jimbo la Ubungo*

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE