March 21, 2018

HII HAPA TAARIFA YA MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU (THRDC) JUU YA ABDULI NONDO LEO

Wanaharakati wakiwa na wakili wao wa pili kushoto mahakamani Iringa Leo 
..,........................

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeendelea kufuatilia kwa karibu suala la Mwanafunzi Abdul Nondo aliyeshikiliwa na Polisi kwa takribani siku 15. Nondo ambaye pia ni Mtetezi wa Haki za Binadamu na Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) alitoweka mnamo tarehe 6/3/2018 kabla ya kuripoti polisi Iringa taarehe 7/03/2018, kuletwa mjini Dar es Salaam na hatimaye kushikiliwa na polisi kwa zaidi ya wiki mbili. 

THRDC kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) pamoja na TSNP ililazimika kupeleka maombi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ya kumshtaki Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. 

Katika kesi hito wapeleka maombi waliiomba Mahakama iamuru vyombo husika kutoa dhamana kwa bwana Nondo, kumpeleka Mahakamani ili aweze kusikilizwa au kumwachia huru. 

Maombi hayo  ya Jinai Namba 49 ya mwaka  2018 yalipangwa kusikilizwa leo tarehe 21/3/2018 mbele ya Jaji Rehema Sameji.

Wakati Mawakili wa Nondo wakisubiri kusikilizwa kwa kesi hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, walipata taarifa kwamba mteja wao alipelekwa Iringa usiku wa kuamkia leo na hivyo angefikishwa mahakamani asubuhi ya leo mjini Iringa kujibu mashtaka dhidi yake. Mtandao ulianza kufanya mawasiliano ya haraka Mjini Iringa na kufannikiwa kumuweka Wakili (Adv. Luoga) kwa ajili ya utetezi wa kesi hiyo. 

Wakili alifanikiwa kufika katika Mahakama ya  Hakimu Mkazi mjini Iringa, na mnamo majira ya saa nne, Nondo alifikishwa Mahakamani hapo. Katika kesi ya Jinai namba 13 ya mwaka 2018, Jamuhuri imemshtaki Nondo kwa makosa mawili. 

Kosa la kwanza ni Kusambaza Taarifa za Uongo kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao na kosa la pili ni Kumpa taarifa za uongo Mfanyakazi wa umma kinyume na kifungu cha 122(a) cha Kanuni ya Adhabu (Penal Code)

Baada ya taratibu za awali za kimahakama kufanyika, Wakili wa Mshtakiwa  (Wakili Luoga) aliiomba mahakama impe mteja wake dhamana. Hata hivyo Mawakili wa upande wa serikali waliiomba mahakama izuie dhamana kwa sababu za kiusalama za mshtakiwa.  
Baada ya kusikiliza hoja za mawakili hao, Hakimu amezuia dhamana ya mtuhumiwa mpaka Jumatatu ya tarehe 26/03/2018 atakapotoa uamuzi.

Wakati kesi hiyo ikiendelea huko Iringa, kesi iliyofunguliwa awali na THRDC, LHRC na TSNP dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, DCI na IGP imesikilizwa leo katika Mahakama Kuu ya Da es Salaam. Katika kesi hiyo wapeleka maombi wameomba Mahakama itoe amri kwa polisi kumleta Nondo Mahakamani.

 Mawakili wa serikali wameiomba Mahakama waruhusiwe kujibu maombi hayo (Cunter Affudavit), na hivyo Jaji anayesikiliza kesi hiyo Rehema Sameji ameamuru upande wa Jamuhuri kujibu ndani ya siku tatu hadi tarehe 26 March 2018. Baada ya hapo upande wa Wapeleka maombi utajibu na Jaji atatoa maamuzi kuhusu suala la dhamana.

*Imetolewa leo tarehe 21 March, 2018*
*Na:*
*THRDC*

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE