March 5, 2018

BANDARI YA MTWARA KUPOKEA MELI KUBWA ZA PANAMAX

Meli kubwa ya mizigo aina ya Panamax  ambazo

Meli kubwa na za kisasa aina ya Panamax zitaanza kuhudumiwa katika Bandari ya Mtwara mwaka 2019 baada ya kukamilika kwa ujenzi wa gati namba mbili.


Gati hili linalokadiriwa kugharimu Sh137 bilioni linajengwa kwa ubia wa kampuni mbili za Kichina za China Railways Major Bridges Engineering Group Co. Ltd (CRMBEG) na China Railways Construction Engineering Group (CRCEG) chini ya usimamizi wa Kampuni ya Ujerumani ya Inros Lackner.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Makame Mbarawa ameagiza kukamilika haraka kwa ujenzi wa mradi huo ili kuwezesha meli hizo kutia nanga bandarini hapo.


“Mradi una maana kubwa kwa upande wa Serikali na TPA (Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari), kwa ujumla na tunahitaji ukamilike kwa haraka ili kuongeza ufanisi wa Bandari ya Mtwara,” amesema.


Profesa Mbarawa amesema ujio wa meli hizo katika Bandari ya Mtwara ni faraja kubwa kwa wana Mtwara, kwani zitachochea kukua kiuchumi kwa mkoa na kuongeza mapato ya Serikali.


Katika kuhakikisha mradi wa ujenzi wa gati hiyo unakamilika kwa wakati, Profesa Mbarawa ameitaka TPA kusimamia mradi huo ili ukamilike kwa wakati kama ulivyopangwa.


Ameahidi kurudi tena Bandari ya Mtwara kukagua mradi huo ndani ya miezi mitatu, ili kuona maendeleo ya ujenzi na jinsi muda wa kukamilika kwa mradi huu unavyozingatiwa.


Naye kaimu mkurugenzi mkuu wa TPA, Karim Mattaka amesema kwamba ujenzi wa gati namba mbili umefikia asimilia 15.


“Kwa sasa mradi wa ujenzi wa gati namba mbili ya Bandari hii ya Mtwara umefikia asilimia 15, upo katika hatua ya mwisho mwisho ya usanifu wa gati lenyewe,” amesema Mattaka.


Mattaka amesema wao kama TPA wameyapokea maagizo ya waziri kwa ajili ya utekelezaji na watamsimamia mshauri na mkandarasi kwa karibu zaidi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.


Mkuu wa Bandari ya Mtwara, Nelson Mlali amesema mradi huu ni ukombozi kwa mikoa ya kusini na Tanzania kwa jumla.


 Mlali amesema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza uwezo wa Bandari ya Mtwara, kwa kuwa bandari hiyo ilishafikia asilimia 93 ya uwezo wake wa kuhudumia shehena.


Kuhusu ujio wa meli, mkuu huyo wa bandari amesema kwa kipindi cha miezi minane (Julai 2017 hadi Februari 2018) meli 61 zilihudumiwa. Kati ya hizo, 45 ni za kimataifa na 16 za mwambao.


Bandari ya Mtwara ni kati ya bandari tatu kubwa zilizopo katika ukanda wa Bahari ya Hindi, ina uwezo wa kuhudumia makasha 200,000 TEUs na shehena mchanganyiko za tani laki nne kwa mwaka.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE