February 12, 2018

WAZIRI MKUU AMJULIA HALI MWENYEKITI WA CWT SINGIDA

 
 WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtembelea na kumpa pole Mwenyekiti wa Chama Cha Walimu (CWT) mkoa wa Singida Mwalimu Aron Jumbe aliyelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Akiwa hospitalini hapo leo (Jumamosi, Februari 10, 2018), Waziri Mkuu amefarijika baada ya kumkuta Mwenyekiti huyo na wagonjwa wengine waliolazwa kwenye taasisi hiyo wakihudumiwa vizuri.
 
Pia Waziri Mkuu amewajulia hali mabinti pacha walioungana Consolata na Maria Mwakikuti ambao nao wamelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
 
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwapa pole wagonjwa hao na kuwaeleza kwamba Serikali inadhamira ya dhati kuhakikisha inaboresha huduma za afya na kwamba madaktari wataendelea kuwahudumia vizuri ili kuhakikishia afya zao zinaimarika na kurejea katika shughuli zao za kila siku
 
Kwa upande wake, Mwalimu Jumbe alimshukuru Waziri Mkuu kwa kutenga muda wake na kwenda kumjulia hali. Aliwashukuru madaktari na wauguzi wa taasisi ya JKCI kwa huduma nzuri wanazompatia tangu alipofika hospitalini hapo.
 
Kwa upande wao Maria na Consolata walishukuru kwa msaada wa huduma za matibabu wanazozipata na kwa sasa wanaendelea vizuri. Pia walimshukuru Waziri Mkuu kwa kwenda kuwajulia hali na kumtakia kheri katika shughuli zake
 
 (mwisho)

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE