
Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Serikali inaendelea na mpango wa
kuhamasisha ulimaji wa mazao makuu matano ya Pamba, Korosho, Tumbaku,
Kahawa na Chai nchini ili kuongeza uzalishaji wa mazao hayo.
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa
ameyasema hayo leo Bungeni Mjini Dodoma wakati wa maswali kwa Waziri
Mkuu alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Sumve Mhe. Richard Ndassa juu
ya namna Serikali ilivyojipanga na utafutaji wa masoko ya Pamba kutokana
na mwitikio mkubwa wa kulima zao hilo mwaka huu.
“Miongoni mwa mikakati ya
kuendeleza mazao hayo ni pamoja na kulima kisasa na kutafuta masoko
ndani na nje ya nchi,” alisema Waziri Mkuu.
Amesema, mwezi huu anatarajia
kukutana na watumiaji wa zao la Pamba hapa nchini ili kuweka mfumo
endelevu wa ununuzi wa zao hilo. Aidha, Wizara ya Kilimo inafanya kazi
ya kutafuta masoko nje ya nchi.
Pia, Mhe. Majaliwa alipokuwa
akijibu swali la Mbunge wa Liwale Mhe. Zuberi Kuchauka juu ugawaji wa
pembejeo za korosho kwa mwaka huu amesema, Serikali ilitoa pembejeo ya
Salfa bure mwaka jana kwa wakulima wa korosho ili kufanya hamasa kwa zao
hilo baada ya wakulima kutelekeza zao hilo kutokana na kukosa pembejeo
hiyo.
“Baada ya ugawaji wa pembejeo hiyo
ya Salfa zao hilo limevunwa kwa kiwango cha juu kwa mwaka jana, hivyo
kutokana na fedha walizozipata wakulima wa zao hilo watatatikiwa
kuchangia gharama za Salfa kwa mwaka huu,” alisema Mhe. Majaliwa.
Wakati huo huo, Mhe. Kassim
Majaliwa alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Urambo Mhe. Margaret Sitta
juu ya migogoro ya mipaka ya mapori na misitu, amesema Serikali
imeiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kushirikisha wanavijiji na
viongozi wa kijiji wakati wa uwekaji wa mipaka hiyo.
Hata hivyo amesema ikiwa kijiji
kitaonekana kiko ndani ya mipaka ya msitu au pori, tathimini itafanyike
na baadae watapewa elimu ya kutoingia ndani ya mipaka ya misitu na
mapori ya Serikali Kuu.
Misitu yote ya Serikali Kuu inahifadhiwa kisheria na mipaka hiyo inaonekana ili kuondoa migogoro na wananchi.
0 comments:
Post a Comment
AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE