February 22, 2018

WATOTO WALIOUNGANA KENYA WAANZA MASOMO


Image result for WATOTO WALIOUNGANA MBEYA
By Godfrey Kahango,


Kyela. Unawakumbuka wale watoto pacha Eliud na Elikana Mwakyusa? Wale wakazi wa Kasumulu – Kyela, Mbeya ambao walizaliwa wakiwa wameungana kiunoni wakatenganishwa nchini India? Ni kwamba juzi walitimiza miaka mitano ya kuzaliwa huku wakisubiri kufanyiwa upasuaji mdogo wa tatu.


Walizaliwa Februari 20, 2013, wilayani Kyela na Serikali ikawapeleka India ambako baada ya madaktari bingwa kuwatenganisha, waliwatengenezea sehemu mbili maalumu ya kutolea haja kubwa na ndogo tumboni kisha wakarejea Kasumulu Kyela, Februari 27, 2014.


Agosti 2014, watoto hao walifanyiwa upasuaji mwingine mdogo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN) na Hospitali ya Rufaa – Mbeya kwa nyakati tofauti wa kuziba haja kubwa ya muda na kuwatengenezea haja ya kudumu chini ya daktari bingwa wa upasuaji kitengo cha watoto Muhimbili, Zaituni Bokhary. Sasa kazi iliyokuwa imebaki ni upasuaji wa kuwawezesha kuwekewa sehemu ya haja ndogo ya kudumu.Watimiza miaka mitano


Walitimiza miaka mitano ya kuzaliwa juzi Jumanne huku wazazi wao wakisema wana furaha tele kuwaona wakiwa wenye afya na furaha tele. Hawakusita kuishukuru Mwananchi Communications Ltd (MCL), ambayo waandishi wake ndio waliosambaza habari ya kuzaliwa kwao.


Juzi mchana, baba mzazi wa watoto hao, Erick Mwakyusa alisema licha ya kuwa na afya njema, bado wanakabiliwa na tatizo la kutokwa na haja kubwa na ndogo bila kujitambua.


“Wanatoka chekechea muda huu... kwa kweli tunamshukuru Mola katika hili. Changamoto kubwa iliyopo ni hili tatizo la kutokwa na haja kubwa na ndogo bila ya kujitambua. Bado wanasubiri upasuaji wa haja ndogo kwa kuziba ile waliyowekewa ya muda ili wawekewe ya kudumu.


“Tofauti na hilo kwa kweli wapo vizuri, tunamshukuru Mola hawana zile homa za watoto za mara kwa mara, wanatembelea vizuri, wanazungumza kwa kweli katika hili tunawashukuru sana Mwananchi kuendelea kufuatilia maendeleo ya wanetu.”


Alisema sasa anatafuta fedha za usafiri, malazi na matibabu ili arudi Muhimbili kwa ajili ya upasuaji huo, “niliongea na Dk Bokhary Desemba mwaka jana kuhusu upasuaji mwingine akaniambia ninatakiwa nijipange kisawa sawa maana kwa sasa gharama ya matibabu pale Muhimbili imekuwa kubwa. Hivyo nipo kudunduliza fedha na nimepanga Juni mwaka huu niende maana ukiangalia uchumi wenyewe unasumbua na sina kitega uchumi kingine zaidi ya bodaboda.”


Kuhusu matunzo kutokana na hali yao mama wa watoto hao, Grace Joel alisema anajitahidi kuzingatia maagizo ya Dk Bokhary ya kuwazoesha kwenda choo na kuwaweka safi muda wote.Waanza chekechea


Grace anasema Januari mwaka huu, Elikana na Eliud walianza masomo ya awali katika shule iliyopo karibu na nyumbani kwao ili kuwa karibu nao kwa jambo lolote linaloweza kuwatokea hususan la usafi wakisaidiana na walimu. Grace alisema tangu waanze shule hawajapata shida yoyote na wameshazoea kuamka mapema asubuhi wenyewe wakisubiri kuandaliwa kwenda shule na mchana wamekuwa wakirudi wenyewe bila kufuatwa kwa vile wameshazoeana na wenzao.Walimu walonga


Elikana na Eliud wanafundishwa na walimu Tumaini Mwasamya na Scola Kaminyoge ambao wanasema watoto hao wapo vizuri darasani kwani ni wepesi kukariri wanachoelekezwa na kufundishwa.


“Tulishaelezwa tatizo lao na wazazi wao hivyo tunakuwa nao karibu sana muda wote kuwaangalia na tukiona kama ni mkojo tu basi tunawasafisha na kama wanahitaji kubadili nguo inapobidi kumuita mama yao tunafanya hivyo. Na mama yao anajitahidi sana usafi kwa hawa watoto kwa hili tunampongeza sana,” alisema Mwalimu Mwasamya.


“Hawa watoto wana akili sana maana wameanza Januari 14, lakini sasa hivi wanajua kidogo kuandika na kuhesabu pia. Wanapenda sana kucheza na wenzao lakini ukiwakanya tu wanasikia na kuacha kisha wanarudi darasani.” Mwalimu Kaminyoge akikumbuka jinsi walivyozaliwa alisema, “Unajua ni miujiza ya Mola tu, maana watu wengi mtaani wanashangaa kuwaona wapo shule. Hawakutarajia kutokana na historia yao, hadi wengine wanatuulizia eti Elikana na Eliud wanasoma hapo kwenu? Na tunawaambia ndio tena wana akili sana darasani.”

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE