February 2, 2018

WATOTO WA MARAIS WENYE USHAWISHI DUNIANI


WENGI wamezoea kuwaona mabinti wa marais kwa mtazamo tofauti kwamba ni watoto wenye kudeka, kutokujituma kwa sababu wazazi wao wamefikia levo ya kuwafanyia chochote.
Lakini ukija kwa upande wa pili, wapo baadhi ya mabinti wa marais ambao wamekuwa na ushawishi mkubwa kwa jamii kupitia kazi zao wanazozifanya sambamba na kuwasaidia wazazi wao.
Katika makala hii fupi wapo baadhi ya mabinti wa marais wa Urusi, Tajikistan, Angola, Cuba na Uturuki wenye ushawishi duniani;

KATERINA TIKHONOVA, URUSI
Ni binti wa Rais wa Urusi, Vladimir Putin wa Urusi ambaye ni mchezaji maarufu wa mashindano ya dansi ya Rock and Roll.
Anatajwa kuwa na utajiri wa dola bilioni mbili kupitia uwekezaji katika gesi na viwanda vya petroli itokanayo na kemikali.
Sasa ana umri wa miaka 30, na anaendesha miradi ya umma ya maendeleo ya elimu katika Chuo Kikuu cha Moscow.
Anaripotiwa kusimamia mikataba yenye thamani ya mamilioni ya dola na washauri wake ni washirika wa karibu baba yake.

BI DOS SANTOS, ANGOLA
Ni mtoto wa kwanza wa rais mkongwe wa Angola, Jose Eduardo dos Santos, ambaye ametawala nchi hiyo tangu 1979.
Anaongoza kampuni ya taifa ya mafuta -Sonangol na mwaka 2013 Jarida la Forbes lilibainisha kuwa ndiye mwanamke tajiri zaidi barani Afrika na mwanamke wa kwanza bilionea (kwa dola za Marekani) akikadiriwa kuwa na mali ya thamani ya dola Bilioni 3.2.

SUMEYYE ERDOGAN, UTURUKI
Binti wa rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan ambaye ameolewa na mfanyabiashara maarufu nchini humo.
Sumeyye mwenye umri wa miaka 31, ni binti mdogo zaidi wa rais wa Uturuki aliyesomea siasa katika mataifa ya Marekani na Uingereza.
Amekuwa mshauri wa baba yake alipoongoza chama tawala cha Haki na Maendeleo (AKP) na amekuwa akimsindikiza baba yake mara kadhaa katika mikutano mbalimbali ya kidiplomasia duniani. Mwaka 2015 kulikuwa na fununu kwamba huenda Sumeyye atawania ubunge, lakini hakufanya hivyo.

OZODA RAHMON, TAJIKISTAN
Ni mmoja kati ya watoto tisa wa Rais wa Tajikistan, Emomali Rahmon.
Ana Shahada ya Sheria na alianza taaluma yake katika huduma za kibalozi, kabla ya kuwa naibu waziri wa mambo ya nje mwaka 2009.
2016 baba yake alimteua kuwa mkuu wa utawala katika ofisi ya rais na akashinda kiti cha bunge la Seneti.
Ndiye pekee katika familia ya Rahmon mwenye kazi ya serikali.

MARIELA CASTRO, CUBA
Ni mpwa wake hayati kiongozi mwanamapinduzi Fidel Castro wa Cuba.
Mariela anaongoza kituo cha kitaifa cha elimu ya ngono (Cenesex), kinachodhaminiwa na serikali mjini Havana ambacho kimekuwa na mchango mkubwa katika kubuni sera juu ya masuala kadhaa kuanzia kudhibiti HIV na Ukimwi hadi haki za wapenzi wa jinsia moja.
Alikuwa kiungo muhimu katika kampeni za kupitishwa kwa sheria mpya mwaka 2008 iliyowezesha utoaji bure wa huduma ya kubadilisha jinsia nchini Cuba.
Na Mwandishi Wa Global

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE