
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, DODOMA
Serikali imewataka wananchi kutoa
taarifa kuhusu hospitali zinazotoza fedha kwa ajili ya matibabu kwa
akina mama wajawazito ili kuweza kuchukua hatua muhimu kukomesha hali
hiyo.
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni
Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee
na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti
Maalumu Hawa Chakoma lililohusu matibabu bure kwa mama wajawazito.
Dkt. Ngugulile amesema kuwa mama
wajawazito ni moja ya makundi maalumu wanaostahili kupata huduma za
matibabu bure kama ilivyooneshwa katika mwongozo na uchangiaji wa huduma
za afya wa mwaka 1997.
“Mwongozo umeweka bayana kuwa kina
mama wajawazito ni haki yao kupewa huduma zote bila malipo na sio zile
tuu zinazohusu huduma za ujauzito katika mwongozo uliopitiwa mwaka
2009/2010 imetamkwa bayana kuwa huduma za afya kwa mama wajawazito ni
bure, ikiwa na maana kwamba mara tu mwanamke anapokuwa na ujauzito
huduma zote kuanzia kliniki ya wajawazito, pale anapogundulika maradhi
yoyote, pamoja na huduma ya kujifungua sanjali na kumuona daktari,
kupatiwa vipimo, kupewa dawa na kufanyiwa upasuaji pale inapohitajika
kufanya hivyo” amefafanua Dkt. Ndugulile.
Aidha, Dkt. Ndugulile amesema kuwa
Wizara imeanzisha utaratibu wa kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa
vifaa vinavyohitajika wakati wa kujifungua ambapo watapewa akina mama
wajawazito wanapokaribia kujifungua.
Hata hivyo, Dkt Ndugulile amesema
kuwa kwa sasa kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa akina mama kujifungua
katika vituo vya afya ambapo zaidi ya asilimia 60 ya akinamama
wanajifungulia kwenye vituo vya afya.
Mbali na hayo, Serikali imezitaka
Halmashauri zote nchini kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sera hiyo
ili akina mama wajawazito wapate huduma za matibabu bure kama Mwongozo
wa Uchangiaji wa mwaka 1997 na Sera ya Afya ya mwaka 2007 inavyoelekeza.
0 comments:
Post a Comment
AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE