February 9, 2018

OLIMPIKI YA MAJIRA YA BARIDI YAANZA NCHINI KOREA KUSINI

Michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi inaanza Ijumaa huko Korea Kusini katika mji wa Pyeongchang na sherehe ya ufunguzi itaonesha jinsi nchi hiyo ilivyojikwamua kutoka kwenye umaskini.
Michezo hii imeanza baada ya majaribio mawili, matayarisho yaliyogharimu mabilioni ya dola na mjadala wa kitaifa wa iwapo kuna umuhimu wake nchini humo. Kwa kipindi cha wiki mbili mji wa Pyeongchang utakuwa mwenyeji wa michezo ya majira ya baridi na pengine maridhiano baina ya Korea Kusini na Korea Kaskazini.
Kutakuwa na mengi ya kutazama kwa wapenzi wa michezo ya majira ya baridi ambayo kawaida inafanyika mara moja katika kila miaka minne. Lakini upande wa riadha wa michezo hii umefunikwa na siasa zinazoendelea baina ya majirani hawa wawili wa Korea. Nchi hizo ambazo zimekuwa zikipeana vitisho vya vita wiki chache tu zilizopita kwa sasa zinajaribu kuonesha ushirikiano.
Kuwasili kwa ujumbe wa Korea Kaskazini kumezusha maandamano
Rais wa Korea Kaskazini Moon Jae-In alikutana Ijumaa na kusalimiana kwa kushikana mikono na kiongozi wa ujumbe wa ngazi ya juu ya Korea Kaskazini katika michezo hiyo, Kim Yong Nam kabla ya ufunguzi rasmi wa michezo hiyo. Ujumbe huo uliwasili kwenye michezo hiyo akiwemo dada wa kiongozi wa taifa hilo, Kim Jong Un.
Südkorea Präsident Moon Jae (R) trifft Kim Yong Nam, Präsident von Nordkorea (picture-alliance/Yonhap) Rais wa Korea Kusini Moon Jae-in na Kim Yong Nam wa Korea Kaskazini
Lakini kuwasili kwa ujumbe huo wa Korea Kaskazini kulizusha maandamano katika mji wa Pyeongchang huku raia wakipinga kujumuishwa kwa taifa hilo katika michezo hiyo.
"Hatukubali michezo hii ya Olimpiki ambayo imechafuliwa na kushiriki kwa Korea Kaskazini. Hatutaki kuwa nchi ya kikomunisti, rais wetu anataka kuibadilisha nchi yetu iwe nchi ya kikomunisti sasa. Kwa hiyo tuko hapa kwa sababu tunaitaka nchi yetu," alisema mmoja wa waandamanaji Thasik Park.
Michezo hiyo haitotumiwa kuzungumza na Korea Kaskazini
Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence pia yuko Pyeongchang kwa sherehe hizo za ufunguzi wa michezo hiyo na anatumia uwepo wake kuitaka jamii ya kimataifa kuiwekea shinikizo zaidi Korea Kaskazini katika mpango wake wa nyuklia na masuala ya ukiukaji wa haki za binadamu.
Nordkorea Kim Yo-Jong (picture alliance/AP Photo/Wong Maye-E) Dada wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, Kim Yo Jong, kulia
Baada ya kufanya mikutano na Rais wa Korea Kaskazini Moon Jae-in na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe, Pence alisema hakuna nafasi ya kuitumia michezo hiyo kama njia ya kufanya mazungumzo na Korea Kaskazini hadi pale mpango wake wa nyuklia utakapokuwa sehemu ya hayo majadiliano.
Korea Kaskazini kawaida ina tabia ya kuhakikisha kwamba uwepo wake unatambulika inapokuwa sehemu ambapo ipo pamoja na mahasimu wao Korea Kusini. Na inasubiriwa kuonekana katika michezo hii iwapo jambo hilo litaonekana au ile kauli ya Korea Kusini iliyoifanya kupata nafasi hiyo ya kuwa mwandalizi kwamba michezo hiyo itachangia kupatikana kwa amani katika Rasi ya Korea.
Lililo wazi lakini ni kwamba michezo hii ikilinganishwa na michezo mingine katika miaka ya hivi karibuni ni zaidi ya michezo tu kwani kuna siasa ndani yake.
Mwandishi: Jacob Safari/APE/AFP

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE