February 21, 2018

Makundi ya kiraia Tanzania yaomba kuundwe tume ya kuchunguza mauaji


 Viongozi wa makundi ya kiraia
Makundi ya kiraia nchini Tanzania yametoa wito wa kuundwa kwa tume huru ya kuchunguza vifo ambavyo vimetokea karibuni nchini humo.

Viongozi wa Asasi za Kiraia (Azaki) wamesema tume hiyo inafaa kuwashirikisha maafisa wa AZAKI, Taasisi za Dini, Vyombo vya Habari, Baraza la Vyama vya Siasa, Wanahabari, Majaji/Mahakimu, Polisi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora.

Maafisa wa Azaki wamesema uchunguzi huru unahitajika juu ya vifo na vitendo vya utekwaji na utesaji vilivyojitokeza wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni.

Aidha, wameomba askari wanaotuhumiwa kuhusika kusababisha kifo cha Mwanafunzi Akwilina Akwiline wafikishwe katika vyombo vya sheria ili hatua stahiki zichukuliwe kwa aliyehusika na tukio hilo.

"Taifa liwe na mfumo huru au chombo huru ya kuchunguza na kusimamia mashtaka yanayohusu vyombo vya usalama badala ya kuwaachia wao kufanya uchunguzi na kuendesha mashtaka," wamesema.

"Matukio yanayowahusu Polisi kama watuhumiwa ni kosa kubwa kuwaachia wao wenyewe wajichunguze na hili limekuwa sasa chanzo cha matukio kuendelea kutokea na kutochukuliwa hatua."

Maafisa hao wa kutetea haki za kibinadamu wamesema hali nchini Tanzania inasikitisha.
"Watetezi wa Haki za binadamu wameendelea kufanya kazi katika mazingira ambayo sio rafiki na hatarishi huku wengi wao wakifunguliwa kesi, kushambuliwa, kukamatwa na vyombo vya Dola ikiwemo kupewa majina mabaya na hata kuzushiwa kuwa baadhi yao sio raia wa Tanzania," wamesema.

"Makundi mbali mbali na Asasi za kiraia zimeendelea kufanya kazi katika mazingira ambayo sio rafiki huku uhuru wao wa kufanya kazi na kujieleza ukiwa umeminywa kinyume na Katiba."

Viongozi hao wa Azaki wametoa wito kwa Serikali itazame upya suala la upatikanaji wa Katiba mpya wakisema "ndiyo suluhisho la matatizo mbali mbali yanayotokea katika jamii kwa sasa."
Aidha, wameomba kuundwe Tume Huru ya Uchaguzi kabla ya uchaguzi wa 2019 na 2020.

Visa vya mauaji ya kutoweka kwa watu Tanzania

  • Mauaji ya Kibiti mwaka 2017: Viongozi wa CCM, askari zaidi ya 10 na wananchi karibu 40 katika eneo la Kibiti walishambuliwa na kuuwawa na watu wasiojulikana.
  • 11 Februari, 2018 Kiongozi wa Chadema Daniel John alitekwa na kisha aliuwawa kikatili wakati wa Kampeni za Uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni.
  • Mnamo 7 Septemba, 2017, Mnadhimu Mkuu wa upinzani bungeni, mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu alipigwa risasi na watu wasiojulikana katika eneo la Area D Mkoani Dodoma. Bw Lissu pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika.
  • 21 Novemba, 2017 Mwandishi wa habari wa Mwananchi Communications Limited Azory Gwanda alipotea katika mazingira ya kutatanisha na mpaka sasa hajapatikana.
  • Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema Ben Saanane alipotea katika mazingira ya kutatanisha na mpaka sasa hajulikani alipo.
Kuuawa kwa mwanafunzi Akwilina
Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Akwilina Baftah aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa katika daladala askari polisi walipokuwa wakiwatawanya wafuasi wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mnamo 16 Februari.

Wafuasi hao walikuwa wanakwenda kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kinondoniambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa ajili ya kudai fomu za mawakala wa uchaguzi.
Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa, lilithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kukiri kwamba tukio hilo limetokea wakati polisi wakiwa wanafyatua risasi angani kuweza kuwatawanya wafuasi wa Chadema.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE