February 22, 2018

Israel yawasweka jela wakimbizi wa Kiafrika

 Israel yawasweka jela wakimbizi wa Kiafrika
Israel imewafunga jela Waafrika 7 raia wa Eritrea walioomba hifadhi katika utawala huo baada ya wakimbizi hao kukataa kupelekwa Rwanda kwa mabavu.

Taasisi za kutetea haki za binadamu huko Israel zimeripoti kuwa, wakimbizi hao wa Kiafrika wamefungwa katika gerezani la Israeli kwa muda mrefu usiojulikana baada ya kukataa kupelekwa Rwanda.

Wakimbizi hao ni wa kwanza kufungwa jela tangu utawala haramu wa Israel utangaze kwamba, utawalazimisha maelfu ya wakimbizi wa Kiafrika kuchagua ama kuhamishiwa katika nchi nyingine au kufungwa jela kwa muda mrefu usiojulikana.

Taarifa iliyotolewa na taasisi mbili za kutetea haki za wakimbizi zenye makao yao mjini Tel Aviv za Hotline for Refugees and Migrants na ASSAF imesema: 

"Hii ni hatua ya kwanza ya operesheni ya kuwahamisha kwa mabavu wakimbizi kimataifa ambayo haina mfano wake, na ni hatua inayochochewa na ubaguzi na kudharau uhai na utukufu wa watu wanaotafuta hifadhi."


Taarifa hiyo imeongeza kuwa, wawili kati ya wakimbizi hao saba wa Kiafrika ambao wamefungwa katika jela ya Saharonim huko Israel ni manusura wa mateso.

Wakati huo huo mamia ya wakimbizi wanaotafuta hifadhi huko Israel walianza mgomo wa kula chakula jana Jumatano katika kituo cha Holot wanakozuiliwa wakimbizi hao. Wakimbizi hao wanapinga kitendo cha utawala wa Kizayuni wa Israel cha kuwafunga jela wenzao saba kutoka Eritrea.

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa, wakimbizi 27,000 kutoka Eritrea na wengine 7,700 kutoka Sudan wameomba hifadhi huko Israel.

Novemba mwaka jana utawala haramu wa Israel ulitangaza kwamba, utawasafirisha wakimbizi walioko katika utawala huo kwa mabavu na kuwapeleka nje.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Isarel, wakimbizi hao wanapelekwa kwa mabavu na bila ya hiari yao katika nchi za Rwanda na Uganda ingawa nchi hizo mbili zimekanusha kuwa zimefikia makubaliano ya aina hiyo na utawala haramu wa Israel.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE