December 2, 2017

WIKI YA MSAADA WA KISHERIA YAZINDULIWA

PIX1b
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Amon Mpanju akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Wiki ya Msaada wa Kisheria leo Jijini Dar es Salaam. Wiki hii ya Msaada wa Kisheria inatarajiwa kuanza tarehe 04 Desemba 2017 ambapo kitaifa itafanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Mashirika yanayotoa Huduma ya Msaada wa Kisheria Tanzania (TANLAP), Bi. Christina Kamili na Kaimu Msajili Msaada wa Kisheria toka Wizara ya Katiba na Sheria Bibi. Felista Joseph.
PIX2
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Mashirika yanayotoa Huduma ya Msaada wa Kisheria Tanzania (TANLAP), Bi. Christina Kamili akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) walipokuwa wakiongea kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria inayotarajiwa kuanza tarehe 04 Desemba katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.Kutoka kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Amon Mpanju na Kaimu Msajili Msaada wa Kisheria toka Wizara ya Katiba na Sheria Bibi. Felista Joseph.
PIX3
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano baina yao na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Amon Mpanju (hayupo pichani) alipokuwa akizungumzia Maadhisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria leo Jijini Dar es Salaam.
(Picha na: MAELEZO
……………
Wizara ya Katiba na Sheria, Wadau wa Maendeleo na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yanayojishughulisha na utoaji wa huduma ya Msaada wa kisheria nchini tunatarajia kuwa na maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria nchini kuanzia tarehe 4 hadi 8 Disemba. Maadhimisho haya yanaenda na kauli mbiu isemayo Msaada wa kisheria kwa maendeleo ya Wananchi.
Kitaifa maadhimisho hayo yatafanyika jijini Dar es Salaam katika Viwanja vya Mnazi Mmoja ambapo Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi atayazindua rasmi na kuzungumza na wananchi juu ya umuhimu wa msaada wa kisheria kwa wananchi.
Maadhimisho hayo pia yatafanyika katika  kikanda zote za Tanzania Bara  ambapo katika Kanda ya Kaskazini yatafanyika mkoani Arusha, Kanda ya Kati yatafanyika mkoani Dodoma, Kanda ya Ziwa yatafanyika mkoani Mwanza, Kanda ya Magharibi yatafanyika mkoani Kigoma, Kanda ya Kusini yatafanyika mkoani Mtwara na Kanda ya Nyanda za Juu Kusuni yatafanyika mkoani Rukwa.
Lengo kubwa la maadhimisho haya ni kutoa elimu kwa umma juu ya uwepo wa Sheria ya Msaada wa Kisheria. Pia Maadhimisho hayo yatajikita katika utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi pamoja na kuwatembeleea wale walioko katika vituo vya Polisi na Magerezani ili kuwapatia huduma hiyo pale walipo.
Katika maadhimisho Mawakili wa kujitegemea, Wasaidizi wa Kisheria na Wanasheria kwa ujumla wataungana pamoja na kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa jamii ili kuhakikisha jukumu la upatikanaji haki kwa wananchi linafanikiwa.
Kupitia maadhimisho ya wiki hiyo, Serikali inawajulisha wananchi wote kuwa msaada wa kisheria ni haki yao kwani ni haki ya kila binadamu kama ambavyo imeelezwa bayana katika Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inavyoeleza na Serikali kupitia Sheria ya Msaada wa Kisheria ya 2017 tumeamua kulisimamia, kuliratibu na kutekeleza jukumu hilo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Maadhimisho hayo pia yatatumika kama jukwaa la wataalamu hawa wa sheria nchini kurudisha kwa jamii kile ambacho wataalamu hao wamepata kupitia kazi, elimu na ujuzi wao kwa kutoa msaada wa kisheria ambalo ni suala la msingi sana katika maendeleo.
Nitoe rai kwa wananchi wenye uhitaji wa huduma hii waje kwa wingi ambapo kila mtu atasikilizwa  na atashauriwa  katika masuala mbalimbalia ya kisheria kadiri ya mahitaji yake.
Nichukue nafasi hii kuwaambia Watanzania kuwa huduma hiyo haitoishi katika wiki hii ya maadhimisho, bali huduma hii ipo na imekuwa ikitolewa na Serikali na mashirika mbalimbali ya watoa huduma ya msaada wa kisheria nchini hivyo ni jukumu la wananchi kuwatembelea watoa huduma hawa ili kuweza kupata huduma ya msaada wa kisheria.
Kama kauli mbiu ya maadhimisho haya inavyosema kuwa Msaada wa kisheria kwa maendeleo ya Wananchi, nami pia niwaambie Watanzania wote kuwa msaada wa kisheria ni haki yenu muiamini na muitumie.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Amon Mpanju
Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Katiba na Sheria
02 Disemba, 2017

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE