JITIHADA za utendaji kazi za waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi kupitia wizara yake zimeendelea kuwa ukombozi kwa wananchi wanyonge kwani baada ya waziri kutoka Dodoma kumaliza mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 10 kwa kupokonya ardhi iliyowekezwa bila utaratibu toka kwa mwekezaji sasa waziri Lukuvi amefanikiwa kutatua mgogoro wa zaidi ya miaka mitano ulikuwa ukiwatesa wananchi wa mtaa wa Vingunguti jijini Dar es Salaam baada Mwekezaji wa Kampuni ya PMM kutaka kujimilikisha ardhi na nyumba za wananchi bila utaratibu .
Akizungumza na wakazi wa Vingunguti leo katika mkutano uliotishwa na Waziri huyo kutaka kujua hatma ya nyumba za wakazi na maeneo hayo wanayoishi, na Waziri Lukuvi amesitisha shughuli ya utathmini na ununuzi wa nyumba zaidi ya elfu 4 na kumtaka mwekezaji huyo kuwalipa wakazi hao hasara aliyoisababisha tangu mwaka 2012.
“Nimepata malalamiko yenu kutoka kwa Mbunge wenu baada ya kunifahamisha kuhusu mgogoro huu na nimesikitishwa na dhuluma iliyokuwa inaendelea pamoja na uendeshaji wa hovyo hovyo wa huyu anayejiita mwekezaji, hawezi kuja mtu kienyeji akawaondoa watu elfu 70 bila ya utaratibu wa kisheria na kuwaeleza kuwa ameshaongea na Wizara ya Ardhi jambo ambalo sio la kweli na kuanza kuwanyanyasa kwa kuwa kuwakataza baadhi yenu kutoendelea na ujenzi au ukarabati wa nyumba zenu wala kupangisha” alisema Waziri Lukuvi.
Aidha Waziri Lukuvi alisema kuwa Serikali haiutambui kabisa mradi huo kwa sababu mambo yalifanyika kienyeji, na kuongeza kuwa serikali haikatazi mtu yeyote kuuza eneo au nyumba yake ili mradi huyo muuzaji ahakikishe analipa kodi ya asilimia 7 ya mapato ya nyumba aliyoiuza, na kuongeza kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli haitokubali kuona mwananchi ananyanyasika dhuluma yoyote ile.
Awali Meneja wa Kampuni ya PMM, Bw. Deogratus Chacha amekiri kuwa wamekuwa katika mazungumzo na wakazi wa maeneo hayo tangu mwaka 2012 kueleza kuwa mpaka kufikia mwakani mwezi wa sita watakuwa wameshakamilisha ulipaji wa fedha zote kwa wakazi ambao bado hawakupata fidia zao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Sophia Mjema alimshukuru Waziri Lukuvi kwa kuweza kuwasaidia wakazi wa maeneo hayo kwa kuweza kuwatatulia mgogoro huo kwani walikuwa hawajui hatma yao ya kuishi maeneo hayo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Segerea Mhe. Bonnah Kaluwa alisema kuwa Kampuni hiyo ya PMM ilianza mchakato wa kuanza kuwalipa wananchi mwaka 2012 na wananchi wengine wameshahama maeneo yao na wengine kushindwa kufanya maendeleo yao na wengine walikuwa wakimfata hadi ofisini kwake kutaka awasaidia na kushukuru sana Serikali ya awamu hii kuwa sikivu na kuweza kuwatatulia mgogoro huo kwani walikuwa hawajui hatma yao itakuwaje.
Utendaji kazi wa Waziri Lukuvi umeendelea kupongezwa kila kona ya nchi huku wengi wakionyesha kumkubali zaidi na kutaka mawaziri wengine kuiga mfano huo katika kumsaidia Rais Dkt John Magufuli kuwatumikia watanzania .
0 comments:
Post a Comment
AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE