December 6, 2017

SINUNULIKI NA HAWAIWEZI BEI YANGU- KUBENEA


Mbunge wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chadema, Saed Kubenea amesema hana mpango wa kuondoka katika chama hicho na kujiunga na CCM, wala kujiuzulu ubunge, kwa madai kuwa hakuna jipya linaloweza kumshawishi kufanya hivyo na wala hanunuliki.
Kubenea ameyasema hayo leo Desemba 6,2017 mbele ya wanahabari jijini Dar es Salaam, ambapo amedai kuwa, CCM inakumbatia rushwa, haitekelezi ahadi zake, na wala haitetei haki za wanyonge kama inavyojinadi, na kwamba hawezi kubadili msimamo wake wa muda mrefu katika kukikosoa chama hicho ili kijirekebishe na kufuata misingi yake ya asili.
“Sina mpango sijawahi kuzungumza na mtu yoyote wa CCM, ya kwamba mimi nataka kujiunga na chama hicho au kunishawishi, lakini pia nimekuwa mkosoaji mkubwa wa sera za CCM juu ya ubinafsishaji wa mashirika ya umma, uuzwaji holela wa nyumba za serikali na uwekezaji, nikiwa mwandishi wa habari za uchunguzi kwa zaidi ya miaka 15 nimekuwa nikikosoa sera hiyo, kwa uelewa wangu, sioni jipya ambalo linaweza kunishawishi nikajiunga na CCM, na mimi sijawahi kununuliwa na huwa sinunuliki,” amesema.                    
Kubenea amesisitiza kuwa, hawezi kujiuzulu ubunge na uanachama kwa kuwa ni muanifu, hawezi kuwaangusha wapiga kura wa Ubungo na watu waliomsaidia hadi kuwa mbunge, pamoja na wale aliowashawishi kuhama CCM na kujiunga Chadema akiwemo Fredrick Sumaye na Edward Lowassa.
“Nimejenga jina langu kwa zaidi ya miaka 15, kuna watu wamenichangia ili niwe mbunge ningewaangaliaje, kuna watu nimeshawishi watoke CCM warudi Chadema wangenifikiriaje, nina mkono wangu kwa Sumaye na Lowasa kuingia Chadema, nimefedheheshwa mno na nimeumizwa kwelikweli na habari za magazeti kwamba wameninukuu mimi nimeondoka Chadema. mimi ni mbunge hadi 2020 labda nife, kwa utashi wangu nitaendelea kuwa mwanachama muaminifu,” amesema na kuongeza.
“..nikifanya jambo lolote basi limetoka ndani ya moyo wangu, kama vishawishi vya fedha nimepitia vingi sana lakini sikuhongeka, sikuwahi kubadilisha msimamo wangu sikuwahi, nimekuwa kwenye historia yangu ya kukosoa CCM kwa dhamira ya chama hiki kijirekebishe kifuate misingi yake ya asili ya utu wa mtu sio kitu, kitimize ahadi yake. niliamini kufanya kazi ya uetetezi wa watu nje ya chama.”
Ameongeza “hiki chama hakijikosoi na hakikosolewi. leo huwezi kujua CCM ni chama cha ujamaa au ubepari, ndani yake kuna ujamaa au ubepari, chama cha wanyonge kinavunja nyumba bila kulipa fidia na ndani ya mwezi mmoja watu wameamriwa wavunje nyumba. kuna watu wagonjwa wako hospitali wako nje unawalazimisha wahame bila kulipa fidia, chama cha wanyonge kimeondoa wenye vyeti feki bila kifuta jasho, yupo mtu ambaye hana vyeti anatumia jina sio lake na bado yuko anakumbatiwa.”
“..chama hicho ambacho naambiwa nataka kuungana nacho, chama kinakataa rushwa nyuma kinabeba rushwa, chama kinarudisha kwenye biashara ya binadamu, binadamu ananunuliwa, ccm inafanya baishara ya kununua watu, mbunge, diwani mimi sina bei, kama ningekuwa na nia ya kuondoka chadema ningeondoka kwa ridhaa yangu, nimejenga jina langu kwa zaidi ya miaka 15,” amesema.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE