December 5, 2017

SEMINA YA UFUNGAJI MIGODI YAENDESHWA NA SERIKALI


Mkufunzi kutoka Taasisi ya Kimataifa ya nchini Canada (CIRDI), Colleen Crystal akitoa mafunzo kuhusu uhifadhi wa mabaki ya uchenjuaji (mining tailings) kwa wataalam wa Madini wa Tanzania na nje ya Tanzania.
Wizara ya Madini kupitia Kitengo cha Mazingira kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa kutoka nchini Canada (CIRDI) wameanza kutoa mafunzo ya ufungaji wa migodi kwa wataalam kutoka Taasisi za Serikali zinazosimamia Sekta ya Madini ndani na nje ya nchi.
Mkuu wa Kitengo cha Mazingira katika Wizara ya Madini,   Gidion  Kasege amesema kuwa wataalam hao watapata mafunzo kuhusu ukokotoaji wa mahesabu ya gharama za ufungaji migodi, usimamizi wa maji migodini na jinsi ya kutengeneza sehemu ya kuhifadhia mabaki ya uchenjuaji (mining tailings).
Alisema kuwa, hii ni mara ya pili kwa taasisi hiyo kutoa mafunzo kwa wataalam hao wa madini na kwamba awamu hii imeshirikisha nchi nyingine za Afrika ili wataalam hao waweze kubadilishana uzoefu na kujifunza mafanikio na changamoto ambazo nchi hizo zinapata katika shughuli za  ufungaji wa migodi.
Alieleza kuwa nchi zinazohudhuria mafunzo hayo ni Tanzania, Kenya, Namibia na Ethiopia ambapo mafunzo yanatolewa kwa njia ya nadharia na vitendo katika Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) na Buzwagi iliyopo mkoani Shinyanga.
Naye, Afisa katika Ofisi ya Madini mkoani Shinyanga, Mhandisi Joseph Kumburu ameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo wataalam wataongeza uelewa katika shughuli za usimamizi wa migodi nchini na hivyo kuhakikisha kuwa migodi inafuata taratibu zote zinazotakiwa wakati wa usitishaji wa shughuli zao nchini.
Wataalam wa Madini kutoka ndani na nje ya nchi wakiwa katika mafunzo ya ufungaji migodi yaliyoratibiwa na Wizara ya Madini na Taasisi ya Kimataifa kutoka nchini Canada (CIRDI).
Alisema kuwa kupitia changamoto ambazo nchi nyingine wamepata katika shughuli hizo za madini,  itawasaidia kuwa makini zaidi wa utekelezaji wa shughuli hizo nchini.
Kwa upande wake, Afisa Mazingira kutoka Wizara ya Madini, Innocent Makomba, alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa wataalam kwani yanaongeza uelewa wa masuala yanayopaswa kutekelezwa kabla ya ufungaji wa migodi ikiwemo suala la kushirikisha jamii inayozunguka migodi kabla ya kufanyika kwa maamuzi.
“Tunajifunza kuwa ni muhimu kushirikisha jamii kwani  wao wanaweza kuamua kuwa maeneo ambayo uchimbaji umeshafanyika yatengenezwe kwa ajili ya kufanyia shughuli nyingine kama uvuvi, kilimo au hata kuwa makazi ya watu na kupitia mafunzo haya tumeona mifano ya jinsi nchi nyingine zilivyotekeleza suala hilo,” alisema Makomba.
Vilevile, Makomba alisema kuwa mafunzo hayo yamewaongezea uelewa katika suala la utengenezaji wa sehemu za kuhifadhia mabaki ya uchenjuaji (mining tailings) ili zisilete madhara kwa wananchi au mazingira.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE