December 15, 2017

RATIBA MPYA LIGI KUU YA VODACOM


Ligi Kuu ya Vodacom iliyosimama kupisha michuano ya Kombe la Chalenji inaendelea mwishoni mwa mwezi huu kwa mechi za raundi ya 12 zitakazochezwa kati ya Desemba 29 na 31 mwaka huu, na Januari mosi mwakani.
 
Vilevile mechi 16 kati ya 152 zilizobaki za Ligi hiyo zitachezwa kuanzia saa 8 kamili mchana. Kwa mujibu wa Kanuni ya 14 (45) ya Ligi Kuu, mchezo wowote wa Ligi Kuu unatakiwa kuchezwa kati ya saa 8 kamili mchana, na saa 4 kamili usiku.
 
Uamuzi huo umefanywa ili kuongeza mechi ambazo zinataoneshwa moja kwa moja (live) na mdhamini wa matangazo, hatua ambayo itaisaidia Bodi ya Ligi kufuatilia kwa karibu uchezeshaji wa waamuzi na pia kutoa nafasi kwa wadhamini wa Ligi pamoja na wa klabu kuonekana zaidi (mileage).
 
Hivyo, mechi 102 kati ya 152 zitaoneshwa moja kwa moja ikiwemo zile zinazofanyika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam ambazo kwa kawaida zinachezwa kuanzia saa 1 kamili usiku. 
 
Mechi za raundi ya 12 ni Desemba 29; Azam vs Stand United (saa 1 usiku), Desemba 30; Lipuli vs Tanzania Prisons (saa 8 mchana), Mtibwa Sugar vs Majimaji (saa 10 jioni), Ndanda vs Simba (saa 10 jioni), Desemba 31; Njombe Mji vs Singida United (saa 8 mchana), Mbao vs Yanga (saa 10 jioni), Januari 1; Mbeya City vs Kagera Sugar (saa 10 jioni), na Mwadui vs Ruvu Shooting (saa 10 jioni).
 
Baada ya raundi ya 12, Ligi Kuu ya Vodacom itapisha mechi za Kombe la Mapinduzi na raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports itakayochezwa kati ya Januari 5 na 7 mwakani kabla ya kuingia raundi ya 13 itakayofanyika kati ya Januari 13 na 17, 2018.
 
Kwa upande wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL), itaingia raundi ya 10 Desemba 30 kwa mechi za Kundi A na C, wakati mechi za Kundi B zitafanyika Desemba 31.
 
Ligi Daraja la Pili (SDL) itaanza hatua ya pili Desemba 29 kwa Kundi B, C na D wakati mechi za Kundi A zitafanyika kuanzia Desemba 30, 2017.


MWANSASU ATANGAZA KIKOSI CHA TAIFA SOKA LA UFUKWENI
Kocha wa timu ya Taifa ya soka la ufukweni, John Mwansasu ameita wachezaji 16 watakaoingia kambini kesho Jumamosi Desemba 16, 2017 kujiandaa na michuano ya Copa Dar es Salaam itakayofanyika kwa siku mbili kwenye Ufukwe wa Coco.
Kikosi hicho cha wachezaji 16 kitaingia kambini kwa muda wa wiki nzima kujiandaa na mashindano hayo ya kimataifa yatakayojumuisha timu nne ambazo ni Malawi, Uganda, Zanzibar na wenyeji Tanzania Bara.
Wachezaji walioitwa ni pamoja na Rajabu Ghana (Huru), Khalifa Mgaya (Chuo cha CBE), Juma Kaseja (Kagera Sugar), Juma Sultan (Chuo Kikuu Ardhi), Ally Rabby (Huru), Mwalimu Akida (Huru), Samwel Salonge (Huru), Athuman Idd 'Chuji' (Coastal Union), Kenan Mwandisi (Huru), John Pauseke (Huru), Joseph Jafet (Huru), Jaruph Rajab Juma (Chuo cha DIT), Mbwana Mshindo (Chuo cha DSJ), Rolland Msonjo (Singida United), Jerry Francis Robert (Huru) na Haruna Moshi (Friends Rangers)
Benchi la ufundi linaongozwa na Mwansasu mwenyewe akisaidiwa na kocha wa makipa Peter Manyika, Meneja Deo Lucas na daktari wa timu Richard Yomba.

Kocha John Mwansasu amesema mashindano hayo ya Copa Dar Es Salaam yatakayofanyika Desemba 25 na 26, 2017 yatasaidia kuwaongezea uzoefu zaidi kwa mchezo huo wa soka la Ufukweni.
UJIO WA TIMU YA OLIMPIQ STARS YA BURUNDI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetoa kibali kwa Chama cha Soka Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA) kusimamia michezo miwili ya kirafiki ya kimataifa itakayofanyika Uwanja wa Kambarage kwa siku za kesho Jumamosi Desemba 16, 2017 na Desemba 17, mwaka huu.
Michezo hiyo itahusu timu ya Olimpiq Stars ya Burundi ambayo kwa sasa iko Shinyanga kwa ajili ya michezo hiyo ya kirafiki ambako kesho Jumamosi itacheza na Stand United na Jumapili itapambana na Mwadui ya Shinyanga.
Lengo kubwa ya ziara hiyo ni kuzipa timu za mazoezi ili ziweze kufanya vema kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara; pia kupima uwezo wa wachezaji ambao timu hizo za Tanzania zimewasajili katika kipindi cha dirisha dogo na kudumisha ujirani mwema.
SHIREFA imeithibitishia TFF kwamba itafuata itifaki zote kwa mujibu wa taratibu za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
......................................................
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA SOKA TANZANIA

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE