December 6, 2017

ASAS , CHALAMILA NA BARAZA WAPANGA SAFU YA KURUDISHA JIMBO LA IRINGA MJINI CCM

MKURUGENZI wa kampuni za usafirishaji  mizigo za Asas Salim Abri Asas aibuka  na ushindi  wa  kishindo katika  nafasi ya  ujumbe  wa Halmashauri  kuu ya  Taifa (NEC) kuwakilisha  mkoa  wa Iringa  huku mwenyekiti   mpya  wa  Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa Albert  Chalamila ametangaza kiama  kwa  wabunge  na  madiwani  wa  CCM  ambao  hawajafanya kazi  majimboni  kutochukua  fomu ya  kuwania nafasi  hizo  mwaka 2020.

Pia  ataka  mali  zote  za CCM   kwa  kila  wilaya kujulikana  ili  kukomesha  ufisadi  unaofanywa na  baadhi ya  viongozi kupitia  miradi hiyo ya  chama .

Asas  na Chalamila walisema  kazi  ya  kulikomboa   jimbo la  Iringa 2020  itaanza katika kata ya  Kihesa jimbo la  Iringa mjini  kwenye uchaguzi mdogo  wa  udiwani utakaofanyika  Januari  mwakani .

Huku  wakimtaka  mbunge  wa  jimbo la  Iringa mjini mchungaji Peter  Msigwa  kuanza  kutafuta kazi nyingine ya  kufanya kwani  uchaguzi  mkuu  ujao hana  chake  tena  jimbo  hilo .

Akitangaza matokeo hayo juzi  msimamizi uchaguzi huo Januari Makamba alisema mkutano huo ulihudhuriwa na wajumbe 617.

Makamba ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) alisema mkutano huo ulimchagua Chalamila kuwa mwenyekiti wake kwa kumpa kura 523 dhidi ya kura 61 alizopata mpinzani wake mkuu wa wilaya mstaafu, Evans Balama na kura 9 alizopata Daniel Kidava.

Kwa upande wa mjumbe wa NEC, Salim Asas alishinda kwa kuzoa kura 502 dhidi ya kura 74 alizopata Marcelina Mkini na 15 alizopata Benard Mbungu.

Aidha mkutano huo uliwachagua Dickens Lulanda na Rita Mlagala kuwa wajumbe wa Halmashauri ya CCM Mkoa wa Iringa kutoka Iringa Vijijini.

Wakati Lulanda alipata kura 311, Mlagala alipata kura 308 dhidi ya kura 261 alizopata Augustino Gwelino, 131 za Daniel Chota, 112 za Joshua Nyagawa na 89 alizopata Lediana Mng’ong’o ambaye hata hivyo alitangaza mapema kujitoa katika kinyang’anyiro hicho.

Kwa upande wa wilaya ya Mufindi, mkutano huo ulimchagua Gerald Kahemela (343) na Donald Kalima (373) kuwa wajumbe wa halmashauri hiyo ya mkoa baada ya kuwashinda Juma Fulgens (108) na Brastus Mgimwa (174).

Kutoka Iringa Mjini,  Vitus Mushi aliyepata kura 297 na  Zainabu Mwamwindi aliyepata kura 202 walichaguliwa kuwa wajumbe wa kikao hicho baada ya kuwabwaga Maxmillan Lugenge aliyejipatia kura 143, Kaijage Kitunzi aliyepata 119 na Kondo Ramadhani aliyeambulia 103.

kutoka Kilolo mkutano huo ulimchagua  Leah Mwamoto  kwa kura 324 na Joseph Muhumba aliyepata kura 322 kuwa wajumbe wa kikao hicho baada ya kuwabwaga Gervas Kahemela (54), Hilda Mwogofi (114), Mari Sauge (126) na Nancy Nyalusi (179).

Baada ya kukamilika kwa uchaguzi huo, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa Christopher Magala kwa kushauriana na mwenyekiti wake mpya waliitisha kikao maalumu cha halmashauri kuu ya mkoa kilichofanya kazi ya kumchagua Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho.

Kwenye kikao hicho, Mwinyikheri Baraza alichaguliwa kuwa Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Iringa katika kinyang’anyiro kilichowashirikisha wagombea wengine wawili akiwemo Andrew Ghemela na Josia Kifunge.

Akiwashukuru wapiga kura kwa ushindi huo mzito, Chalamila alisema cheche zake ataanza kuzionesha kupitia uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Kihesa huku akipiga marufuku majungu, fitina, chuki, umbea na uzushi akisema mambo hayo yamekilemaza chama hicho kwa muda mrefu na kusababisha migawanyiko isiyo ya lazima.

Aidha amesema uongozi wake unataka kuanza majukumu yake ukiwa na mikono safi kwahiyo watakachofanya pamoja na mambo mengine ni kufanya uhakiki wa mali zote za chama na jumuiya zake ili kujua namna zinavyotumika na kukisaidia chama hicho.

Huku Asas alisema mkoa wa Iringa ni mkoa ambao kwa miaka mingi umekuwa ukiongoza kwa kutoa kura nyingi kwa wagombea wa ngazi mbalimbali za uongozi.

Akijifananisha na Paka alisema anatambua uwepo wa panya (wapinzani) katika Jimbo la  Iringa mjini na sehemu kadhaa
wakiahidi kukomboa jimbo la Iringa Mjini katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Pamoja na kukomboa jimbo hilo linaloongozwa na Mchungaji Peter Msigwa kwa awamu ya pili sasa (toka 2010), viongozi hao wapya wameahidi pia kukiwezesha chama hicho kushinda kwa kishindo uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Kihesa, utakaofanyika Januari, mwakani, na kukomboa halmashauri ya manispaa ya Iringa kutoka mikononi mwa Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Chalamila anayependa kuitwa Mwalimu ni Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa (IUCo) na Asas ni mkurugenzi wa kampuni za ASAS zinazojishughulisha na usafirishaji, ufugaji, viwanda, biashara ya mafuta na majengo ya kupangisha.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE