November 24, 2017

SERIKALI INACHUNGUZA KIFO CHA MTOTO ALIYEFARIKI KWA KUPIGWA NA SILAHA INAYODAIWA NI GOBORE HUKO LUKENGE

IMG_20171123_112908
MKUU wa wilaya ya Kibaha,Assumpter Mshama akizungumza kwenye mkutano maalumu wa kijijini cha Lukenge,kata ya Magindu,wilayani hapo.
Picha na Mwamvua Mwinyi
……………
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha 
SERIKALI inaendelea kuchunguza tukio la mtoto ambae anadaiwa kuuwawa kwa kupigwa na gobore na baba yake mdogo Ally Sakalawe (43) wakati akijibizana na makachero wa polisi walipokwenda kufanya upekuzi wa silaha zinazomilikiwa kinyume na sheria,kijiji cha Lukenge kata ya Magindu ,Kibaha.
Wakati serikali ikiendelea na uchunguzi huo ,wakazi wa kijiji hicho wametakiwa kuendelea na shughuli zao na kuishi kwa amani .
Akizungumza kwenye mkutano mkuu maalumu wa kijijini hapo, mkuu wa wilaya ya Kibaha, Assumpter Mshama alisema serikali itatoa taarifa kamili ili kuondoa utata ambao umegubika tukio hilo kwa baadhi ya familia na wakazi wa kijiji hicho kudai kuwa polisi ndiyo walimwua mtoto huyo aitwaye Mark Joel Modest (15).

Alieleza anajua kuwa tukio hilo limeumiza familia na wakazi lakini wawe na subira kupisha uchunguzi .
“Nawaomba muishi kwa amani na msiwe na wasiwasi serikali inaendelea na uchunguzi na mtapewa majibu utakapokamilika “;:
“Watu wanaosema kuwa hawaishi majumbani kuhofia kukamatwa wasiogope kama wanajijua sio wahalifu hawana haja ya kuogopa,” alisema Assumpter.
Alieleza vyombo vyote vya ulinzi na usalama vinafanya kazi zake na haki itatolewa kwani jambo hili linasikitisha kwakuwa mtoto kapoteza uhai na alikuwa hausiki kwa lolote.
Aidha aliwataka wananchi hao kuwa wawe makini katika kumiliki silaha ambapo mtuhumiwa licha ya kutokea kwa tukio hilo la mauaji pia alibainika kuwa alikuwa akimiliki gobore kinyume na taratibu.
Pamoja na hayo alikutwa na vitu mbalimbali ambavyo vinaleta maswali mengi juu ya matumizi ya silaha hiyo.

“Lazima tujiulize licha ya kifo cha mtoto huyo lakini mtuhumiwa ambaye anashikiliwa na polisi alikutwa na bunduki mbili aina ya gobore, risasi ya mark 4, vipande vya nondo na gololi vyote vikitumika kama risasi hivyo lazima tujiulize matumizi ya silaha hizi,” alifafanua Assumpter.
Awali akielezea juu ya tukio hilo mke wa mtuhumiwa ,Zaina Manoza alisema siku ya tukio hilo walikuwa wamelala ndani majira ya saa 8 kwenda saa 9 usiku askari walifika na kuanza kupiga bunduki na wao kuanza kupiga kelele wakiomba msaada kwa majirani.

Walitakiwa watoke nje na kujitambulisha kwa majina lakini yeye akawaambia katika hao mtoto mmoja hayupo wakamwambia akamwangalie chumba kingine na alipokwenda alimkuta mtoto huyo akiwa anavuja damu ubavuni.

“Baada ya hapo walinitaka nikamwite mwenyekiti wa kitongoji na alipofika wakawaambia wampeleke mtoto akapate tiba na kunitaka niongozane na huyo mtoto na mwanangu mwingine tukiwa tumembeba nikaona kama hali ni mbaya nikajua tayari kafa,” alisema Zaina.

Kamanda wa Polisi wa wilaya ,Caster Ngonyani alisema wananchi wanapaswa kuishi kwa amani na hawatakiwi kuwa na hofu.
Ngonyani alisema kuwa ripoti aliyopewa juu ya tukio hilo ilisema kuwa polisi walikwenda kwenye nyumba hiyo baada ya kupata taarifa kuwa kuna silaha aina ya gobore inayomilikiwa bila ya kibali.
“Taarifa hizo walizipata kutoka kwa wakazi wa kijiji hicho ndipo walipokwenda kwa ajili ya kuzikamata”Na kulikuwa na wamiliki wawili wa hizo silaha ambao ni Ally Sakalawe na Robinus Almas na hawakutoa taarifa kwa uongozi kwa hofu taarifa kuvuja “
“Walipofika waligonga na kushindwa kuingia ndani baada ya mtuhumiwa kukataa kufungua mlango na kuanza kurusha  hewani,” alisema Ngonyani.

Alisema kuwa mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi kwenye Hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Tumbi mbele ya baba Mzazi Modest na Anna Raphael mama mzazi.

“Kulikutwa kipande cha chuma ambacho ni kipande cha nondo kwenye tumbo la marehemu hali ambayo inaonyesha silaha iliyotumika ni gobore na silaha ya polisi haitumii chuma inatumia risasi na zingekutwa tungejua kuwa polisi walihusika,” alisema Ngonyani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ni dhahiri kuwa mtoto huyo alipigwa na mtuhumiwa kwani tumboni kulikutwa kipande cha nondo ambazo zimekatwa na hutumika kama risasi kwenye magobore hayo ambapo vipande vingine 10 vilikutwa nyumbani kwa mtuhumiwa.

Tukio hilo lilitokea Oktoba 28 mwaka huu wakati polisi walipokwenda kufanya upekuzi juu ya uwepo wa silaha hizo aina ya magobore ambaye yalikuwa yakitumika kwa uhalifu na uwindaji haramu.
Licha ya mtuhumiwa wa kwanza kukutwa na silaha hizo pia walimkamata Robson Almas naye akiwa na magobore mawili yakiwa hayana vibali vya umiliki.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE