November 14, 2017

REKODI YA ITALIA BAADA YA MIAKA 60 KUPITA


Ulimwengu wa kandanda unazungumzia ukweli kwamba kwa mara ya kwanza katika miaka 60, miamba wa kandanda Italia, mabingwa mara nne wa dunia, hawatashiriki katika dimba la Kombe la Dunia
Wachezaji kutoka timu zote walijibwaga chini kwenye nyasi, wachezaji wa Sweden wakiwa wamechoka na wenye machozi ya furaha, nao Wataliano wakibubujikwa na machozi ya huzuni na uchungu.
Katika usiku uliojaa hisia kali mjini Milan, mabingwa mara nne Italia, walishindwa kufuzu kwa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika miongo sita. Sweden walijikatia tikiti kwa mara ya kwanza tangu 2006.
Licha ya kuumiliki mchezo kwa asilimia 70, Italia ilitekwa kwa sare ya bila kufungana bao katika mchuano wa mkondo wa pili wa mechi yao ya mchujo jana usiku na Sweden ikaibuka na ushindi wa bao moja kwa bila kutokana na mchuano wa mkondo wa kwanza.
Fußball WM Qualifikation 2018 Italien - Schweden Gian Piero (picture-alliance/AP Photo/L. Bruno) Kocha Ventura anasema atatathmini mustakabali wake
Wachezaji wa Sweden walishangilia uwanjani na mashabiki wao, wakati Wataliano wakitiririkwa machozi hasa nahodha na mlinda mlango Gianluigi Buffon, ambaye alicheza kile alisema ni mechi yake ya mwisho ya kimataifa baada ya kuwa mlangoni mwa miaka 20 na timu yake ya Azzurri.
Italia ilishindwa kufuzu katika Kombe la Dunia mara moja tu hapo kabla, mwaka wa 1958, na baada ya hapo ikafuzu mara 14 mfululizo. Mashindano makuu ya mwisho ambayo Italia ilishindwa kufuzu ni ya ubingwa wa Ulaya mwaka wa 1984 na 1992.
Inaweza kuwa rahisi kumlaumu Gian Piero Ventura. Kocha huyo wa italia kawaida atabeba lawama kubwa, lakini matatizo ya timu yake yamekita mizizi sana.
Matatizo yalianza hata kabla Ventura kuchukua usukani. Baada ya kushinda Kombe la Dunia 2006 kwa mara ya nne, Italia iliondolewa katika hatua ya makundi ya Kombe la Dunia 2010 na 2014. Ilifanya vyema katika ubingwa wa Ulaya, kwa kufika fainali ya 2012 na kuondolewa katika robo fainali 2008 na 2016.
Fußball WM Qualifikation 2018 Italien - Schweden Gianluigi Buffon (picture-alliance/Zumapress/M. Ciambelli) Buffon aliiaga timu ya Azurri baada ya miaka 20
Hata hivyo, Italia ya kocha Antonio Conte ilionekana kupata mafanikio makubwa Ufaransa mwaka jana, wakati iliichabanga Uhispania katika hatua ya 16 kabla ya kushindwa kupitia mikwaju ya penalty na mabingwa wa dunian Ujerumani.
Kwa muda mrefu, italia imekosa ubunifu, warithi wa Andrea Pirlo na Francesco Totti wa timu ya 2006 ambao wangeweza kuubadilisha mchezo kwa kutumia fursa moja tu. ukosefu wa wachezaji nyota katika timu ya Italia unaonekana kwenye ligi ya Italia Sirie A.
Juventus imenawiri katika miaka ya karibuni barani Ulaya, ambapo imefika fainali mbili kati ya tatu za mwisho za Champions League. Lakini wakati safu yake ya ulinzi ina wachezaji muhimu kutoka timu ya taifa, safu yake ya kiungo na mashambulizi inawajumuisha wachezaji wengi wa kigeni.
Italia itahitaji kusonga mbele bila ya baadhi ya wachezaji wao wenye uzoefu mkubwa. Daniele de Rossi pia alitangaza kuwa anazitundika njumu baada ya mechi ya jana sawa na beki Andrea Barzagli.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE