November 6, 2017

MWAKALEBELA ANG'ARA KAMPENI ZA UDIWANI CCM KATA YA KITWIRU

Image result for mwakalebela CCM
kada  wa  CCM  Frederick  Mwakalebela  ambae  alikuwa mgombea  ubunge  jimbo la  Iringa  mjini  
Umati  wa  wananchi  wakiwa  katika mkutano  wa  uzinduzi  wa kampeni  za CCM kata ya  Kitwiru Iringa mjini

Sehemu ya  wananchi  waliofika  katika mkutano wa CCM 
Aliyekuwa  diwani wa  kata ya  Kihesa (Chadema)  akipokelewa na katibu  wa  itikadi na  uenezi  CCM Taifa Bw  Pole  Pole jana  baada ya  kujiuzulu na  kujiunga na CCM

Waliokuwa  madiwani  wa  viti maalum Chadema Iringa mjini  Leha  na Husna wakicheza baada ya  kujiunga  CCM 


Makada  wa  Chadema  waliojiunga CCM


Viongozi  wa   Chadema  Kitwiru  waliojiunga CCM
ALIYEKUWA  mgombea  ubunge  jimbo la  Iringa mjini katika  uchaguzi wa mwaka 2015 Iringa mjini kupitia  CCM Frederik Mwakalebela atikisa  kampeni za  CCM Iringa mjini huku diwani wa Chadema kata ya  Kihesa  Edga Mgimwa akijiuzulu na kujiunga na CCM .

Mbele  ya katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa wa chama hicho, Livingstone Lusinde Mwakalebela  alionyesha  kuendelea  kukubalika  zaidi Iringa mjini baada ya wananchi  kupaza  sauti  kumtaka apande  jukwaani wasikie sauti  yake .


Mwakalebela  akiwa  jukwaaani aliwaomba  wananchi wa  Kitwiru  kutopoteza  muda kumchagua mpinzani  katika kata  hiyo na kuwataka  kura  zote  kumpa Baraka  Kimata wa CCM .

" Nawaombeni sana kama  mlivyoonyesha kunikubali  naomba kura  zenu  zote  mpeni Kimata  ili  kwa  kushirikiana na Rais Dkt John Magufuli aweze  kuleta maendeleo "


Pamoja na Mwakalebela pia tukio kubwa jingine ambalo lilitikisa mkutano  huo ni la kujiuzulu kwa  aliyekuwa  diwani wa Chadema kata ya  Kihesa  Edgar Mgimwa (Chadema) na wanachama wengine sita wa Chadema walikihama chama hicho na kujiunga na CCM kwa  kueleza  kuchoshwa na ubabaishaji ndani ya  Chadema .

Tukio  hilo  kwa  Chadema ni kama pigo kubwa baada ya ya miezi miwili na kidogo tangu ikimbiwe na madiwani wengine watatu, akiwemo diwani wa kata ya Kitwiru, Baraka Kimata na Leah Mleleu na Husna Daudi ambao ni madiwani wa viti maalumu.

Baada ya kutangazwa kwa uchaguzi wa marudio wa kata hiyo, Kimata aliyejiunga CCM muda mfupi baadae alishinda kura za maoni na kusimamishwa kwa tiketi ya chama hicho kuwania tena udiwani wa kata hiyo utakaofanyika Novemba 26, mwaka huu.

Akitetea uamuzi wa CCM kumsimamisha tena Kimata kuwania udiwani katika kata hiyo aliyoiongoza kwa miaka miwili akiwa Chadema, Lusinde alisema; “Kwa kuwa Chadema walisema mtu kwanza, chama baadae ndio maana tumemrudisha Kimata ili tuone unafiki wao.”

Pamoja na kwamba Kimata alijiunga na CCM muda mfupi baada ya kujitoa Chadema, Leah na Husna walipokelewa na Polepole jana katika tukio lililokwenda sambamba na kumpokea diwani wa kata ya Kihesa na wanachama wengine sita wa Chadema wakati wa uzinduzi wa kampeni za udiwani wa kata hiyo.

Akiwapokea madiwani na wanachama hao, Polepole alisema mwaka 2015 CCM walifanya kosa la kizembe lililosababisha jimbo la Iringa Mjini liende tena kwa Mchungaji Peter Msigwa na wapoteze halmashauri ya manispaa ya Iringa kwa wapinzani wao hao.

Katika uchaguzi huo, Mchungaji Msigwa alimshinda kwa mbali Frederick Mwakalebela wa CCM ambayo pia ilipoteza kata 14 kati ya 18 katika uchaguzi wa madiwani.

“Tukiri tulifanya makosa ya kizembe akapata ubunge, lakini leo nimekuja Iringa kumpa ujumbe mzito Mchungaji Msigwa kwamba ajiandae kurudi kanisani akachunge kondoo wa bwana,” alisema.

Alisema siku za Mchungaji Msigwa zinahesabika kwa kuwa watu wa Iringa, wakiwemo madiwani na wanachama wa Chadema wanaorudi CCM wameanza kubaini jinsi wasivyostahili kuongozwa tena na mtu muongo.

“Huyu Mbunge ndiye yule aliyewahi kusema mtu yoyote atakayemuunga mkono Edward Lowassa anastahili kupimwa akili, cha kushangaza baada ya muda mfupi alikuwa mmoja wa viongozi wa Chadema aliyemuunga mkono kiongozi huyo lakini hadi leo, hajaenda kupimwa akili,” alisema.

Aliwapongeza wana Chadema wanaojitoa na kujiunga na CCM akisema wanaridhishwa na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM unaosimamiwa na Rais Dk John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa.

Akizungumza kwa niaba yao, Diwani wa Kihesa alisema hajutii uamuzi wa kujitoa Chadema na kujiunga CCM kwasababu anaridhishwa na jinsi siasa zake zinavyoendeshwa na namna serikali ya awamu ya tano inavyoshughulikia kero mbalimbali za wananchi.

“Kimsingi mimi nilikuwa mwana CCM kabla ya kugombea udiwani katika kata hiyo mwaka 2015, nilifuatwa na Chadema Julai 2015 na kuombwa kugombea, kuna matatizo makubwa ndani ya Chadema, hakuna demokrasia na kimekithiri kwa ubabe, kwahiyo nimeamua kurudi nyumbani,” alisema Mgimwa.

Polepole na Lusinde waliwataka wapiga kura wa kata hiyo kumchagua Kimata kuwa diwani wa kata hiyo wakisema pamoja na uchache wao katika manispaa ya Iringa, wanaangaliwa kwa jicho kubwa na Rais Dk Magufuli na chama kwa ujumla.

 “CCM tunatambua sehemu ya kata hii kuna tatizo la upatikanaji wa maji, lakini pia kuna tatizo la daraja la Kitwiru. Hiyo ni kazi yetu, ipo ndani ya Ilani yetu hivyo tutaziagiza mamlaka zinazohusika ili zishughulikie,” Polepole alisema.

Akiomba kura kwa wananchi wa kata hiyo Kimata alisema kuna kila dalili Mchungaji Msigwa akabaki  pekee yake katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 kwa kuwa hataki kuambiwa ukweli.

“Nilipokuwa Chadema nilikuwa na mvutano mkubwa na wa muda mrefu wa kiutendaji na mbunge wa jimbo la Iringa Mjini kwasababu ni mtu asiyeambilika, hataki ukweli na anayeamini anajua kila kitu, nilikuwa pia Katibu Mwenezi wa Chadema Jimbo na hii iliniweka katika mazingira magumu sana. Nimevumilia kulinda heshima ya mbunge na chama lakini ikafikaa mwisho nikasema kuvumilia,” alisema.

Alisema baada ya kujitoa Chadema na kujiunga CCM baadhi ya wana Chadema walimtukana sana na akatumia mkutano huo kuwasamehe na kuwaomba kura kwa kuwa rekodi yake ya utendaji wanaijua.
0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE