November 29, 2017

MPANGO WA KUSAIDIA WAKULIMA WADOGO NCHINI WATAMBULISHWA


1
Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa  Kituo cha Kuendeleza Kilimo
Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Bw. Salum Shamte
(wa pili kushoto) akimkabidhi vitendea kazi mwenyekiti mpya, Bw. Ally
Laay katika hafla ya uzinduzi wa Bodi mpya iliyofanyika jijini Dar es
Salaam jana. Wanaoshuhudia wa pili kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya
Kilimo, Mhandisi   Mathew Mtigumwe na Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT,
Bw. Geoffrey Kirenga (kushoto)
2
Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa  Kituo cha Kuendeleza Kilimo
Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Bw. Salum Shamte
akisisitiza jambo wakati hafla ya uzinduzi wa Bodi mpya iliyofanyika
jijini Dar es Salaam jana.Katikati ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo,
Mhandisi   Mathew Mtigumwe na mwenyekiti mpya wa Bodi Bw. Ally
Laay(kulia)
3
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi   Mathew Mtigumwe (mstari
wa mbele waliokaa katikakati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wajumbe
wa Bodi waliomaliza muda wao na wale wapya pamoja na wafanyakazi wa
SAGCOT muda mfupi mara baada ya kuzindua Bodi mpya jijini Dar es
Salaam jana. Wengine  (kushoto) Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Bw.
Salumu Shamte na Mwenyekiti mpya wa Bodi Bw. Ally Laay(kulia)
………………………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KATIBU Mkuu Wizara ya Kilimo, Mhandisi Mathew Mtigumwe amesema serikali inakusudia kutekeleza  Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo awamu ya pili,(Agricultural Sector Programme Development (ASPD II) kwa mtindo unaotumiwa na Kituo cha Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) inayojulikana kama ‘SAGCOT model’
“Huu utaratibu unaotumiwa na SAGCOT tutautumia kwenye ASPD II kwa sababu umeonyesha mafanikio makubwa, tunapozungumzia serikali kufanyakazi na sekta binafsi maanayake wanaguswa wakulima wadogo ambao ndiowazalishaji wakubwa,” alisema Mhandisi Mtigumwe.
Akizindua Bodi mpya Wakurugenzi ya SAGCOT jijini Dar es Salaam jana, Mhandisi Mtigumwe alisema serikali itahakikisha utekekelezaji wa ASPD 11 unafanikiwa nakuleta matokeo chanya kati sekta ya kilimo nchini.
Katika hafla ilishuhudia makabidhiano ya uenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa kituo hicho kutoka kwa Bwana Salum Shamte aliyedumu kwa miaka sita na kwenda kwa Mwenyekiti mpya Bwana Ally Laay.
“Kwa muda wa miaka sita bodi ya wakurugenzi chini ya Salum Shamte ilifanya kazi kubwa kuendeleza kilimo ukanda wa nyanda za juu kusini, naomba bodi mpya ianzie wanapoishia hawa wanaoondoka, serikali tukiwa wafadhili wakubwa tunaahidi ushirikiano wa hali na mali kila tutakapohitajika,” alisema Mhandisi Mtigumwe.
Kwa upande wake, Bwana Shamte alisema sababu za kuanzishwa kwa kituo hicho ilikuwa ni kubadili kilimo kutoka cha kimazoea hadi chenye tija kwa wakulima wadogo, hivyo kwa muda wote huo wamekuwa wakifanya kazi na wakulima wadogo mashambani na kuwaonyesha fursa.
“Tulitaka kilimo kimlipe mkulima ili iwe sababu ya kuondokana na umasikini uliokithiri, vilevile tulidhamiria kuondoa tatizo la chakula nchini pamoja na kukuza uchumi. Tunafahamu Tanzania ya viwanda inahitaji malighafi ambayo inatoka shambani, tumeona viwanda vipya vingi vimeanzishwa lakini vimekufa kwa kukosa malighafi,” alisema Bw. Shamte.
Akifafanua mtindo wa kushirikisha sekta binafsi na sekta ya umma katika utaratibu wa kufanikisha shughuli za kituo hicho, Shamte
alisema: “Tuliona watu wote wanaoguswa moja kwa moja na shughuli za kilimo kila mmoja anafanya kazi kwa mtindo wake, tukakubaliana tuwakusanye.
“Hivyo serikali ikakaa pamoja na sekta binafsi, wakulima, wafanyabiashara wa pembejeo na viwanda pamoja na wadau wa maendeleo.
Kwa mtindo huu ndivyo tunavyoendesha shughuli za SAGCOT.” Awali, Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Wakurugenzi wa SAGCOT, Bwana Laay alisema hakutegemea kama itatokea siku atafanya kazi na kituo hicho,lakini kwa namna alivyoisoma na kuielewa vema ni kuwa lengo kuu ni kuwaondolea umaskini watanzania wa hali ya chini.
“Mimi nimetokea Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF), hivyo lengo letu ni lile lile. Vilevile asili yangu nimekulia kijijini ambako kwa kiasi kikubwa shughuli ni kilimo na ufugaji, lakini sehemu kubwa ya ardhi haijaguswa na bado watanzania wanalalamika umasikini,” alisema Bw. Laay.
 SAGCOT inaendesha shughuli zake kwa mtindo wa kongani, imetenga kongani sita ambazo ni Ihemi inayojumuisha mikoa miwili ya Iringa na Njombe, Mbarali (Mbeya na Songwe), Kilombero (Morogoro), Ludewa (Ruvuma), Sumbawanga (Rukwa) na Rufiji (Pwani), ambapo katika maeneo hayo inaangaziwa ongezeko la mnyororo wa thamani katika mazao yanyanya, viazi mviringo, chai, mahindi, mchele, soya na maziwa.
Wabia wa kituo hicho ni Serikali ya Tanzania, Ubalozi wa Norway, Benki ya Dunia, UKAID, USAID, UNDP na AGRA.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE