November 22, 2017

MLADIC HUENDA AKAFUNGWA MAISHA HII LEO

Majaji wa Mahakama ya Uhalifu wa Kivita mjini The Hague, Uholanzi, wanatarajiwa kutoa hukumu ya kihistoria Jumatano katika kesi ya mauaji ya halaiki inayomkabili kamanda wa zamani wa Bosnia na Serbia Ratko Mladic.
Hii ni hatua itakayofunga ukurasa wa yale mauaji ya miaka ya tisini ya eneo la Balkan. Kesi ya Mladic ndiyo ya mwisho kutoka iliyokuwa Yugoslavia na uamuzi huo umekuwa ukisubiriwa na maelfu ya wahanga katika eneo hilo ambalo limegawika pakubwa.
Mladic ambaye anakabiliwa na mashtaka 11 anashutumiwa kwa kuongoza kikosi kilichohusika na uhalifu ikiwemo mauaji mabaya zaidi ya vita hivyo, ambayo yalijumuisha uvamizi wa miaka mitatu wa Mji Mkuu wa Bosnia, Sarajevo, pamoja na mauaji ya halaiki ya mwaka 1995 ambapo wanaume na wavulana 8,000 wa Kiislamu waliuwawa katika eneo la Srebrenica. Hayo yalikuwa mauaji mabaya zaidi kuwahi kufanyika Ulaya tangu vita vya pili vya dunia.
Jopo la majaji watatu katika mahakama hiyo wataamua iwapo wamempata na hatia Mladic mwenye umri wa miaka 75 au la na iwapo watamhukumu basi watatoa kifungo pia mara moja.
Waendesha Mashtaka wanataka ahukumiwe kifungo cha maisha
Waendesha mashtaka wanataka ahukumiwe kifungo cha maisha ingawa mawakili wa Mladic wanataka aachiliwe huru na aondolewe mashtaka yote. Waendesha mashtaka wanamtuhumu Mladic na mwandani wake wa kisiasa Radovan Karadzic kwa kutaka kufanya mauaji ya kimbari ambapo walinuia kuwaangamiza Wabosnia Waislamu na Wabosnia Wacroatia kutoka maeneo yaliyokuwa yanadaiwa kumilikiwa na Wabosnia Waserbia pia.
Niederlande Urteil Ratko Mladic (Getty Images/M. Porro) Ratco Mladic akiwasili kusikiliza kutolewa kwa hukumu yake
Munira Subasic, ni rais wa chama kinachojiita "Kina mama wa Srebrenica," ambao ni wahanga wa yaliyotokea katika miaka hiyo, "Bosnia na Herzegovina inahitaji uwiano, bila shaka inahitaji hili, lakini kivipi? Kupitia uamuzi wa sawa na wa haki, kupitia kuwahukumu wahalifu wa kivita kwasababu ya ukweli. Bila ya ukweli hakuna uaminifu na bila uaminifu, hakuna uwiano," alisema Subasic. "Haki, uaminifu na uwiano ni vitu vitakavyokuwepo iwapo wale wote waliofanya uhalifu na mauaji ya halaiki watahukumiwa na majina yao yajulikane kama ya wahalifu wa kivita, kama vile tu majina ya watoto wetu yanavyojulikana kama ya wahanga," aliongeza rais huyo.
Radovan Karadzic alipewa kifungo cha miaka 40
Katika kesi iliyosikilizwa kwa kipindi cha miaka mitano, karibu mashahidi 600 walijitokeza kutoa ushahidi wao na kuliwasilishwa zaidi ya nyaraka 10,000 za ushahidi.
Bosnien und Herzegowina Geschichte über einen Knochenjäger (DW/Z. Ljubas) Kumbukumbu ya makaburi ya waliouwawa huko Srebrenica
Mzozo wa iliyokuwa Yugoslavia uliebuka baada ya kuvunjika kwa lililokuwa shirikisho la makabila tofauti katika miaka ya tisini, ambapo uhalifu mbaya zaidi ulitokea huko Bosnia. Zaidi ya watu 100,000 waliuwawa na mamilioni walipoteza maisha yao kabla mkataba wa amani haujatiwa saini mwaka 1995.
Rais wa zamani wa Bosnia Radovan Karadzic alipewa kifungo cha miaka 40 mwaka jana kwa kupanga mauaji ya Bosnia ingawa amekata rufaa kuhusiana na uamuzi huo.
Mladic alikuwa mafichoni baada ya vita hivyo na alisalia mafichoni hadi kukamatwa kwake nchini Serbia mwezi Mei mwaka 2011.
Mwandishi/Jacob Safari/APE/AFPE

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE