November 5, 2017

MIAKA MIWILI: IKULU YAMFUNDA RAIS MAGUFULI

RAIS Dk. John Magufuli anatimiza miaka miwili madarakani leo akiwa tayari ameacha alama kadhaa zinazoweza kutumika kueleza safari ngumu ya uongozi akiwa katika kilele cha mamlaka ya juu kitaifa.
Tayari watu mbalimbali kutoka kada tofauti wamekuwa wakitoa tathmini zao juu ya safari ya uongozi ya Rais Magufuli na hususan serikali yake.
Wako wanaoitazama serikali na hususan Rais Magufuli katika jicho la bashasha na kuunga mkono dhamira iliyojengwa juu ya msingi wa kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’, aliyoitumiwa yeye na chama chake kumnadi mwaka 2015.
Miongoni mwa watu walio katika kundi hili, ni mawaziri, watendaji serikalini, wanazuoni na makada kadhaa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Tayari Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, katika siku kadhaa sasa amesambaza video zinazomwonyesha akichanganua mafanikio ya miaka miwili ya Rais Magufuli Ikulu.
Aidha katika mazungumzo yake na Mhariri Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda, mbali ya kuzungumzia mafanikio na safari ya miaka miwili ya urais wa Magufuli, Polepole ameeleza kushangazwa na watu wanaojaribu kuikosoa serikali kwa namna ya kutaka kuilazimisha ijijengee taswira ya umalaika.
Polepole katika kauli yake aliyoitoa kabla ya kukutana na kufanya mahojiano ya ana kwa ana na gazeti hili alisema: “Kufanya makosa, tena makosa makubwa unapokuwa umeshika mamlaka ya juu kabisa ya kidola, si jambo la ajabu hata kidogo.”
Kwa mujibu wa Polepole, makosa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu mazito, ambayo usahihishwaji wake unapaswa kufanywa na wasaidizi na watendaji wakuu wanaomsaidia rais kutimiza majukumu yake.
Naye Msemaji Mkuu wa serikali, Dk. Hassan Abbasi, akizungumza na MTANZANIA Jumapili kuhusu safari hiyo ya Rais Magufuli mamlakani, alisema kuna mengi yametokea na kufanyika na kwamba ilikuwa ni miaka miwili ya mabadiliko ya kuchagiza pamoja na mageuzi ya kisera na kiutendaji karibu kila sekta.
Mbali ya hao, wako pia wachambuzi katika kundi la pili ambao wanautafakari uongozi wa Magufuli, almaarufu JPM au Katapila kwa namna ya mshangao au kupinga mwelekeo wake na ule wa serikali yake katika kipindi cha miaka miwili ya kwanza.
Uchambuzi wa karibuni wa walio katika kundi hili, ni ujumbe alioutoa aliyekuwa kada wa CCM na Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, wakati akitangaza uamuzi wa kujivua uanachama wa chama hicho tawala na nafasi zake zote za uongozi na uwakilishi alizokuwa akizishikilia.
Nyalandu ambaye japo hakumtaja rais kwa jina, alitoa sababu sita kubwa zilizomfanya afikie uamuzi huo. ambazo zote zilitoa mwelekeo kwamba mwenendo wa mambo serikalini, ndani ya CCM na kwa taifa kwa ujumla katika kipindi cha miaka miwili, haukuwa mzuri.
IKULU INAVYOONEKANA KUMBADILISHA JPM
Hata hivyo, wakati Rais Magufuli akiwa amebakiza kipindi kisichozidi miezi sita kufikia nusu ya muhula wake ofisini, kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, jambo moja ambalo linaonekana kutoangaliwa kwa karibu na wachambuzi wa makundi yote mawili, ni lile la namna Ikulu inavyoonekana kumbadilisha taratibu na kumfanya azidi kuwa rais mwenye haiba tofauti na ile aliyoingia nayo madarakani.
Ni bayana kwamba JPM wa leo si yule aliyeingia na kasi kubwa ya kutumbua majipu, kufanya ziara za kushtukiza na kuchukua uamuzi mgumu na uharaka kila alipojitokea hadharani kama ilivyokuwa miezi sita, mwaka au miaka miwili iliyopita.
JPM ambaye hivi majuzi alikuwa katika ziara ya kikazi Mwanza, alionyesha kuwa mtulivu na pengine mwenye subira zaidi hata pale alipoonekana dhahiri kubaini hali ya mambo kutokwenda sawasawa.
Aliingia Mwanza muda mfupi tu baada ya tukio la kutiwa ndani kwa Meya wa jiji hilo, James Bwire, tukio ambalo lilipokewa kwa mabango na kelele kutoka kwa wananchi.
Akihutubia mamia ya wakazi wa jiji hilo, JPM aliwaomba kuwa watulivu na akawapa taarifa za meya wao kutoka korokoni na mwisho akahitimisha hotuba yake kwa kuupongeza uongozi wa Mkoa wa Mwanza na akatoa wito kwa viongozi kukaa chini kumaliza tofauti zao.
Miaka miwili Ikulu inaonyesha kumfinyanga zaidi Rais hata katika eneo la uundaji wa serikali yake na uteuzi wa viongozi mbalimbali wanaomsaidia.
Mabadiliko madogo na ya msingi aliyofanya katika Baraza la Mawaziri alilolitangaza Oktoba7, mwaka huu, akibadili sura za baadhi ya mawaziri, kuongeza idadi yao na ile ya wizara ni ushahidi mwingine wa namna Rais Magufuli anavyoendelea kupata taswira halisi ya uzito wa mamlaka aliyonayo kama mkuu wa dola aliye na uzoefu wa kazi tofauti na ile aliyoingia nayo.
Hatua yake ya kuongeza ukubwa wa Baraza la Mawaziri iliibua maswali ya msingi na yaliyotarajiwa, kuhusu dhamira yake ya miaka miwili iliyopita ya kubana matumizi kwa kupunguza idadi ya mawaziri na naibu mawaziri, aliyoitangaza Desemba 10, mwaka 2015 wakati alipounda serikali yake ya kwanza.
Uamuzi wake huo wa Oktoba 7 mwaka huu wa kuivunja iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini na kuunda wizara mbili; ya Madini na ile ya Nishati, ni moja ya hatua zinazoonyesha uzoefu na uhalisia zaidi wa kimamlaka na kiufanisi alivyopata miaka miwili akiwa Ikulu.
Alifanya hivyo pia kwa iliyokuwa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, ambayo nayo aliunda wizara mbili; ya Kilimo na nyingine ya Mifugo na Uvuvi, ambayo yeye mwenyewe alipata kuiongoza kwa kipindi kifupi wakati Jakaya Kikwete akiwa rais.
Mabadiliko hayo ya kuongezeka kwa wizara mbili zaidi kiidadi, yaliongeza idadi ya mawaziri kamili kutoka 19 hadi 21 na naibu mawaziri kutoka 16 hadi 21.
Ongezeko hilo liliongeza pia idadi ya watendaji wakuu wa wizara kutoka makatibu wakuu na manaibu wao hadi makamishna, wakurugenzi na maofisa wengine, hatua ambayo wachambuzi wa masuala ya kiserikali wameielezea kuwa inakidhi zaidi matakwa ya kimuundo, kiutendaji na kiufanisi kuliko ilivyokuwa awali.
Baada ya mikasa na migogoro ambayo imekuwa ikiigusa iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini kila mara, wachambuzi wa masuala ya utawala bora wamekuwa mara kadhaa wakishauri kutenganishwa kwa majukumu ya madini kutoka yale ya nishati, gesi na petroli.
Ni wazi, japo Rais mwenyewe hakueleza sababu hasa za uamuzi wake huo wa kutenganisha majukumu katika wizara hiyo, mahitaji ya wakati yalikuwa na nguvu kuliko dhamira ya msingi ya kupunguza idadi na ukubwa wa serikali yake kama njia ya kubana matumizi.
Hatua nyingine kadhaa ambazo Rais Magufuli amezichukua akionyesha kujifunza zaidi na pengine kuelewa majukumu na uzito wa dhamana kuu ya kitaifa aliyonayo, ni pamoja na kila wakati kuchukua hatua ya kurekebisha kasoro au uteuzi anapobaini makosa au nyufa.
Hatua ya serikali yake kupeleka kwa hati ya dharura miswada ya sheria za madini na rasilimali za taifa, siku chache baada ya kuibuka kwa mzozo wa makinikia na wawekezaji wa kampuni ya uchimbaji madini ya Acacia, ni moja ya mambo ambayo yanaonyesha kusikia na kuzifanyia kazi hoja za wachambuzi na baadhi ya wakosoaji wa serikali yake kimya kimya.
Miongoni mwa miswada mitatu, mmojawapo ni ule uliozaa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi wa Mwaka 2017.
Muswada huo ulipendekeza kuweka utaratibu ambao Bunge litakuwa na mamlaka ya kupitia na kujadili makubaliano na mikataba yote inayohusu rasilimali za nchi, ambayo imefungamana na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kujiridhisha na masharti yaliyomo.
Nyingine ni Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kuhusu Umiliki wa Maliasili wa mwaka 2017, ambayo inaweka masharti yatakayohakikisha hatua yoyote inayochukuliwa kuhusu uwekezaji wa rasilimali za taifa, inatambua na kuzingatia haki ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama taifa huru lenye mamlaka ya kusimamia na kutumia rasilimali zake kwa masilahi ya taifa.
Ya tatu ni Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ya mwaka 2017.
Uamuzi wa serikali kupeleka sheria hizo tatu ulikuja baada ya kuwapo kwa vuta ni kuvute kati yake kwa upande mmoja na wawekezaji na wakosoaji kwa upande wa pili, ambao walipinga hatua ya serikali kushikilia makontena ya mchanga wa dhahabu bandarini.
Miongoni mwa wapingaji wakubwa wa hatua za awali za serikali, alikuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), ambaye mara kadhaa aliinyoshea kidole serikali akiitaka kuwa makini na sheria za madini za zile za kimataifa ambazo zingeweza kutumiwa na wawekezaji na nchi tajiri duniani kuibana na kuiwekea vikwazo vya kisheria Tanzania.
Miongoni mwa hoja ambazo Lissu ambaye sasa amelazwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya akiuguza majeraha ya risasi alizopigwa na watu wasiojulikana, ni ile ya kutahadharisha juu ya uwezekano wa Tanzania kubanwa na Mkataba wa Kimataifa wa Uwekezaji (Multilateral Investment Guarantee Agency – MIGA).
Kama ilivyo katika hayo, Rais Magufuli alichukua mara moja hatua ya kumteua Kamishina wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga na makamishna wake siku chache tu baada ya kubaini kuwapo kwa kasoro kubwa kisheria katika vita ya kupambana na mihadarati, iliyokuwa ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kabla ya kuakisiwa na wakuu wengine wa mikoa.
Hatua ya Rais Magufuli kuunda mamlaka hiyo, ilizima mzozo mkubwa wa kitaifa ulioibuka serikalini, ndani na nje ya Bunge.
Alikuwa ni Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya (Chadema), ambaye kwanza alikumbusha juu ya Bunge kupitisha sheria ya kuundwa kwa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya tangu 2015, kisha akaeleza kushangazwa na hatua ya serikali kuendesha operesheni hiyo dhidi ya mihadarati kinyume cha sheria.
Tukio jingine lililomgusa Rais Magufuli mwenyewe moja kwa moja, lilikuwa ni kosa lililofanyika katika uteuzi wa rais, wa wabunge 10 ambao kwa mujibu wa katiba kunapaswa kuwapo kwa uwiano wa kijinsia.
Kasoro iliibuka baada ya Rais Magufuli kuwateua Profesa Palamagamba Kabudi na Abdallah Bulembo kuwa mawaziri na hivyo kubaini kwamba idadi ya wateule wanaume ilikuwa kinyume cha sheria.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 66 Kifungu (e), inamtaka Rais kuhakikisha miongoni mwa wateule wake 10, wanawake wanapaswa kutopungua watano.
Baada ya kosa hilo kubainika, mmoja wa wateule wa Rais, Dk. Abdallah Possi ambaye alikuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na watu wenye Ulemavu), alitangaza mwenyewe kujiuzulu ubunge.
Hatua hiyo ambayo ilifuta kasoro ya uteuzi, ilimfanya Rais amteue Dk. Possi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani.
Kujiuzulu kwa Dk. Possi kulimpa Rais Magufuli fursa ya kurekebisha kasoro hiyo kwa kuwateua kwanza Salma Kikwete, Anne Kilango na hivi majuzi Janeth Masaburi kuwa wabunge.
Wengine ambao tayari walishakuwa wabunge wa kuteuliwa na rais kabla yao mbali ya Profesa Kabudi na Bulembo, ni Dk. Tulia Ackson, Profesa Joyce Ndalichako, Profesa Makame Mbarawa, Dk. Augustine Mahiga na Dk. Philip Mpango.
#Mtanzania

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE