November 14, 2017

KUISHI KIZEMBE SABABU KUBWA YA KISUKARI KWA WATANZANIA


IMG-20160129-WA0139
Ndugu Wananchi,
Siku ya Kisukari Duniani, huadhimishwa duniani kote kila mwaka tarehe 14 ya Mwezi Novemba. Siku hii ilianzishwa mwaka 1991 na mashirika mawili ya kimataifa (Shirika la Ugonjwa wa Kisukari Duniani na Shirika la Afya Duniani) baada ya kuona ugonjwa wa kisukari unaongezeka sana duniani kote.
Tanzania kama zilivyo nchi nyingine zote Duniani inaadhimisha siku hii, ambapo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kushirikiana na Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania,  kwa kutoa elimu ya umuhimu wa kuzuia na kujikinga na madhara mbalimbali yatokanayo na ugonjwa wa kisukari.
Ndugu Wananchi,
Ugonjwa wa Kisukari ni hali ambayo hutokea wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu. Sukari hutumiwa na mwili ili kupata nishati lishe. Ili mwili uweze kutumia sukari inayotokana na vyakula, unahitaji kichocheo cha insulin. Insulin husaidia sukari kuingia kwenye chembechembe hai ili kutengeneza nishati lishe. Ugonjwa wa kisukari unasababishwa na kichocheo hiki kupungua au kutofanya kazi kama inavyotakiwa, hivyo kiwango cha sukari kinabaki kikubwa kwenye damu.
Kwa bahati mbaya, watu wengi  hawajitambui ya kuwa wana ugonjwa huu. Wengine wanakuwa na dalili lakini hawachukui hatua mapema. Dalili za kisukari ni rahisi kuzitambua nazo ni: kiu isiyoisha, kukojoa mara kwa mara, kupungua uzito, kusikia njaa kila wakati na mwili kukosa nguvu. Ukiwa na mojawapo kati ya dalili hizi nenda hospitali ukapime sukari.
Ndugu Wananchi,
Asilimia 80 ya wagonjwa wote wa kisukari ulimwenguni wanaishi katika nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania. Tafiti za ugonjwa wa kisukari zinaonyesha kuwa mwaka 2007 kulikuwa na wagonjwa 246 milioni duniani, mwaka 2013 kulikuwa na wagonjwa 382 milioni duniani kote. Ifikapo mwaka 2035 inatarajiwa kuwa na wagonjwa 592 milioni. Katika bara la Afrika kulikuwa na wagonjwa wa kisukari 19.8 millioni mwaka 2013 ambapo nusu ya wagonjwa hawa walikuwa hawajaanza matibabu. Wagonjwa hao wataongezeka kufikia million 41.1 ifikapo mwaka 2035. Utafiti uliofanyika mwaka 2012 na kuhusisha wilaya 50 nchini Tanzania ulionyesha ya kuwa asilimia 9.1 ya Watanzania wenye umri wa miaka 25 na kuendelea wana ugonjwa wa kisukari. Katika nchi 10 zinazoongoza kwa kisukari barani Afrika Tanzania inashika nafasi ya 8.

Kwa upande wa watoto, hadi kufikia mwanzoni mwa mwaka huu, zaidi ya watoto elfu mbili wameingizwa kwenye reiista za watoto kwenye kliniki za ugonjwa wa kisukari, ikiwa ni baadhi tu ya watoto wote wenye ugonjwa huu hapa nchini.

 

Ndugu Wananchi,
Kauli mbiu  ya  Maadhimisho ya  Siku ya  Kisukari Duniani mwaka 2017 ni “Wanawake na kisukari; haki yetu ya afya bora ya baadae”.  Kwa lugha ya kigeni ni ‘ Women and Diabetes ; Our right to a healthy future’. Kauli mbiu hii imetolewa na shirika la Afya Duniani, itumike ulimwenguni kote, kuhamasisha huduma za kisukari kwa wanawake kwa ajili ya afya bora ya sasa na baadae.
Mambo yanayoongeza uwezekano wa kupata ugonjwa wa kisukari ni pamoja na ulaji usiofaa hasa matumizi ya mafuta na sukari kwa wingi, uzito uliozidi, kutofanya mazoezi na unywaji pombe kupita kiasi.
Aidha mambo mengine yanayo ongeza uwezekano wa kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni pamoja na matumizi ya chumvi kwa wingi pamoja na uvutaji wa sigara na bidhaa za tumbaku.

Ndugu Wananchi,
Ili kuzuia ugonjwa wa kisukari ni muhimu kufuata kanuni za afya ambazo ni ulaji bora, na mtindo bora wa maisha ambao ukifuatwa vyema huweza kwa kiasi kikubwa kuzuia mtu kupata kisukari au kwa mtu ambaye tayari ana ugonjwa wa kisukari hupunguza uwezekano wa kupata madhara makubwa ya kiafya. Madhara au athari za ugonjwa wa kisukari ni upofu, shinikizo la damu kuwa juu, kiharusi, ugonjwa wa figo, kupungua nguvu za kiume, upungufu wa kinga mwilini, kuwa na vidonda hasa miguuni visivyopona mapema pamoja na ganzi katika miguu au mikono na mwisho kukatwa mguu kwa sababu ya kuathirika mishipa ya damu na mishipa ya fahamu miguuni.
Ndugu Wananchi,
Serikali inaendelea na utekelezaji wa Sera ya Afya (2007) ambayo inalenga kutoa huduma kwa magonjwa yasiyo ya  kuambukiza ikiwemo kisukari kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani ya nchi na wa kimataifa. Serikali pia inaeendelea kuandaa miongozo na mikakati ya kisera kwa kushirikisha jamii katika kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ikiwemo kisukari. Serikali imeimarisha ushiriki wa sekta mbalimbali za umma na za binafsi katika kukabiliana na vyanzo vinavyosababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

Kwa kutambua gharama za kutibu ugonjwa wa kisukari, kuanzia mwaka 1993, serikali ilitoa msamaha kwa wagonjwa wote wa kisukari kutochangia gharama za matibabu na inajitahidi kwa uwezo wa bajeti yetu pamoja na wahisani wetu kuhakikisha kuwa dawa muhimu zinapatikana. Kwa sasa watoto wote na vijana chini ya miaka ishirini na saba walio na kisukari wanapata mahitaji yao yote bila malipo kupitia kliniki za kisukari zilizopo nchini. Kwa sasa dawa za mstari wa kwanza na mstari wa pili za matibabu ya kisukari zipo kwenye mwongozo wa matibabu wa Kitaifa na zinapatikana kupitia bohari kuu ya dawa.
Kuanzia mwaka 2012, serikali pamoja na washirika wake inatekeleza mpango wa kudhibiti ugonjwa wa kisukari nchini. Lengo ni kuwa na kliniki hizo hadi katika ngazi ya vituo vya afya pamoja na kuwapatia wananchi elimu ya ugonjwa wa kisukari ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye kinga na tiba ya magonjwa haya.
Tanzania inaungana na mataifa yote duniani kutekeleza azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 2011 la kuhakikisha ya kuwa kuna mpango kabambe wa kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Nchi yetu inaungana na mataifa mengine kuhakikisha ya kuwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza yanapungua kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2030. Mwishoni mwa mwaka jana, Serikali ilizundua mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambao ulishirikisha wadau mbalimbali.
Ndugu wananchi,
Kwa bahati mbaya, unaweza kuwa na ugonjwa huu kwa muda mrefu bila kuwa na dalili zilizotajwa hapo awali. Hata hivyo, jinsi sukari inavyokuwa juu, inaharibu mishipa ya damu na ya fahamu, macho  na kusababisha upofu,  moyo na figo kushindwa kufanya kazi, na miguu kufa ganzi na kuwa vidonda, au kunyauka kwa kukosa mzunguko wa damu.
Hivyo ninatoa wito kwa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anapima afya yake kwa kuwa ugonjwa huu unaweza usionyeshe dalili yoyote mapema. Ni vyema kila mwenye umri wa miaka arobaini na kuendelea akapima afya yake angalau mara moja kwa mwaka ili kutambua hali yake ya afya. Endapo utatambuliwa kuwa una ugonjwa wa kisukari tumia huduma za afya kulingana na ushauri utakaopewa na wataalam wa afya.
Kama sehemu ya maadhimisho haya, Wizara kwa kushirikiana na Chama cha Kisukari Tanzania tutafanya zoezi la uchunguzi kwenye shule za sekondari za Kisutu na Jangwani. Pia Mikoa na Wilaya mbalimbali kwa kupitia Waratibu wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ngazi ya Mikoa na Wilaya watafanya mazoezi na pia uchunguzi.
Kwa wale ambao  wameshajitambua kuwa na matatizo ya kisukari lakini hawatumii huduma za afya ipasavyo, nawaasa watumie huduma za afya zilizopo kwa manufaa ya afya zao na kuepusha athari zinazotokana na ugonjwa ya kisukari.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE