October 11, 2017

UAMUZI MPYA WA BUNGE NA MAHAKAMA NCHINI KENYA

Bunge la Kenya limepitisha marekebisho tata kuhusu sheria ya uchaguzi, likisema ikiwa mgombea mmoja atajitoa katika uchaguzi wa marudio mwingine atashinda moja kwa moja. Wapinzani wamekosoa na kususia kikao cha bunge.
Kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, alitangaza kujitoa katika uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Oktoba 26, akielezea wasiwasi kuhusu uadilifu na uwazi katika mchakato mzima. Sheria hiyo sasa inapaswa kutiwa saini na rais Uhuru Kenyatta.
Hatua hiyo imekuja huku mahakama ya juu ikitoa hukumu kuwa mgombea aliepata chini ya asilimia moja ya kura katika uchaguzi wa Agosti 8 ambayo mahakama ya juu iliubatilisha, Ekuru Aukot ana haki ya kujumlishwa kwenye kura mpya.
Jaji John Mativo alisema siku ya Jumatano kuwa hakuona sababu yoyote kwa Aukot kuzuwia kushiriki uchaguzi wa marudio. Aukot alipata karibu kura 27,000 kati ya zaidi ya kura milioni 15 zilizopigwa katika uchaguzi uliobatilishwa.
Mahakama iliukataa uchaguzi wa Agosti 8, ambamo Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi baada ya Odinga kupinga matokeo hayo akisema wadukuzi waliingilia mfumo wa computer wa tume ya uchaguzi na kubadilisha matokeo kwa faida ya Kenyatta.
Kenia | Proteste gegen den Wahlausgang vor dem Obersten Gerichtshof in Nairobi (picture-alliance/AP Photo/B. Curtis) Wafuasi wa Odinga wakiandamana.
Odinga alitangaza kujiondoa katika uchaguzi mpya siku ya Jumanne, akisema tume ya uchaguzi laazima ibadilishwe. Na wakati maafisa wa uchaguzi wakitafakari hatua inayofuata baada ya Odinga kujitoa, wafuasi wake wameingia mitaani Jumatano kuandamana kushinikiza mageuzi ndani ya tume hiyo.
Mgawanyiko kuhusu uamuzi wa Odinga
Maoni yamegawanyika kuhusu nini uamuzi wa mwanasiasa huyo mkongwe unamaanisha, kwa uchaguzi ambao tayari umezusha taharuki, ambapo rais Kenyatta anasisitiza kura ya Oktoba 26 laazima ifanyike.
Maelfu ya wafuasi wa Odinga waliingia katika mitaa ya ngome zake magharibi mwa Kenya - Kisumu na Homa Bay, wakiwa wamebeba viboko na mabango yenye ujumbe usemao: "Hakuna mageuzi, hakuna uchaguzi".
Mahakama ya juu nchini Kenya ilibatilisha ushindi wa Kenyatta na kuamuru uchaguzi mpya uitishwe ndani ya siku 60. Lakini mchakato huo ulikwaa kisiki haraka, ambapo Odinga alidai mageuzi makubwa ambayo tume ya IEBC ilisema hayawezekani kufanyika katika muda uliohurusiwa kikatiba.
Ni kushindwa huu kufanya mabadiliko yanayohitajika ambako Odinga alisema kumemsukuma kujotoa katika uchaguzi mpya wa Oktoba 26. "Ishara zote zinaonyesha kwamba uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba 26 utakuwa mbaya kuliko wa mwanzo," alisema.
Odinga aliweka matumaini yake kwa  hukumu ya mahakama ya juu mwaka 2013 iliyotaka kufafanua sheria za sasa kwa kusema kwamba iwapo mgombea anafariki au kujitoa kwenye uchaguzi, IEBC laazima ianze mchakato wa uteuzi kuanzia sifuri. Matarajio yake yalikuwa kwamba hilo lingetoa muda zaidi wa kufanyika mageuzi.
Kenias Staatschef Kenyatta gewinnt Präsidentschaftswahl (Picture-Alliance/dpa/AP/S. A. Azim) Rais Uhuru Kenyatta
Hali ya mashaka yatawala
Uamuzi wa Odinga uliongeza hali mashaka iliowakumba raia wa taifa hilo kuhusiana na uwezekano wa kutumbukia tena katika machafuko na kukwama kwa uchumi katika taifa hilo tajiri zaidi kitika kanda ya Afrika Mashariki, na mshirika wa muda mrefu wa mataifa ya Magharibi.
Kwa wakati huu hakuna uwezekano wa kurudiwa kwa mapigano ya kikabila yaliosababisha vifo vya watu 1,200 yaliofuatia uchaguzi wa rais uliobishaniwa mwaka 2007. Lakini watu wasiopungua 37 waliuawa katika maandamano yalifuatia kura ya mwaka huu, karibu wote wakiuawa na polisi, kulingana na shirika la haki za binadamu la Kenya.
Uamuzi wa Mahakama ya Juu wa Septemba 1 uliobatilisha ushindi wa kura milioni 1.4 wa Kenyatta, ulianisha pia kwamba uchaguzi unapaswa kufanyika ndani ya siku 60. Ikiwa hilo halitafikiwa, katiba inaagiza spika wa bunge, ambaye ni manachama wa chama cha Kenyatta, kuchukuwa madaraka.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE