October 12, 2017

TRUMP ATOFAUTIANA TENA NA MWENZAKE


Rais Donald Trump ameashiria kuwa Marekani, Mexico na Canada huenda zisifikie makubaliano katika kuujadili upya mkataba uliodumu zaidi ya miaka 20 wa biashara huria katika mataifa ya Amerika ya kaskazini, wakati alipofanya mazungumzo na waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau katika ikulu ya White Hosue.
Waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau baada ya mazungumzo yake na rais Trump, amesema kwamba anayo matumaini kuhusu mustakabali wa mkataba huo wa NAFTA wakati duru ya nne ya mazungumzo ikitarajiwa kufanyika nje kidogo ya Washington. Trump ambaye kwa muda mrefu amekuwa akiukosoa mkataba huo na alikaribia kuiondoa Marekani mapema mwaka huu kabla ya kuyapatia tena mwanya majadiliano mapya, amesema "inawezekana kusifikiwe makubaliano na inawezekana pia makubaliano hayo yakafikiwa.
Hamburg G20 Treffen Trum Pena Nieto (Reuters/C. Barria) Rais Trump na mwenzake wa Mexico Enrique Pena Nieto
Trump amesema lengo lake ni kuwalinda wafanyakazi wa Marekani akihoji Trudeau pia atafanya hivyo ili kuwalinda Wacanada. "Na namaanisha, nafikiria Justin anaelewa hili, kama hatutafikia makubaliano, mkataba utasitishwa na hiyo itakuwa sawa. Watafanya vyema na sisi pia tutafanya vizuri lakini nadhani hilo halitahitajika. Lakini unapaswa kuwa sawa kwa nchi zote."
Canada bado inazingatia majadiliano mapya, amesema waziri mkuu wake wakati alipokiri maamuzi ya kushangaza ya kiongozi wa Marekani. Trudeau atasafiri  baadae kuelekea Mexico ambako atakuwa na mazungumzo na rais wa taifa hilo Enrique Pena Nieto.
"Tuna mahusiano ya karibu, nchi zote mbili zina uhusiano wa kiuchumi, utamaduni na mahusiano baina ya watu wake. Lakini tuna mahusiano mazuri siku zote na kuna njia ya kuyaboresha. Masuala yote haya tunapaswa kuyazungumzia na ndio maana tuko na mahusiano ya kujenga kati ya rais na waziri mkuu, ni muhimu na nimefurahi kukutana na wewe tena hii leo," amesema waziri mkuu.
 USA Trump und Trudeau im Wei├čen Haus | NAFTA (picture alliance/dpa/Photoshot/Y. Bogu) Waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau na rais Donald Trump
Waziri mkuu huyo wa Canada ameongeza kwamba mkataba wa NAFTA una manufaa makubwa kwa nchi zote tatu. Rais Trump ameweka uwezekano wa kufunga mkataba wa pande mbili kati ya Canada au Mexico ikiwa makubaliano mapana hayatafikiwa lakini Trudeau ameelezea dhamira yake ya kuuboresha mkataba huo wa NAFTA badala ya kufanya majadiliano ya pande mbili baina ya mataifa  hayo matatu.
Mwakilishi wa biashara wa Marekani Robert Lighthizer amesema duru ya hivi karibuni ya mazungumzo iliweza kujadili ajenda  nyingi baada ya duru ya awali kujikita katika biashara ndogo na ya kati pamoja na ushindani.
Tangu kuanza 1994, makataba wa NAFTA umeunganisha uchumi wa mataifa hayo matatu jirani , kuimarisha biashara baina yake  na kufungua masoko na uzalishaji katika bara. Trump anataka kuiondoa Marekani katika mkataba wa NAFTA baina ya Marekani, Canada na Mexico akisema makubaliano hayo yana athari kwa uchumi wa Marekani.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE