October 17, 2017

TAARIFA YA SERIKALI KWA WALIOPOTEZA VITAMBULISHO VYA KUPIGIA KURA


Wapiga kura waliopoteza vitambulisho vya kupigia kura watapata fursa ya kupiga kura katika uchaguzi mdogo wa madiwani wa kata 43 unaotarajiwa kufanyika Novemba 26, mwaka huu.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu Oktoba 16, 2017 na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Ramadhani Kailima mjini Dodoma ikiwa ni siku ya pili ya mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi yanayoratibiwa na kuendeshwa na NEC.
Kailima amesema wapiga kura hao wataruhusiwa kutumia vitambulisho vya uraia vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), hati ya kusafiria na leseni ya udereva.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia kifungu namba 62 (a) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, ambacho kinasema mpiga kura aliyeandikishwa kwenye daftari atakwenda mwenyewe kwenye kata aliyojiandikisha, kwenye kituo alichopangiwa, kumridhisha msimamizi wa kituo au msimamizi msaidizi wa uchaguzi kwamba yeye ndiye mpiga kura kwa kumuonyesha kadi ya kupigia kura lakini kinasema kwamba Tume inaweza ikaelekeza utambulisho mwingine wowote utakaomsaidia mpiga kura kuweza kupiga kura iwapo kadi hana,” amesema Kailima.
Mkurugenzi huyo wa uchaguzi amesema, “Tume kwa kuzingatia kifungu hicho, kuanzia uchaguzi huu imetoa maelekezo kwenye mafunzo haya kwamba Tume imekubali vitambulisho vifuatavyo vitumike, moja ni pasi ya kusafiria, pili ni kitambulisho cha Taifa kilichotolewa na Nida na mwisho ni leseni ya udereva.”
Amesema ruhusa hiyo imetolewa kwa sharti kwamba, “Majina na herufi yaliyopo kwenye kitambulisho hicho yafanane na majina na herufi zilizopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.”
Kailima amesema NEC itakutana na vyama vya siasa hivi karibuni kuwajulisha juu ya maagizo hayo, lakini akasisitiza kwamba tofauti yoyote itakayokuwepo kwenye majina itamnyima mpiga kura fursa ya kupiga kura.
Amesema uamuzi huo umefikiwa kutokana na kuwepo kwa changamoto kubwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambalo kwa mara ya mwisho liliboreshwa mwaka 2015.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE