October 1, 2017

MILIONI 280 ZILIVYOTAFUNA KWENYE MSIBA WA SPIKA SITTA


Kufa kufaana, ndivyo ripoti ya tathmini ya utendaji kwa mwaka 2016/17 ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) inavyoonyesha jinsi msiba wa Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta ulivyonufaisha wajanja.
Sh280 milioni zinaonekana zilitumika bila ya kufuata taratibu.
Sitta, aliyekuwa mbunge wa Urambo Mashariki, alifariki dunia Novemba 7 mwaka jana na kuzikwa Novemba 12, huku maofisa wa umma waliopewa jukumu la kusimamia maziko yake wakibainika kutofuata utaratibu.
“Ingawa kulikuwa na sababu ya msingi ya fedha hizo kutumika, lakini ofisa mwenye dhamana hakuzingatia Kifungu cha 65 (4) cha Sheria ya Ununuzi na kanuni yake namba 63 (6),” inasema ripoti ya PPRA. Uchunguzi wa mamlaka hiyo unaeleza licha ya dharura iliyokuwapo, Ofisi ya Waziri Mkuu imeshindwa kuthibitisha kuzingatiwa kwa utaratibu kwenye matumizi ya Sh284.53 milioni kwa mujibu wa sheria na utaratibu unaotakiwa.
Kwenye uongozi wake akiwa Spika, Sitta aliruhusu demokrasia na ushiriki sawa wa kutoa mawazo bungeni kwa wawakilishi kutoka vyama vya upinzani na chama tawala. Ni kwenye Bunge lililoongozwa naye, kashfa kubwa kama vile sakata la Richmond ziliibuliwa na kufanyiwa kazi.
Uwazi aliouonyesha mwanasiasa huyo aliyekuwa waziri kwenye wizara kadhaa zikiwamo za Uchukuzi na Afrika Mashariki, haujaacha alama kwa waliopewa dhamana kwenye mazishi yake.
Kwenye ukaguzi wake, PPRA inasema haikuziona nyaraka za dhamana ya ununuzi (LPO) ili kujiridhisha kama waliotoa huduma ndiyo walioombwa kufanya hivyo au kinyume chake.
Kuonyesha ukubwa wa utata huo, ripoti inasema: “Hata vocha za malipo hazikuwasilishwa wakati wa ukaguzi huo.”
Kutokana na upungufu uliobainika, PPRA ilimshauri mlipaji mkuu wa Serikali (PMG) ambaye ni katibu mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango kutotekeleza malipo hayo.
Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwaipaja alisema jana kuwa hana uhakika kama malipo hayo yameidhinishwa au la kwa kuwa ndiyo kwanza ripoti hiyo imetoka na bado hajaisoma.
“Alichokisema waziri ndicho kinachopaswa kufuatwa. Aliagiza waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria. Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango zinahusika pia,” alisema Mwaipaja.
Ripoti hiyo iliyokagua mikataba 73,154 yenye thamani ya Sh6.31 trilioni kutoka taasisi 186 kati ya 533 zilizostahili, ilikabidhiwa kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango juzi ili aiwasilishe bungeni ikajadiliwe kama sheria inavyotaka.
Taasisi zilizowasilisha taarifa zake mwaka huu ni sawa na asilimia 35 zikipungua kutoka asilimia 65 ya mwaka 2015/16 ambazo zilikuwa 322 kati ya 493 zilizostahili. Mikataba 109,575 yenye thamani ya Sh3 trilioni ilikaguliwa mwaka 2015/16.
Huenda taasisi hizo zikapungua zaidi kwa miaka ijayo baada ya Serikali kujitoa kwenye Mpango wa Uwazi Serikalini (OGP) unaotaka taarifa za utekelezaji wa masuala mbalimbali ya umma kuwekwa wazi ikiwamo mikataba ya maendeleo baina ya Serikali na taasisi za umma, binafsi au kimataifa.
Kuepuka hasara inayoweza kujitokeza kutokana na gharama za maziko ya kada huyo mkongwe wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ukaguzi ulimtaka katibu mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuzingatia sheria ya ununuzi wa umma wakati wowote anapotekeleza majukumu yake.
Sitta anakumbukwa kwa mchango wake kwenye mchakato wa Katiba Mpya akiwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba ambao ulisitishwa kupisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE