October 25, 2017

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA KONGAMANO LA 49 LA AFYA NA MKUTANO MKUU WA MWAKA WA CHAMA CHA MADAKTARI


14
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 49 la Afya na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Madaktari Tanzania ulioanza na kufanyika kwenye hoteli ya  Kunduchi Beach jijini Dar es Salaam.
6
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiangalia moja ya chupa zenye maji anayongezewa mgonjwa mwilini wakati wa Ufunguzi Kongamano la 49 la Afya Kitaifa na Mkutano Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania, kushoto pichani ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu na Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania Dkt. Obadia Nyongole.
Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais
………………..
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameliagiza Baraza la Mitihani kufanya uhakiki haraka ili wataalamu wa Sekta za Afya wapangiwe vituo.
Makamu wa Rais aliyasema hayo leo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 49 la Afya na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama Cha Madaktari, alisema “Tangu tuingie madarakani  serikali imeweza kutoa vibali vya ajira mpya vipatavyo 3,410 kwa awamu mbili, awamu ya kwanza vibali vya madaktari 258 na awamu ya pili vibali 3,150 kwa wataalamu wa kada ya afya na taratibu za ajira kwa wataalamu hawa 3150 zimekamilika na imebakia hatua ya uhakiki wa vyeti katika Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA)” Hivyo Makamu wa Rais alielekeza Baraza la Mitihani la Taifa kukamilisha uhakiki huo haraka ili wataalamu hao waweze kupangiwa maeneo ya kazi na kuanza kutoa huduma kwa Wananchi.
Makamu wa Rais aliwapongeza Chama cha Madaktari kwa kuweza kuandaa Kongamano la 49 na kuweka historia ya kuandaa Makongamano tangu mwaka 1965.
Kauli mbiu ya mwaka huu inayosema “ Malengo ya Maendeleo Endelevu: Uweledi wa Kitaaluma na Utoaji Bora wa Huduma za Afya Nchini Tanzania.” Mada hii ni muhimu sana katika kipindi hiki ambacho Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza kwa vitendo wajibu wake wa kuhakikisha kuwa wananchi wanapatiwa huduma za afya zenye viwango na zinazokidhi mahitaji alisema Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais alisema Serikali imechukua hatua mbali mbali ikiwemo kuandaa muswada  wa Bima ya Afya kwa wote kwani itasaidia sana kukabiliana na ongezeko la gharama za matibabu.
Aliendelea kusema kuwa Serikali itaendelea kutoa motisha kadri ya uwezo unavyopatikana  kwa watumishi wa kada ya afya.
Vile vile Makamu wa Rais alisema Serikali tayari imeshashughulikia suala lakuwa na mtihani mmoja kwa watahiniwa wote wa vyuo vyote vya afya nchini ambapo suala hili limezingatiwa katika sheria ya madaktari, madaktari wa weno na wataalamu wa afya shirikishi iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Septemba, 2017.
Makamu wa Rais alisema Serikali imeanza utaratibu wa kununua moja kwa moja Dawa, Vifaa, Vifaa Tiba na Vitendanishi moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji ili kupunguza gharama zilizokuwa zinatumika.
Mwisho Makamu wa Rais aliwapongeza na kuwataka kufanya kazi kwa weledi na mapendekezo yao atayachukua na kumfikishia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Kwa Upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia , Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu alihimiza weledi lakini pia alikemea vitendo vya Viongozi wengine kuwachukulia hatua madaktari na badala yake wafuate utaratibu uliowekwa.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE