October 26, 2017

AFRIKA MASHARIKI YATAKIWA KULINDA MAZINGIRA YAO


PICHA NAMBA 1
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Profesa Faustine Kamuzora akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya kujadili Takwimu za Mazingira inayoendelea jijini Arusha. Semina hiyo inajumuisha wadau wa takwimu kutoka nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutoka Ofisi ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa (UNSD).
PICHA NAMBA 2.
Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS), Irenius Ruyobya akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya kujadili Takwimu za Mazingira inayoendelea jijini Arusha. Semina hiyo inajumuisha wadau wa takwimu kutoka nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutoka Ofisi ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa (UNSD).
PICHA NAMBA 3
Baadhi ya washiriki waliohudhuria  semina ya kujadili Takwimu za Mazingira inayoendelea jijini Arusha. Semina hiyo inajumuisha wadau wa takwimu kutoka nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutoka Ofisi ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa (UNSD).
PICHA NA EMMANUEL GHULA
……………..
Na Emmanuel Ghula – Arusha
26 Octoba, 2017
NCHI Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimetakiwa kuongeza juhudi katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaoendelea kutokea kutokana na shughuli za kibinadamu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina ya Takwimu za Mazingira inayoendelea jijini Arusha, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Profesa Faustine Kamuzora amesema uharibifu wa mazingira unaoendelea kutokea ni lazima udhibitiwe ili kuepusha madhara makubwa ambayo tayari yameshaanza kuzikumba nchi zingine.
Amesema ni wajibu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuungana pamoja ili kuhakikisha changamoto zilizopo na zinazopelekea uharibifu wa mazingira zinatatuliwa.
“Mazingira ni chanzo cha maisha na yakiharibiwa na uhai unakuwa mashakani. Hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha kwa pamoja tunazikabili changamoto zinazopelekea mazingira yetu hasa Afrika ya mashariki kuharibika,” amesema Profesa Kamuzora.
Amesema uharibifu wa mazingira umesababisha vifo pamoja na maafuriko kwa baadhi ya nchi na hivyo nchi za Afrika ya mashariki hazina budi kujipanga pamoja ili kuepusha majanga hayo kutokea katika ukanda wa Afrika mashariki.
Amesema Serikali hutegemea sana takwimu rasmi zinazotolewa na ofisi ya takwimu na hivyo kupitia semina hii ya kujadili takwimu za mazingira, itasaidia katika uboreshaji wa ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu hizo zitakazotumiwa na Serikali katika kupanga mipango mbalimbali inayohusu namna ya kuhifadhi na kukabiliana na madhara yatokanayo na uharibifu wa mazingira.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS), Irenius Ruyobya amesema semina hii ni muhimu sana katika kuboresha takwimu za mazingira ambazo ndio nguzo muhimu ya Serikali katika kupanga na kusimamia utekelezaji wa mipango mbalimbali inayohusu mazingira nchini na kimataifa.
Amesema NBS Tanzania itahakikisha inashirikiana na ofisi za takwimu za nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pamona na Umoja wa Mataifa divisheni ya takwimu ili kuhakikisha takwimu bora za mazingira zinapatikana.
Semina ya kujadili takwimu za mazingira inafanyika mkoani Arusha kwa siku tano ambapo imejumuisha wawakilishi kutoka ofisi za takwimu za nchi za Afrika Mashariki na imeanza Jumatatu ya Octoba 23 na itahitimishwa Octoba 27, 2017. Semina hii imeandaliwa na kuratibiwa na Ofisi ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa (UNSD) na Sekretariati ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE