September 22, 2017

ZITTO ASHUSHA MAMBO 10, SERIKALI YAYAPANGUA


 Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe jana amesisitiza msimamo wake kwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwa Bunge limekosa meno na limeingiliwa na mhimili wa Serikali, huku pia akiihusisha Serikali na shambulio la risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Hata hivyo, Msemaji wa Serikali Hassan Abbas amekanusha madai ya Zitto akimtaka kufuata kanuni za Bunge na kuheshimu sheria za nchi.
Zitto aliyekamatwa juzi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akitokea Kigoma, alikiri kutoa maoni kwenye mitandao ya kijamii akimkosoa Spika wa Bunge, Job Ndugai na Serikali na kusisitiza kuwa anatumia uhuru wake wa kikatiba kutoa maoni.
Awali, Zitto alimkosoa Spika baada ya ripoti ya kamati aliyoiunda kuchunguza biashara ya madini ya almasi na Tanzanite kwenda kusomewa Ikulu, Septemba 7, jambo lililosababisha aitwe kwenye kamati hiyo. Hata hivyo, kabla hajaenda kwenye kamati hiyo, Zitto aliandika tena kwenye mtandao wa Twitter akimshutumu Spika Ndugai. Katika maelezo yake kwa kamati hiyo ya Bunge ambayo gazeti hili limeyaona, Zitto alikiri kuandika maoni yake katika mtandao wa Twitter yenye kichwa cha habari ‘Bunge siku hizi ni Idara ya Tawi la Utawala’ akisema Bunge la 11 limekuwa likifanya kazi kwa kuingiliwa na Serikali chini ya Rais John Magufuli. “Maneno na vitendo vya Rais yanaashiria kuwa Bunge halina uhuru wake na mimi kama mbunge nina wajibu wa kuonyesha kutopendezwa kwangu,” alisema. Mbunge huyo alitaja mambo 10 ambayo alisema yanathibitisha maelezo yake kuwa ni pamoja na kuzuiwa kuonyeshwa kwa vipindi vya Bunge moja kwa moja kupitia televisheni akisema ilikuwa ni kwa kisingizio cha kupunguza gharama za uendeshaji wa mhimili wa Bunge.
“Ni dalili ya wazi ya kufifisha sauti ya Bunge na kupandisha sauti ya Serikali. Hata vituo binafsi ambavyo vilipanga kurusha Bunge Live bila malipo vilizuiwa, lakini vinarusha live mikutano ya Rais,” alisema.
Pia, aliseka kitendo cha uongozi wa Bunge kurudisha serikalini Sh6 bilioni bila ridhaa ya wabunge kwa kisingizio kwamba zimebaki kutokana na kubana matumizi ni dalili ya “kujipendekeza” kwa Serikali na kuongeza kuwa; “Wakati Uongozi wa Bunge ukirejesha kiwango hicho cha fedha, kuna taarifa kwamba kamati nyingi za Bunge zinashindwa kutekeleza wajibu wake kwa sababu ya ukata.”.
Alitaja sababu ya tatu kuwa ni maelekezo ya Serikali kwa Bunge kupitia maagizo ya Rais Magufuli kwa Spika Ndugai aliyoitoa wakati akipokea Ripoti ya Profesa Osoro kuhusu mikataba ya madini Juni 12, 2017 aliposema awashughulikie wabunge aliowaita waropokaji.
Alisema kauli hiyo inaonyesha picha dhahiri kuwa Bunge linapokea maelekezo kutoka serikalini ya kuwadhibiti wabunge hasa wanaoiwajibisha Serikali.
Pia, alisema kitendo cha Bunge kuhariri hotuba za kambi ya upinzani kwa kushinikiza kuondolewa kwa vipengele vinavyoikosoa Serikali ni sababu mojawapo ya Bunge kukosa nguvu, huku akitoa mfano wa hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Godbless Lema iliyoamriwa kuondolewa maneno yanayohusu kashfa ya mkataba wa Lugumi, kumhusisha Rais na kuuzwa kwa nyumba za Serikali, mauaji ya wanasiasa pamoja na Bunge kulinda wahalifu.
“Kauli ya Rais Magufuli ya Novemba 4, 2016 akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuwa mzizi wa mhimili wa Serikali ni mrefu zaidi kuliko mihimili mingine, baada ya kuulizwa juu ya matumizi ya Serikali nje ya bajeti inaonyesha dhahiri fikra ya Rais na Serikali yake juu ya ukuu wa mhimili wa Serikali dhidi ya Bunge,” alisema Zitto.
Alitaja pia kitendo cha ripoti ya kamati za Tanzanite na Almasi kusomwa nje ya Bunge na kuwasilishwa kwa Waziri Mkuu na Rais bila kuwasilishwa na kujadiliwa bungeni ili kuwekewa azimio la Bunge akisema kinazifanya kamati hizo kuonekana kuwa za Serikali badala ya Bunge. “Kauli ya Rais kuwa Spika alimpigia simu kumuuliza juu wajumbe wa kuwaweka kwenye kamati ya Bunge ya Tanzanite na Almasi inaonyesha dhahiri kuwa Spika anafanya kazi kwa maelekezo ya Rais. Bunge na Spika hawajawahi kuikana kauli hii ya Rais,” alisisitiza.
Vilevile alikitaja kitendo cha Serikali kutowasilisha taarifa za utendaji wa robo mwaka kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti ya mwaka 2014 ni dharau kwa mhimili wa Bunge.
“Ni dharau zaidi kwamba Serikali ilileta muswada wa sheria kuondoa kifungu kinacholazimisha Waziri wa Fedha kutoa taarifa hizo na Bunge kupitisha kuwa Sheria, hivyo kuondoa kabisa uwajibikaji wa kibajeti wa Serikali ndani ya Bunge,” alisema.
Alisema licha ya Katiba kuonyesha mihimili mitatu ya dola ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama kufanya kazi bila kuingiliana kikatiba, mbali na wajibu wake wa kutunga sheria, Bunge ni kama kiranja wa Serikali. “Haijapata kutokea katika historia ya Bunge letu, wabunge kukamatwa hovyo mbele ya mageti ya Bunge na kusafirishwa usiku usiku bila hata Spika kujulishwa kama taratibu za mabunge ya Jumuiya ya Madola zinavyotaka. Tukio linalolenga kuliziba mdomo Bunge,” aliongeza.
Shambulio la Lissu
Akiendelea kufafanua mambo hayo 10, Zitto aligusia suala Lissu kushambuliwa kwa risasi wakati mkutano wa Bunge ukiendelea Septemba 7 akisema ni mara ya kwanza kwa historia ya nchi. “Kitendo cha ‘watu wasiojulikana’ kummiminia risasi zaidi ya 30 Mbunge wa Singida Mashariki, Ndugu Tundu Lissu akitokea bungeni tena kwenye makazi yake ambayo kwa mujibu wa sheria ni sehemu ya Bunge ni dharau ya hali ya juu kwa mhimili huu,” alisema.
Katika makala yake aliyoiandika kwa ajili ya kuwasilisha kwenye kamati hiyo ya Bunge yenye kichwa cha habari ‘Asiyehusisha jaribio la mauaji ya Lissu hana moyo; asiyeamini kwamba vyombo vya dola vinahusika hana kichwa’, Zitto amejenga dhana ya shambulio hilo akilihusisha na Serikali
Msemaji wa Serikali
Akizungumza kwa njia ya simu, Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas alikanusha madai ya mhimili wa Serikali kuingilia Bunge akimtaka Zitto kuchukua hatua kama sheria zimevunjwa. “Serikali ina majukumu yake, inatoa bajeti kwa Bunge, huko ndiyo kuingilia Bunge? Bunge linatunga sheria ndiyo tuseme linaingilia mahakama? Mahakama inapotafsiri sheria inaingilia Bunge? Hii mihimili haiwezi kufanya kazi in isolation (kwa kutengana).”
Kuhusu Serikali kuhusika na shambulio la Lissu, Dk Abbas alimtaka Zitto kusubiri uchunguzi wa Serikali badala ya kujadili hisia.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE