September 27, 2017

SHIRIKA LA PELUM TANZANIA LAJIDHATITI KUMALIZA MIGOGORO YA ARDHI NCHINI.Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
DAR ES SALAAM
29.9.2017

Ardhi ni moja ya rasilimali za msingi katika uhai na maendeleo ya binadamu, wanyama, mimea na viumbe.

Ongezeko la watu, maendeleo ya kiteknolojia, kiuchumi na kijamii limesababisha uhitaji mkubwa wa ardhi kwa makundi mbalimbali hali ambayo husababisha ardhi kupanda thamani na wakati mwingine husababisha kuibuka migogoro baina ya watuamiaji.
Ugawaji, umiliki wa ardhi na maamuzi yanayofanyika na mamlaka mbalimbali kuhusiana na ardhi wakati mwingine husababisha migogoro, hivyo ili kuhakikisha haki inatendekea migogoro hiyo haina budi kutatuliwa kwa mujibu wa taratibu za kiasili na kisheria.
Ili kufikia maamuzi juu ya ardhi ni wajibu kwa wanajamii kujengewa kuhusu uelewa na ufahamu juu ya mfumo wa vyombo vya utoaji maamuzi na ili kuwawezesha wazalishaji wadogo waishio vijijini kuweza kudai, kutetea na kulinda haki zao za ardhi.
Katika baadhi ya ngazi ya kijiji kuna usuluhishi wa migogoro ya ardhi unaopitia katika njia zisizo rasmi mfano wazee wa kimila, Viongozi wa dini pamoja na mabaraza ya wazee, ambayo hayatambulizi na sheria kuwa ni sehemu ya mamlaka ya utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kupunguza na kuondoa migogoro ya aradhi nchini, Shirika la PELUM Tanzania linatekeleza mradi wa Ushiriki wa wananchi katika kusimamia sekta ya kilimo (CEGO) unaolenga kushirikisha wananchi katika kusimamia utekelezaji na uwajibikaji wa Serikali katika masuala ya ardhi nchini.
Mradi wa CEGO unaotekelezwa katika Vijiji 30 katika Halmashauri 6 za Mikoa ya Morogoro, Dodoma na Iringa umekusudia kutumia mifumo isiyo ya gharama na isiyotumia muda mwingi kusuluhisha migogoro ya ardhi hatua inayolenga kuwawezesha wananchi kupata muda wa kujihusisha na uzalishaji mali.
Afisa Programu wa PELUM Tanzania, Angolile Layson anasema mradi wa CEGO umekusudia kujenga mtazamo chanya kwa wananchi wa vijijini kuhusiana na ushirikishwaji, kujenga, kutambua na kuhakikisha uwajibikaji katika maeneo yao na kuweza kushughulikia matatizo yao bila kutegemea msaada kutoka nje.
Anaongeza kuwa mradi unatekelezwa kwa kushirikiana na Wataalamu wa Idara za Ardhi katika Halmashauri za Wilaya nchini, ambapo Shirika la PELUM Tanzania huweza kuendesha warsha na semina za mafunzo kwa Viongozi wa Serikali za Vijiji pamoja na wananchi.
Anaongeza kuwa kupitia Mpango wa Matumizi bora ya ardhi utaratibu wa mgawanyo wa rasilimali za ardhi huweza kufanywa kupitia majadiliano na makubaliano ya wahusika wote yaliyojengwa katika vipaumbele, uwezo, utamaduni na maarifa ya wenyeji kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu.
“Ushirikishwaji usiwe njia ya kushawishi walengwa kushiriki katika shughuli ambazo maudhui ya msingi yameamuliwa na watu wan je, bali uwawezeshe wanannchi kuwa na mamlaksa zaidi katika utaratibu wa upangaji wa matumizi ya rasilimali ili kuweza kuboresha maisha yao” anasema Angolile.
Kwa mujibu wa Angolile anasema Shirika la PELUM Tanzania lilitumia vigezo mbalimbali kwa ajili ya kuchagua vijiji vya utekelezaji wa mradi ikiwemo maeneo yenye migogoro ya ardhi, vijiji visivyo na mipango ya matumizi bora ya ardhi, vijiji visivyo na vyeti vya vijiji kwa kuzingatiaa mamlaka na ukubwa wa kijiji husika.
Akifafanua zaidi anasema katika kufikia malengo ya mradi huo, Shirika la PELUM Tanzania kwa kushirkiana na Halmashauri ya Wilaya husika zinateua mratibu wa mradi anayewajibika katika kusimamia mradi na kutoa elimu kwa wananchi na kuweza uwazi wa mradi kwa wananchi kupitia Serikali za Vijiji.
Angolile anataja changamoto mbalimbali zinazoikabili mradi huo ni pamoja na gharama katika upimaji wa mipaka ya vijiji na mashamba, ambapo kwa gharama za haraka kijiji kimoja huweza hugharimu kiasi cha Tsh Milioni 20-25.
“Changamoto nyingine ni pamoja na migogoro ya ardhi baina ya Wilaya na Wilaya ambayo huchukua muda mrefu kuimaliza na hivyo kuibua changamoto katika kutekeleza mpango wa matumizi bora ya ardhi” anasema Angolile.
Kwa upande wake Afisa Tathimini na Ufuatiliaji wa PELUM Tanzania, Frank Maimo anasema kupitia Mradi wa (CEGO) Shirika hilo limekusudia kupima na kutoa hati miliki za kimila za mashamba kwa wananchi 5000 katika vijiji 30 vya Halmashauri 6 za Mikoa ya Iringa, Morogoro na Dodoma.
Maimo anasema PELUM Tanzania imekusudia kuhakikisha kuwa maeneo yaliyoanishwa katika mradi huo yanaondokana na changamoto za umiliki wa ardhi ikiwemo migogoro ya mara kwa mara na kuhakikisha kuwa CEGO inaongeza fursa za uwekezaji katika kilimo na sekta nyingine.
Anasema ili kufanikisha makusudio ya mradi huo, PELUM imekuwa ikishirikiana kwa karibu zaidi na Wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya kuweza kuendesha mafunzo mbalimbali na kuwezesha upatikanaji wa vibali vya hati za umiliki.
“Kupitia Mpango wa matumizi bora ya ardhi tumekusudia kuhakikisha kuwa wananchi tunapima mashamba ya wananchi 5000 na kuwapatia hati miliki za kimila, ambapo kwa kufanya hivi migogoro baina ya wakulima itakuwa historia” 
Anaongeza kuwa hadi sasa, mradi wa CEGO umewezesha kuundwa kwa kamati katika vijiji 25 ambavyo vimeweza kusimamia na kutoa maamuzi na mashauri ya kesi mbalimbali zitokanazo na migogoro ya ardhi.
Akifananua zaidi anasema mradi wa CEGO umekusudia kuwajengea uwezo Wakulima na Wafugaji kuweza kutambua umuhimu wa matumizi ya ardhi ikiwemo kufanya kilimo endelevu na kinachokidhi mahitaji ya kizazi cha sasa na baadaye bila kuathiri ardhi na mazingira”  anasema Sensia.
Afisa Mipango Miji na Vijiji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Andrea Biashara anasema Mradi wa CEGO umekuja katika wakati mwafaka kwa kuzingatia migogoro ardhi ikihusisha mipaka na mashamba imekuwa ikirudisha nyuma maendeleo ya jamii ya Wakulima na Wafugaji.
Anaongeza kuwa Serikali kwa upande wake itahakikisha kuwa itasimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi huo ili uweze kuleta tija iliyokusudiwa ikiwemo utoaji wa hati za ardhi za mashamba na mipaka ya viijiji vya Wakulima na Wafugaji ili kuachana na mfumo usio rasmi wa umiliki wa ardhi.
Anasema katika Mkoa wa Morogoro, mradi wa CEGO unatekeleza katika Halmashauri za Wilaya ya Mvomero na Morogoro Vijijini kwa kuwa maeneo hayo ndiyo yenye idadi kubwa ya jamii za Wakulima na Wafugaji, hivyo Serikali itahakikisha kuwa jamii zinaondiokana na migogoro ya umiliki wa inayojitokeza mara kwa mara baina yao.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Kibaoni, Wilayani Mvomero, Stephano Udoba alipongeza juhudi za PELUM Tanzania kwani semina na mafunzo waliyopata yamewapa mwanga wa matumaini ya umoja, ushirikiano na mshikamano baina ya jamii za Wakulima na Wafugaji katika Wilaya hiyo.
Aidha Bi. Nesiginda Athumani Mkazi wa Kijiji cha Mela, Wilayani Mvomero amepongeza shirika la PELUM Tanzania  kwa kuwa mafunzo yaliyotolewa yamewasaidia kuongeza uelewa na sheria zinazogusa haki za ardhi za wanawake na hivyo kuwaweka katika nafasi sawa na wanaume katika kutumia, kumiliki na kuitunza aradhi.
“Mafunzo haya yamekuwa ni nyenzo ya kuamsha uelewa wa wanajamii hasa waishio vijijini juu ya masuala mbalimbali ya haki za ardhi hususani kwa wanawake ukizingatia kuwa kwa sasa kuna changamoto kubwa katika jamii juu ya uelewa kuhusu sheria zinazogusa haki za ardhi za wanawake” alisema Nesiginda.l
Maeneo ya vijiji ndipo chimbuko kuu la maendeleo ya uchumi, kwa kuwa wakulima wengi huishi huko na kuendesha shughuli zao za kiuchumi na kijamii, hivyo ili kuwepo na mwongozo wa ardhi vijijini, wilayani na mkoani, kunahitajika mipango thabiti ya matumizi ya ardhi.
Mradi wa CEGO unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani unatekelezwa katika Halmashauri za Kilolo, Mufindi (Iringa), Morogoro Vijijini, Mvomero (Morogoro), Bahi, Kongwa (Dodoma).
MWISHO


0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE