September 6, 2017

JUA SHERIA ; TARATIBU ZA UTUTUZI WA MIGOGORO YA ARDHI HII HAPA  UTATUZI wa migogoro ya ardhi, ni mojawapo ya mambo yalitengenezewa mchakato mahsusi katika kupata suluhu ya matatizo ya ardhi.

Baada ya kutungwa kwa sheria mpya za ardhi mwaka 1999, yaani Sheria ya Ardhi na Sheria ya Ardhi ya Vijiji, utaratibu wa utatuzi wa migogoro ya ardhi, pia umebadilika.

Miongoni mwa mambo makubwa yaliyofanywa na sheria hizi, ambazo ni matokeao ya sera ya ardhi ya taifa, ni kutengeneza mfumo wa kipekee wa kutatua matatizo ya ardhi.

Sehemu ya tano ya sheria ya ardhi ya vijiji, namba 5 ya mwaka 1999, inahusu utatuzi wa migogoro ya ardhi ya kijiji.

Kwanza kabla hatujajua njia hizi za utatuzi wa migogoro ya ardhi, ni vema tukajua maana ya vitu vifuatavyo, ambavyo vinauhusiano wa moja kwa moja na sheria hii ya ardhi ya vijij
i na utatuzi wa migogoro kwa ujumla.

Kwanza ni hati ya hakimiliki ya kimila kama ambavyo imeelezea na kifungu cha 2 cha sheria hii, ambacho kinafanya rejea katika kifungu cha 25(2) amabcho kinaelezea kwamba hatimiliki ya kimila itatolewa katika fomu maalum iliyoainishwa na sheria.

Na itakuwa na sahihi ya mwenyekiti wa halmashauri ya kijiji na katibu wake. Pia hati hii itatakiwa kuwekewa sahihi au alama ya dole gumba na mtu atakayepewa hati hii kama mmiliki, pia itatakiwa kutiwa sahihi na kuwekwa na ofisa ardhi wa wilaya ambayo kijiji husika kipo.

Dhana ya pili ambayo ndugu msomaji utatakiwa uwe nayo akilini wakati wa kutatua migogoro ya ardhi ya kijiji ni ya mwanakijiji aliyepewa sheria hii chini ya kifungu cha 2 kwamba ni mtu ambaye kwa kawaida ni mkazi wa kijiji au ni mtu ambaye anatambuliwa na halmashauri ya kijiji huisika.

Vilevile, vizuri tukajua tasfiri ya halmashauri ya kijiji kama inavyoelezewa na sheria hii kwamba ni tasfiri iliyotolewa na sheria ya serikali za mitaa (mamlaka za wilaya) ya mwaka 1982.

Pia baraza la ardhi la kijiji pia limepata tafsiri ndani ya sheria hii kwamba ni baraza la lililoanzishwa maalum kwa ajili ya kusuluhisha na kusaidia kupatikana kwa muafaka kwa pande mbili zinazopingana katika mgogoro wa ardhi ya kijiji.

Baada ya kuangalia dhana hizo, basi tuanze kuangalia taratibu za utatuzi wa migogoro ya ardhi za kjiji.
Chini ya kifungu cha 16 cha sheria hii, kila kijiji kimeamuriwa kiuende baraza lake la ardhi la kijiji, ambalo, kama tulivoona hapo awali, litakuwa na kazi kubwa mbili, kwanza kusuluhisha migogoro yote inayotokana na ardhi katika kijiji kilichopo, na kazi ya pili ni kusaidia kusuluhisha pande zinazohusika katika mgogoro wa ardhi za kijiji, kufikia muafaka.

Baraza hili kwa mujibu wa sheria hii, linatakiwa kuwa na wajumbe saba ambao watatu kati yao watakuwa ni wanawake, ambao sheria chini ya kifungu cha 60(2) kifungu kidogo cha (a) na (b) kimeweka taratibu za kuwapata na kwamba watatakiwa kuwa wameteuliwa na halmashauri ya kijiji na pia watatakiwa kuafikiwa na mkutano wa kijiji.

Mkutano huu, umetafsiriwa na sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) ya mwaka 1982.
Kwa mantiki hiyo, mtu anapokuwa anataka kupitia sheria hii, basi anatakiwa kutilia maanani pia sheria hiyo ya Serikali za Mitaa (mamlaka za wilaya) ya mwaka 1982.

Chini ya sheria hii, kuna athari pale mtu ambaye kama mjumbe. anatakiwa kuthibitishwa na akashindwa kuthibitishwa basi mtu mwingine atatakiwa kuteuliwa na kuthibitishwa kuchukua nafasi kama mjumbe wa baraza la ardhi la kijiji.

Hali hii pia itatokea kama mjumbe husika atajiuzulu nafasi yake, au kama atafariki dunia, au kama atakosa heshima na sifa nzuri za kuwa na ufahamu wa sheria za mila za ardhi na kama mtu mwenye msimamo.
Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 60(3) cha sheria hii.(chanzo JF)

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE