September 21, 2017

HAYA NI MAELEZO YA MBUNGE ZITTO KABWE LEO ALIPOHOJIWA

TAARIFA KWA UMMA
_______
Kwa siku za hivi karibuni imeibuka tabia kwa baaadhi ya Wanasiasa na Wananchi 
kulishambulia Bunge na Viongozi wake kwa kutoa maelezo potofu kwamba Bunge la 
Kumi na Moja halina meno, halitekelezi wajibu wake ipasavyo na kwamba Bunge 
limetekwa na Serikali hivyo linaendeshwa kwa kufuata maelekezo kutoka Serikalini. 
Aidha, kwa kutumia lugha za kejeli, matusi na uchochezi watu hao wamekuwa 
wakilikebehi Bunge na Viongozi wake, mathalan kwamba Mhe. Spika anatumia ubabe, 
ameshindwa kusimamia uhuru na hadhi ya Bunge, hafuati Kanuni na hatendi haki kwa 
baadhi ya Wabunge. 
Gazeti la kila wiki la MwanaHALISI Toleo Namba 409 la Jumatatu, Septemba 18 -24, 
2017 nalo limefuata mkondo huo wa kulishambulia Bunge kupitia makala zenye vichwa 
vya habari kama vile “Risasi yakwama kwenye waleti” (Saed Kubenea), “ Ndugai 
anatamani aendeshe Bunge Kiimla” (Chris Alan,) “Ndugai Atumia Polisi Kuita Kubenea, 
Zitto” (Mwandishi Wetu), “Ubabe wa Ndugai si Ujasiri” (Gululi Kashinde) na “Kwa 
Mwenendo huu Ndugai hatamkaribia Sitta” (Mwananchi, Buguruni Malapa). Makala zote
hizo zimejaa upotoshaji kuhusu uendeshaji wa shughuli za Bunge. Makala zote hizi zina
maelezo yanayopotosha mwenendo wa shughuli za Bunge na mamlaka aliyonayo Mhe. 
Spika katika kusimamia shughuli za Bunge.
Ni wazi kuwa upotoshaji huo, kashfa na matusi vinalenga kumshambulia na
kumdhalilisha Mhe. Spika na Bunge kwa ujumla pamoja na kumchonganisha Mhe. Spika 
na Wananchi. Chanzo cha kashfa hizo ni maelezo ya Mhe. Spika aliyoyatoa kwa nyakati 
tofauti kufafanua utaratibu wa matibabu kwa Wabunge, kauli na vitendo vya baadhi ya 
Wabunge vinavyovunja Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge na utekelezaji wa shughuli 
za Bunge.
Bunge linachukua fursa hii kufafanua kwamba, Ibara ya 100 na 101 za Katiba ya 
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 imetoa uhuru kwa Wabunge kujadili hoja 
mbalimbali Bungeni na kufikia uamuzi. Kanuni za Bunge zimeweka utaratibu mahususi 
wa kuwezesha uamuzi wa wengi kuwa ndio uamuzi ya Bunge. Hivyo, Katiba, Sheria na 
Kanuni za Bunge hazitoi nafasi kwa chombo kingine chochote kulielekeza Bunge jambo 
au uamuzi unaopaswa kufikiwa Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge (Sura ya 296) inatoa ufafanuzi wa Haki na 
Kinga za Bunge na Wabunge. Vilevile Sheria hiyo na Kanuni za Kudumu za Bunge 
vinazuia mtu yeyote kuingilia kinga, uhuru, haki na madaraka ya Bunge na kutoa
adhabu kwa wanaokiuka Sheria na Kanuni hizo. Miongoni mwa makatazo hayo ni 
kusema uongo, kudhalilisha Bunge na kudharau mamlaka ya Mhe. Spika. 
Mbunge au Mwananchi anayekiuka misingi ya kinga, uhuru haki na madaraka ya Bunge 
hufikishwa kwenye Kamati ya Bunge inayosimamia masuala ya maadili ambako 
mlalamikiwa hutakiwa kupewa Hati ya Wito (Summons). Endapo mlalamikiwa atakataa 
wito huo, Sheria imeweka utaratibu wa kulitumia Jeshi la Polisi kuhakikisha anafika 
mbele ya Kamati.
Kumekuwa na upotoshaji kuhusu utaratibu uliotumika katika kuunda Kamati Maalum za 
Bunge. Mhe. Spika ana mamlaka kuunda Kamati mbalimbali kwa ajili ya kurahisisha 
utekelezaji wa shughuli za Bunge. Kanuni zilizopo zinajitosheleza hivyo hakuna 
uwezekano wowote wa Mhe. Spika kushinikizwa kupanga Wajumbe wa Kamati. Vilevile
Kanuni ya 5 imempa Mhe. Spika mamlaka ya kuamua jambo lolote ambalo 
halijawekewa utaratibu na Kanuni za Bunge. Moja ya mambo hayo ni uundwaji wa 
Kamati Maalum za Bunge. Utaratibu huu ndio uliotumiwa na Mhe. Spika kuunda Kamati 
zilizofanya uchunguzi kuhusu Mfumo wa uchimbaji wa Madini ya Tanzanite na Almasi
nchini. Aidha kwa kutumia mamlaka yake chini ya Kanuni ya 5 Mhe. Spika alizielekeza 
Kamati hizo kuwasilisha kwake Taarifa za uchunguzi huo. Kwa muktadha huo taarifa 
hizo huwa haziingii Bungeni. Utaratibu huo sio mpya kwani Kamati iliyofanya uchunguzi 
kuhusu bomba la gesi, kushauri kuhusu vyanzo vipya vya mapato (Chenge 1 & 2) 
zilitumia utaratibu huo.
Madai kwamba Bunge linaendeshwa kibabe na kwa misingi ya kibaguzi kwa itikadi za 
vyama pia si sahihi. Kanuni ya 5(4) inatoa fursa kwa Mbunge yeyote asiyeridhishwa na 
namna Mhe. Spika anavyoendesha Bunge au uamuzi anaoutoa kuwasilisha sababu za 
kutoridhishwa kwake kwa Katibu wa Bunge ambaye atafanyia kazi kwa mujibu wa 
Kanuni.
Aidha Kanuni ya 71 inatoa haki kwa raia yeyote ambaye atajisikia kwamba amepata 
athari hasi kutokana na kauli, maneno au shutuma kutokana na mjadala Bungeni 
kuwasilisha maelezo yake kwa Mhe. Spika. Kanuni hiyo imetoa haki ya raia huyo 
kujisafisha dhidi ya kauli hizo.
Aidha, katika kusimamia utaratibu wa majadiliano Bungeni Kanuni za 59 – 68 hutumika. 
Kanuni hizo zinazuia Wabunge kutoa kauli za uongo, zisizoruhusiwa na zenye kuudhi. 
Katika kusimamia utekelezaji wa Kanuni hizi walalamikaji hudhania kuwa Mhe. Spika 
anatumia ubabe.
Kanuni za 74, 75 na 76 zimeweka utaratibu mahsusi kwa ajili ya kudhibiti fujo Bungeni 
ambapo Kanuni hizo zimempa Mhe. Spika mamlaka ya kuhakikisha kwamba amani na 
utulivu unakuwepo Bungeni wakati wote wa Vikao vya Bunge. Kwa kutumia mamlaka 
yake huweza kuwatoa nje Wabunge wanaokiuka Kanuni hizo na vilevile anayo mamlaka 
ya kumtaka Mpambe wa Bunge kuingia ndani ya Ukumbi wa Bunge na kudhibiti fujo 
zinapotokea ikiwemo kuwatoa nje ya ukumbi Wabunge wanaosababisha vurugu.
Ikumbukwe kwamba, hakuna adhabu yoyote iliyowahi kutolewa kwa Mbunge kinyume 
cha Sheria na Kanuni. 
Kuhusu madai ya kutelekezwa kwa Mhe. Tundu A. Lissu, Bunge linapenda 
kuukumbusha umma kwamba, Mhe. Spika zaidi ya mara moja alitoa ufafanuzi 
kuhusiana na jitihada zilizofanywa na Viongozi wa Bunge katika kuhakikisha Mhe.
Tundu A. Lissu anapata matibabu. Aidha alielezea kuhusu uamuzi uliofikiwa na 
Viongozi wa CHADEMA na familia ya Mhe. Tundu A. Lissu kwamba waliona ni busara 
kumsafirisha Mheshimiwa Lisu kwenda Nairobi nchini Kenya kupata matibabu kwa 
utaratibu binafsi badala ya utaratibu wa kawaida wa matibabu kwa Wabunge kwa njia 
ya Bima ya Afya. 
Tunapenda kuukumbusha Umma kwamba Bunge ni chombo cha uwakilishi wa 
wananchi kinachoendeshwa na Sheria, Kanuni, taratibu zilizowekwa na kuzingatia mila 
na Katiba, desturi za Mabunge mengine yenye utaratibu wa kibunge unaofanana na 
utaratibu wa Bunge la Tanzania. Toka kuanzishwa kwake chombo hiki kimekuwa rafiki 
kwa wananchi kwa kusikiliza na kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili, hivyo 
wananchi wasikubali kupotoshwa kwa maneno ya baadhi ya watu wenye chuki na nia 
mbaya dhidi ya Bunge na Viongozi wake. Aidha, ikumbukwe kwamba maneno na 
vitendo vya dharau, kushusha heshima na kulidhalilisha Bunge ni mambo yasiyokubalika 
na yanapaswa kupigwa vita na watu wote wanaoitakia mema nchi yetu. 
Imetolewa na:
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano,
Ofisi ya Bunge,
DODOMA.
20 Septemba, 2017

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE