September 21, 2017

ASHA ROSE MIGIRO AREJESHWA UMOJA WA MATAIFA

Image result for asha migiro


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres ameteua jopo la wataalamu 18 watakaokuwa na kazi ya kuhakikisha wanatumia uzoefu wao kukabiliana na migogoro duniani kwa njia ya kidiplomasia, huku mwanadiplomasia wa Tanzania, Dk Asha- Rose Migiro akiwa miongoni mwa wateule hao.
Hatua ya kuteuliwa Dk Migiro aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa UN kwenye jopo hilo imeelezwa na wataalamu wa masuala ya diplomasia kuwa ni uthibitisho mwingine wa namna Tanzania ilivyo mshiriki muhimu katika kusaka amani ya dunia.
Jopo hilo ambalo linafahamika kama ‘Bodi ya Ngazi ya Juu ya Ushauri kuhusu Usuluhishi’ limeundwa kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na uwakilishi wa kikanda, pia likizingatia historia ya wahusika katika masuala ya diplomasia na utatuaji wa migogoro.
Pamoja na Dk Migiro ambaye kwa sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, wengine walioteuliwa ni aliyekuwa mke wa rais wa Msumbiji na baadaye akaolewa na Rais Nelson Mandela wa Afrika Kusini, Graca Machel, Rais mstaafu wa Nigeria, Olesegun Obasanjo, Rais wa zamani wa Chile, Michelle Bachallete na Rais mstaafu wa Finland, Tarja Halonen.
Pia, wamo wanadiplomasia, mawaziri wa zamani, watu waliowahi kuongoza taasisi za kimataifa na watu wengine mashuhuri. Jopo hilo pamoja na kazi nyingine litakuwa na jukumu la kumshauri Katibu Mkuu wa UN kuhusu njia zinazopaswa kuzuia migogoro na kushiriki kutatua mizozo katika maeneo yanayokumbwa na hali hiyo.
Baadhi ya wataalamu wa masuala ya diplomasia wamesema kuteuliwa kwa watu kama Dk Migiro na Graca Machel kwenye jopo hilo kunaonyesha jinsi walivyoiva kidiplomasia na watatoa mchango mkubwa katika kuhakikisha amani inapatikana duniani.
“Mtu kama Dk Migiro ana uzoefu mkubwa wa mambo haya na kuteuliwa kwake kunadhihirisha namna Tanzania ilivyo mstari wa mbele katika kusaidia kupatikana kwa amani duniani,” amesema Innocent Shoo, Mhadhiri wa Chuo cha Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia (CFR).
Amesema Tanzania imekuwa ikishiriki katika utatuzi wa migogoro katika maeneo mbalimbali duniani, hivyo kuteuliwa kwake hakushangazi kwa vile kunaendelea kudhihirisha diplomasia ya Tanzania kwenye eneo hilo.
“Hivi sasa tunaweza kuona jinsi Rais wetu mstaafu Benjamin Mkapa anavyoendelea na upatanishi katika mzozo wa Burundi, wakati Rais Jakaya Kikwete akipatanisha nchini Libya na hata Dk Migiro amewahi kushiriki kikamilifu katika kusaka amani katika eneo la Nchi za Maziwa Makuu wakati alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na hata alipokua UN kama Naibu Katibu Mkuu,” amesema.
Kuhusu Graca Machel amesema amekuwa mstari wa mbele katika kupigania usawa ambao mara nyingi unapokosekana huwa chanzo cha kuzuka kwa migogoro mingi duniani.
 “Lakini pia alishiriki katika kusaka amani nchini Kenya wakati wa machafuko baada ya uchaguzi wa mwaka 2007,” amesema.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE