August 13, 2017

WAZIRI MAGHEMBE ATUMBUA BODI YA MBOMIPA AFUTA MIKATABA YA UWINDAJI MAKAMPUNI MATATU

Waziri  wa maliasili na utalii Prof  Jumanne Maghembe  kushoto akimsikiliza  mke wa mwekezaji  wa Camp  ya Tandale ,Johnsia  Filiakosi ,katikati ni mkuu  wa  mkoa  wa  Iringa Amina Masenza
Aliyekuwa  katibu  wa bodi ya  MBOMIPA  Joseph Kisanyaga akisoma taarifa ya  asasi   hiyo  kabla ya waziri  kuivunja
Mkuu  wa  mkoa wa  Iringa Amina Masenza akimweleza  waziri kero ya  asasi  hiyo
Kamanda  wa  polisi  mkoa  wa Iringa  Julius Mjengi na  viongozi mbali  mbali wakimsikiliza waziri Maghembe
Mkutano  wa waziri Maghembe na bodi ya Mbomipa

                          Mke  wa mwekezaji  akitoa maelezo kwa  waziri Maghembe
...............................................................................................................................
Na  MatukiodaimaBlog

WAZIRI wa maliasili na utaliii Profesa Jumanne Maghembe ameivunja bodi ya jumuiya ya uhifadhi wa wanyamapori Idodi na Pawaga (MBOMIPA) pamoja na kuvunja mikataba yote ambayo bodi hiyo iliingia na wawekezaji kwa madai ya bodi hiyo kufanya kazi kifisadi zaidi.

Pamoja na kuvunja bodi hiyo na mikataba yote iliyoingiwa na bodi hiyo pia waziri Prof Maghembe ameagiza taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU)  kuanza uchunguzi wake na kuwachukulia hatua wote waliohusika na ufisadi katika MBOMIPA.
waziri Prof Maghembe alifikia uamuzi huo jana wakati wa ziara yake katika jumuiya hiyo ya MBOMIPA na kufanya mkutano na wajumbe wa dodi ya hiyo kabla ya kuvunjwa.
Alisema kuwa anashangazwa kuona MBOMIPA inajiendesha kwa hasara na kuomba omba kwa wahisani fedha za kujiendesha wakati kimsingi asasi hiyo ilipaswa kuwa msaada mkubwa kwa wanachama wao ambao ni vijiji vinavyozunguka hifdhi hiyo.
"Hii ni aibu kubwa kwa chombo hiki ambacho kinapaswa kuwa msaada kwa jamii chenyewe kimegeuka kuwa ombaomba hivi inawezekana vipi MBOMIPA kuomba hadi msaada wa sare na mataili mawili kwa wahisani...hili ni jambo la aibu kifupi halikubaliki hakuna cha mwekezaji hapa wala cha bodi tunaanza upya vitu vyote tunaanza sifuri "
Waziri huyu alisema kuanzia jana bodi yote imevunjwa na kampuni zote zilizoingia mikataba na bodi hiyo nazo mikataba yake imevunjwa na watalazimika kuomba upya kama watakuwa na haja na sifa za kuomba.
Pia aliagiza wanasheria wawili akiweno wa halmashauri na mmoja kutoka katika tume iliyoundwa kuchunguza ufisadi wa MBOMIPA kutoka wizara yake kuandaa katiba mpya ya MBOMIPA ndani ya siku 20 .
Huku akimwomba mkuu wa mkoa wa Iringa Kusimamia mchakato mzima wa uchaguzi wa bodi mpya ya MBOMIPA na mara zoezi hilo litakapokamilika atafika kuizindua bodi hiyo mpya.
Katika hatua nyingine waziri Prof Maghembe ameagiza askari wa vijiji wa wanyamapori (VGS) ambao wanajihusisha na ujangili kukamatwa mara moja.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza alimweleza waziri huyo kuwa asas hiyo ya MBOMIPA ni moja kati ya asas ambazo zimekuwa zikimsumbua na ndio maana siku zote alikuwa hachoki kumtafuta waziri na kumuomba kuingilia Kati kutafuta ufumbuzi wa MBOMIPA.
 
Pia alisema kutokana na usimamizi mbaya wa MBOMIPA baadhi ya viongozi wake wamekuwa chanzo cha ujangili na uharibifu wa mazingira katika eneo la Nyaluhu hivyo kuanzia sasa anamtaka mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Iringa kuorodhesha majina ya wananchi wote wanaolima eneo la Nyaluhu pamoja na kuwapa notisi kabla ya kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Iringa ikiongozwa na ofisi yake kufanya oparesheni ya kuwaondoa wakulima hao na wananchi wa kijiji cha Mkumbwani.

"Kazi hii nitaisimamia  mwenyewe na kamanda wa polisi mkoa wa Iringa kama itatushinda basi tutakuwa tumeshindwa kumsaidia Rais Dkt John Magufuli na sitakubali kushindwa nachoagiza wote wanaotakiwa kuondoka waondoke wenyewe "
Akitoa taarifa ya MBOMIPA kwa waziri Prof Maghembe kwa niaba ya mwenyekiti wake katibu wa MBOMIPA Joseph kisanyaga alisema kuwa jumuiya inakabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo ya wawekezaji kushindwa kulipa madeni yao pia jumuiya hiyo kutokuwa na uwezo wa kifedha.
Mjumbe wa kamati kuu ya MBOMIPA vicent Kibiki akimpongeza waziri kwa hatua zilizochukuliwa alisema shida kubwa ni wanasiasa ambao ni madiwani na wenyeviti wa vijiji kuvuruga jumuiya hiyo.
Huku diwani wa kata ya Idodi Onesmo Mtatifikolo akidai kuwa tuhuma hizo dhidi yao hazina ukweli kwani wao huingia katika mkutano mkuu mmoja ambao wanapikea taarifa za jumuiya hiyo na kupitia wao wameweza kuvunja mkataba mmoja baada ya kushinda kesi mahakamani hivyo alidai wao kazi yao ni kuinusuru jumuiya hiyo.
"Bodi ilitaka kusaini mkataba na mwekezaji wa wa uwindaji wa Kilombero kwa miaka 20 ambao ulikuwa ni mkataba mbovu na kupitia sisi wanasiasa tulikataa na kwenda mahakamani kushinda kesi hiyo "
Mkuu wa hifadhi ya Taifa Ruaha Dkt Christopher Timbuka alisema kuwa uwepo wa MBOMIPA ni mafanikio ya uhifadhi ila kuyumba kwako ni pigo kwa hifadhi hiyo hivyo lazima chombo hicho kuwa imara zaidi na uamuzi wa Waziri utasaidia uhifadhi na kukomesha ujangili hifadhi ya Ruaha.
wawekezaji ambao mikataba yao imevunjwa na waziri Prof Maghembe ni Mkwawa Hunting safaris ,Kilombero North safaris ,Wembele hunting Safaris.
MWISHO

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE