August 13, 2017

WAFANYABIASHARA WAKWEPA KULIPA USHURU WA MAZAO KUJIFANYA WAKULIMA

WAKATI  wafanyabiashara  wakidaiwa  kutumia  agizo la  serikali la kufutwa kwa  ushuru wa mazao kukwepa ushuru ,baraza  la madiwani  la  Halmashauri ya  Kilolo  mkoani Iringa limesema ushuru  wa mazao kwa  wafanyabiashara  upo  pale pale  isipo  kuwa kwa  wakulima pekee  hawatalipa ushuru  huo.

Hatua  hiyo  imekuja  baada ya kuwepo kwa mkanganyiko mkubwa wa  ukusanyaji  wa mapato ya  halmashauri hayo  yatokanayo na  ushuru  mbali mbali wa  mazao na  kupelekea  wafanyabiashara  kukwepa  kulipa  ushuru  kwa  kisingizio  cha kufutwa  kwa  ushuru  huo.

Wakizungumza  katika  kikao  cha madiwani   wajumbe wa baraza  hilo  jana  walisema  kumekuwepo na malalamiko  mengi  toka kwa  wafanyabiashara  wanaofika  kukusanya mazao  kwenye maeneo  yao  wakieleza  kusikitishwa na hatua ya  maofisa  watendaji  kuwadai ushuru  wa mazao  wakati  serikali  ilitangaza  kufuta  ushuru  huo .

Hivyo  walitaka  baraza  hilo  kutolea  ufafanuzi  wa aina ya  ushuru  ambao  unatakiwa  kukusanywa na ule  ambao haupaswi  kutozwa kwa  mujibu  wa  maelekezo ya  serikali  kupitia  wizara ya fedha na mipango .

Akitolea  ufafanuzi  juu ya mkanganyiko   huo  uliojitokeza  mbunge wa  Kilolo  Venance  Mwamoto  alisema  kuwa ni  kweli  serikali ya  awamu ya  tano  chini ya  Rais  Dkt  John Magufuli  imekusudia  kuwatua  wakulima mzigo  wa ushuru  wa mazao   na  kuwa  ushuru  ambao  umefutwa  ni  ule wa mazao ya  chakula  na  sio  ushuru wa mazao ya  biashara.

' serikali  kwa  kutambua  mzigo mzito wa  ushuru wa  mazao  ya  chakula  ambayo wakulima  wamekuwa  wakikumbana  nao  imeamua  kufuta  ushuru  wa usafirishaji wa mazao  kuanzia gunia  moja  hadi  tani  moja kwa  wakulima'

Mbunge  Mwamoto  alisema  kuwa  kwa mkulima  hapaswi  kutozwa  ushuru  kwa  usafirishaji wa mazao kuanzia tani moja  kushuka  chini  ila kwa  wafanyabiashara  wanapaswa  kulipa  ushuru kwani  kupitia  ushuru  huo  ndivyo huduma  nyingine  zinaweza  kutolewa na Halmashauri  kupitia makusanyo  ya mapato  ya  ndani .

' Mazao ya  chakula   yanajulikana kama  mahindi , mchele na mengine  sasa  mtu unasafirisha  ngunia  tano  au tani  moja ya  vitunguu unasema  ni kwa  ajili ya matumizi kweli  Halmashauri  yetu itaweza  kujiendeshwa .......mtu  unawezaje  kusema  gunia hizo  zote ni  za  chakula '

Kwa  upande  wake  mwenyekiti  wa halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Vellance Kihwaga alisema  ni  vema  sasa  madiwani  kwenda  kuwaelekeza  wananchi  wa  kata  zao  ili kuwabana  wafanyabiashara  ambao  wanatumia  mwanya  huo wa  kusafirisha  mazao tani moja  kushuka  chini  bure .

Aidha  baraza  hilo  limeagiza  mwanasheria wa  Halmashauri  hiyo  kupitia  upya  mikataba  yote  ya  minala ya  simu na  Radio  katika wilaya  ya  Kilolo  ili  kuona kama  minala   hiyo  inanufaisha  vipi  vijiji  na Halmashauri  hiyo katika  uchangiaji  wa  ukusanyaji wa mapato .

Wakati  huo  huo baraza  hilo la  madiwani limepitisha  azimio  la  kuendesha  oparesheni ya  kuua mbwa wote  wanaozurula mitaani na  kuwachukulia hatua wenye  mbwa hao  katika  mji  mdogo wa Ilula .
Awali  akitoa  hoja   juu ya wanyanchi  wa mji  wa Ilula  wanavyoendelea  kupoteza maisha kwa  kushambuliwa na mbwa  hao  diwani  wa kata ya Nyalumbu David Mfungwa (Chadema)  alisema  kuwa  hadi  sasa  watoto  wawili  wamepoteza maisha kwa  kushambuliwa na mbwa  hao  huku  wengine  watatu  wakiendelea na matibabu Hospitalini .

Ikumbukwe  kuwa serikali  ya  awamu ya  tano  kupitia kwa waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango Juni 8, 2017 wakati  akiwasilisha Bungeni Bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 alifuta ushuru  huo  kuwa mtu anayesafirisha mazao yake kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine yasiyozidi tani moja 1 asitozwe Ushuru
MWISHO

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE