August 30, 2017

RC IRINGA AONYA WATUMISHI MANISPAA YA IRINGA KUJIHUSISHA NA SIASA OFISINIMKUU  wa  mkoa  wa  Iringa  Amina Masenza amewaonya   watumishi  wa halmashauri ya  Manispaa ya  Iringa ambao  wanajihusisha na siasa  katika ofisi zao kuacha  mara  moja  kabla ya  kuwajibishwa  kuwa  moja  kati ya mambo yanayokwamisha shughuli  za  kimaendeleo ni pamoja  na  watumishi kuacha  kutimiza majukumu yao na kukijita  kujadili mambo ya  siasa  .

Akizungumza kwa nyakati tofauti na  wenyeviti wa  serikali za  mitaa pamoja na   baadhi  ya watumishi  wa  halmashauri  hiyo  juzi  wakati  wa  kikao  chake na wazee  wanaotoka  katika  familia duni wanufaika na mradi  wa TASAF katika Halmashauri ya  Manispaa ya  Iringa   ,mkuu  huyo wa  mkoa  alisema  ili  wananchi  wote  waweze  kupata  huduma  bora na kwa wakati ni lazima watumishi  wa umma kuacha kuendekeza siasa  maeneo ya kazi .

“ Ninyi  ni  watumishi  wa umma  mpo  katika nafasi  hizo kwa  ajili ya  kuwatumikia  wananchi  wote  wanaofika  katika ofisi  zenu  sipendi  kuona wala kusikia mwananchi akilalamika  kushindwa  kupewa  huduma kwa ajili yenu watumishi  wapenda  siasa ….mkiona  kuwa hamuwezi kujizuia  kufanya siasa maeneo ya kazi basi acheni kazi  ya  umma nendeni kwenye  ulingo  wa siasa “

Alisema  kuwa  tabia  ya  watumishi  wa  umma kuendekeza  siasa  maeneo ya  kazi ni  moja ya  sababu ya  kuchelewa  kwa utendaji  kazi  kwenye maeneo yao kwani  muda  mwingi  watapata  kutumia kuzungumza  mambo ya  siasa na  siasa  za  vyama  badala ya  kutumikia  wananchi  na kutimiza wajibu  wao wa msingi .

“ Sitawavumilia  watumishi  wanasiasa  ambao  muda  wa kazi  wanaeneza  siasa badala ya  kufanya kazi … uwe  wa CCM uwe wa Chadema ama chama  chochote kile  nikikubaini  unafanya  hivyo nitakuwajibisha  mpo  kwenye maeneo  yenu kwa  ajili yakuwasaidia  wananchi  wote  sio kuwabagua ama  kutumika  kufanya  siasa  za  vyama  vyenu “

Alisema  kuwa kumekuwepo na  uchochezi unaofanywa na  watumishi  wa umma wanaotumiwa na wanasiasa ama  wao  wenyewe  na mambo mbali mbali ambayo hayakubaliki katika serikali  hii kwani  huu  si muda wa  kufanya siasa ni  wakati wa  kuwatumikia  wananchi siasa  muda  wake  ukifika  kwa  wanasiasa  watafanya  siasa  ila  sio  sasa  .

Hata  hivyo  mkuu  huyo wa mkoa alionya  wasimamizi wa mradi wa TASAF Manispaa ya  Iringa  kusimamia  vizuri  fedha  za  TASAF na kuwa iwapo itatokea  malalamiko juu ya pesa  hizo  atakayeguswa na malalamiko hayo atawajibika .

Kuwa  lengo la  serikali kutoa fedha   za  TASAF  ni  kuona  wananchi walengwa wananufaika   hivyo  lazima  fedha   hizo  ziweze  kusaidia kuwatoa  walengwa  kwenye umasikini na kuwasogeza katika  hali ya kipato  cha  wastani  kwa  kupata  walau mlo mara tatu kwa  kutwa  na  fedha  hizo  kusimamiwa  ili  kutumia  fedha hizo kwa malengo  sahihi .

Mratibu wa TASAF katika Halmashauri ya  Manispaa ya  Iringa Lucy Mtafya alisema  kuwa  madhumuni ya  TASAF awamu  ya tatu  ya  mpango wa  kunusuru kaya  ulilenga  kuziwezesha kaya masikini kupata mahitaji ya  msingi na fursa  za  kujiongezea  kipato ,kulinda raslimali zao  na kuweka akiba  kwa ajili ya kujiletea maendeleo  na hatmaye kujitoa katika umaskini .

Alisema  kuwa   jumla ya  kaya  4503  zilitambuliwa katika Manispaa ya  Iringa  kwenye mitaa 98 na  idadi ya kaya  zilizopitishwa ni  3485 huku  kaya zisizopitishwa kwenye mfumo ni 1018 na  idadi ya kaya zilizoandikishwa ni 3,467 ambazo zipo katika  kata 18  za Manispaa ya Iringa zinanufaika na TASAF  

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE