August 16, 2017

NYUMBA YA MFUGALE NA VIGOGO WENGINE KUBOMOLEWA


Nyumba tatu za vigogo zilizopo eneo la Mbezi kwa Msuguri na Mbezi kwa Yusufu zimewekewa alama ya X kwa lengo la kubomolewa ili kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro inayoanzia Mbezi hadi Kiluvya.
Vigogo hao ni balozi mstaafu wa Tanzania nchini Botswana, Gracian Rutha, mmiliki wa Hoteli ya Peacock iliyopo eneo la Mnazi Mmoja jijini hapa, Joseph Mfugale pamoja na mkurugenzi mstaafu katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mukola Nkulu.
Hizo ni miongoni mwa nyumba nyingi zinazotakiwa kubomolewa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kutokana na kuwa ndani ya hifadhi ya barabara ya mita 121.5 kila upande.
“Hakuna nyumba ya mkubwa katika nchi hii, ambaye nyumba yake iko kwenye hifadhi ya barabara itaachwa, itabomolewa tu,” ni kauli ya mhandisi mkuu Tanroads Mkoa wa Kimara, Jonson Lutechura.
Nyumbani kwa Rutha
Waandishi wetu walifika nyumabani kwa Balozi Rutha na kupokewa na Ombeni, kijana aliyejitambulisha kuwa ni mtoto wa balozi huyo.
“Ni kweli hapa ni nyumbani kwa Balozi lakini alishastaafu. Nyumba yake kweli itavunjwa lakini Balozi ametoka muda kidogo,” alisema kisha akatoa namba za simu za Balozi huyo ili atafutwe kwa maelezo zaidi.
Alipotafutwa balozi huyo alisema, “Ni kweli nyumba yangu inavunjwa lakini siwezi kuongea chochote kwa sasa kwani nipo kwenye kikao, mnaweza kunitafuta kesho,” alisema.
Nyumbani kwa Mfugale
Waandishi wetu pia walifika nyumbani kwa Mfugale na kukuta ukimya ukiwa umetawala kana kwamba hakuna mtu.
Nyumba nzuri ya ghorofa moja iliyopakwa rangi nyeupe na kupambwa na madirisha ya vioo, huku ikizungushiwa uzio mkubwa, nayo imechorwa alama kubwa ya X na maandishi ya rangi nyekundu yaliyosomeka, “Bomoa Tanroads DSM” kila upande wa nyumba hiyo.
“Hodi” waandishi walibisha lakini ukimya ulizidi kutawala kiasi cha kudhani kwamba huenda hakuna mtu, mara sauti ya kukaribishwa ilisikika.
“Karibuni, tuwasidie nini? Alikaribisha na kuhoji mama mmoja ambaye baadaye waandishi walielezwa kuwa ni mtoto wa kigogo akitaka kujua wageni hao kina nani na wametoka wapi.
Baada ya kujitambulisha, mama huyo alisema baba yake hayupo na kwamba hawezi kuzungumza chochote mpaka awasiliane naye.
“Baba hayupo naomba kwanza tuongee naye,” alisema kisha akatoa simu na kupiga, “Baba kuna waandishi wametoka gazeti la Mwananchi wamekuja hapa wanaulizia kuhusu bomoabomoa.”
Baada ya dakika moja alimpa simu hiyo mwandishi ili azungumze na na baba yake.
“Samahani baba tunafuatilia kuhusu nyumba yako kuwekewa alama X,” alisema mwandishi aliyepokea simu hiyo.
Mfugale alijibu, “Kwanza niseme mimi siwezi kubomoa nyumba yangu mpaka nilipwe.”
Alisema alijenga nyumba yake hiyo tangu mwaka 1996 akisema kipindi hicho, sheria ilikuwa ni mita 30 na nyumba yake ilikuwa mbali kabisa na umbali huo na kulikuwa na mawe ya mpaka wa barabara.
“Baadaye tukaletewa hiyo sheria ya mita 121 ambayo hatujui ilitoka wapi, kiukweli mimi nasema tena siwezi kubomoa mpaka nilipwe na wala siwezi kuhamisha familia yangu mpaka siku watakapokuja wao kunibomolea,” alisema.
Mfugale alisema nyumba yake ina vyumba vitatu na ni ghorofa moja.
“Kiukweli inaumiza sana kuona nyumba nzuri inataka kubomolewa, lakini utafanyaje ndiyo maendeleo, ninachoomba tu Serikali iwaangalie watu waliojenga wakati wa mita 30 kwani walijua wako nje ya barabara hivyo iwafikirie kuwalipa fidia,” alisema.
Mstaafu wa BoT
Tulifika Mbezi kwa Msuguri, Nyumbani kwa Nkulu ambaye alistaafu BoT tangu mwaka 1992, na tulipomkuta alieleza alivyonunua kiwanja katika eneo hilo tangu mwaka 1976 na kujenga mwaka 1980 akisema kuwa kipindi hicho eneo hilo lilikuwa pori.
“Nataka kujua hao watu wa Tanroads wametumia sheria ipi, katika kuweka hizo alama za X kwenye nyumba ambazo wanadai zipo kwenye hifadhi ya barabara,” alihoji.
Alisema kwa mujibu wa taratibu na sheria, Serikali inapotaka kuchukua eneo lolote inatakiwa ikae na wanachi, ijadiliane nao kisha wakubaliane na kuwalipa fidia kwa kuzingatia tathmini iliyofanywa kwa mujibu wa sheria.
“Sasa wanataka sisi tubomoe wakati tumejenga hapa miaka mingi, wanataka twende wapi? Hatukatai mpango wa Serikali, basi itulipe hata fidia ili tujue tutaanzia wapi,” alisema.
Imeandikwa na Jackline Masinde, Hidaya Nyanga na Asna Kaniki    

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE