August 3, 2017

CHADEMA YAENDELEA KUING"ANG"ANIA SERIKALI YA MAGUFULI

Chama cha Chadema kimedai kuwa, serikali bado haijajibu hoja zilizotolewa na  Kamati yake Kuu hivi karibuni, kuhusu mwenendo wa hali ya uchumi nchini, huku ikiikomalia kutoa ufafanuzi juu ya hali ya chakula, deni la taifa, ukusanyaji kodi, vyanzo vya mapato vilivyopokwa halmashauri pamoja na hali ya uchumi kwa wananchi.
Akizungumza na Wanahabari, leo Agosti 3, 2017, Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, Halima Mdee, amedai kuwa  majibu yaliyotolewa na serikali kupitia Msemaji wake Mkuu Dkt. Hassan Abass, hayajatolea ufafanuzi wa hoja zilizotolewa na chama hicho, na kutuhumu kwamba ripoti zilizotumiwa kujibia hoja zao zilikuwa za uongo.
“Muda wa maneno umepitwa na wakati tunataka watujibu hoja hizi, suala la deni la taifa halijajibiwa, tunataka serikali iangalie upya sera ya deni la taifa sababu utaratibu uliopo sasa umepitwa na wakati,” amesema. 
Aidha, ameitaka serikali kupitia Wizara ya Kilimo, na Wizara ya Fedha na Mipango itoe majibu kwa nini hali ya chakula inakuwa mzigo kwa wananchi katika kipindi hiki, pamoja na kutoa ufafanuzi wa sababu ya sekta ya kilimo iliyoajiri 75% ya watanzania inaporomoka. 
“La kwanza, juu ya akiba ya chakula, tulisema 2015 akiba ya chakula ilikuwa tani 468,846 wakati Rais Jakaya Kikwete anamaliza muda wake, miaka 2 baadae, akiba iliporomoka kutoka tani zaidi ya laki nne kwenda tani 74,826. Ikumbukwe kuwa,serikali inapokuwa na akiba ya chakula ya kutosha kwenye ghala la chakula inakuwa na uwezo wa kudhibiti bei holela ya chakula kutoka kwa wauzaji binafsi,” amesema na kuongeza.
 “Katika kipindi cha Kikwete, malengo yalikuwa kilimo kikue kwa 6% katika mpango wake wa miaka 5, lakini kiliporomoka kwa  3.5%, baada ya Magufuli  kuingia kimekuwa kwa asilimia 1.7, badala ya kwenda mbele tunarudi nyuma, tunatarajia serikali ije na majibu hapa, kwa nini kilimo kinachotoa ajira kinaporomoka, watupe mpango mkakati. Mwaka 2015 tulisema fedha zilizotengwa kwa ajili ya  mbolea ni  bilioni 78 na bado ilikuwa haijitoshelezi, 2017 imeshuka mpaka bilioni 10.”
Kuhusu sekta ya biashara, amedai kuwa,“kwa mwaka mmoja, kwa jinsi serikali isivyo rafiki na wafanyabishara, wafanyabiashara wanaambiwa wezi, wananchi wanaaminishwa kuwa wafanyabiashara wezi, serikali haioni madhara ya kuminya mabenki ya biashara kwamba kunagandamiza wafanyabiashara, hadi sasa biashara 7,277 zimefungwa, haioni jambo la ajabu kufungwa biashara. Haijajibu sababu ya kudorola kwa biashara.”
“Tulizungumzia ukata, wafanyabiashara kushindwa kulipa mikopo serikalini. kilichozungumzwa juzi, leo kiimezungumzwa na taasisi ya wafanyabishara na uwekezaji kwamba sababu ya serikali kuondoa fedha katika benki za biashara na kuziweka BOT ambapo haizalishwi na haizunguki,
“Kumeleta athari katika sekta ya kibenki inayochangia 30% ya pato la taifa ikiwemo kukopesha wafanyabiashara, sasa hivi hakuna asiyejua benki zimepata hasara, mabenki hayakopeshi wafanyabiashara sababu wanajua mzunguko wa fedha haulipi tunaishia kukopesha wafanyakazi,” amesema.
Mdee amedai kuwa, serikali inabidi ifanye uchambuzi kuhusu vyanzo vyake vipya vya mapato na vile vilivyohamishwa kutoka halmashauri kwenda serikali kuu, pamoja na hali ya maisha ya wananchi wake ili ijiridhishe kama uchumi wa nchi na wa wananchi unakua au la.
“Uchumi wa Tanzania kwa miaka 3 uko katika ukuaji usiopungua kwa asilimia 7. uchumi umeanza kukua tangu awamu ya pili ya Mkapa katika mapinduzi ya uchumi, majibu tunayotaka, huu uchumi ulio palepale umeweza kujitokeza vipi kwa maisha ya mtanzania, hayo ndiyo majibu tunayotaka, kwa zaidi ya miaka 10 uchumi umekua, mkulima maisha yake yamesogea, maji vijijini yanapatikana. serikali ituambie kwa kiasi gani  uchumi unajitafsiri kwa maisha ya watanzania,”

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE