July 5, 2017

WAZAZI TIMIZENI WAJIBU WENU

Image result for mwanamke  akichota  maji
Na Fatma Salum (MAELEZO)

Kadri siku zinavyosonga mbele inakuwa ni desturi kwa baadhi ya wazazi mijini na hata vijijini kutoa uhuru usio na mipaka kwa watoto wao kwa kisingizio cha kuwapenda au kutotambua wajibu wao kama wazazi.

Katika zama hizi za utandawazi kila mzazi au mlezi anapaswa kuwa makini na mtoto wake katika kila hatua ya ukuaji ili kumuwezesha mtoto huyo kujitambua na kuishi kwa malengo .

Kwenye jamii yetu tunawaona baadhi ya wazazi ambao wameshindwa kabisa kuwafundisha watoto wao heshima na utii ikiwemo kutumia vizuri uhuru walionao kama watoto hasa wanapofikia umri wa kupevuka.

Wazazi wengi na walezi hudhani kwamba jukumu lao kuu kwa watoto ni kuwapa chakula, malazi, mavazi na elimu lakini suala la kuwaongoza kimaadili hawalipi kipaumbele hivyo wanawaacha watoto wajiongoze wenyewe na hatimaye kuibua matatizo makubwa kwenye jamii.

Si ajabu kwa dunia ya sasa kumkuta kijana au binti wa umri chini ya miaka 18 ni mwanafunzi lakini anamiliki vitu vya thamani kama simu na kadhalika bila ya mzazi au mlezi wake kuuliza ama kufuatilia ili kujua amepataje vitu hivyo.

Baadhi ya wazazi hufikia hatua ya kuwasifia watoto wao ambao bado ni wanafunzi kuwa ni wajanja wanaweza kujinunulia mahitaji yao wenyewe hivyo wanawapunguzia mzigo wa kuwahudumia.

Wengine huenda mbali zaidi kufikia hatua ya kuomba msaada wa mahitaji ya nyumbani kutoka kwa watoto wao ambao wana uhakika kwamba hawana shughuli yoyote ya kuwaingizia kipato.

Wazazi wengine hawajali muda wa mtoto kutoka na kurejea nyumbani wala kufuatilia mwenendo wake shuleni kwa maana ya maendeleo yake kitaaluma na tabia kwa ujumla.

Imefika hatua baadhi ya wazazi kwenye jamii yetu hasa kina mama wanashirikiana na binti zao ambao ni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kupanga mipango ya kutafuta wanaume wa kuwanunulia mahitaji mbalimbali ya nyumbani.

Tabia hiyo ya wazazi kujisahau na kutotimiza wajibu wao katika malezi ya watoto inachangia kwa kiwango kikubwa kuzalisha matatizo mengi tunayoyaona sasa kwenye jamii yetu ikiwemo wizi, kuongezeka kwa vitendo vya kikatili, unyanyasaji wa kijinsia, UKIMWI na mimba za utotoni.

Tumemsikia Mhe. Rais Magufuli akisema kwamba hataruhusu mwanafunzi yeyote aliyepata ujauzito kurudi shuleni kwa sababu ruhusa hiyo itawahamasisha wengine kubeba mimba na kukwamisha juhudi za Serikali za kutoa elimu bora kwa kila mtanzania.

Ni wajibu wetu sasa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wetu hasa mabinti wanajitambua na kuepuka vishawawishi vya aina yoyote vitakavyoweza kuwaharibia maisha yao na ndoto zao.

Watoto wa kiume pia wanapaswa kuangaliwa na kufuatiliwa kwa karibu na tuache kasumba ya kudhani kwamba watoto wa kiume hawahitaji uangalizi kwani na wao wanapata athari kama watoto wa kike.

Kila mzazi au mlezi atambue kuwa suala la maadili ya mtoto ni jukumu lake la msingi katika kuhakikisha ustawi wa mtoto huyo kwenye elimu, afya, na makuzi kwa ujumla.

Kaulimbiu ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu ni “Maendeleo Endelevu 2030: Imarisha Ulinzi na Fursa Sawa kwa Watoto” Kaulimbiu hii inawataka wazazi, walezi, Serikali na wadau wengine kutimiza wajibu katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na maendeleo ya mtoto ili iweze kudhibiti changamoto ya ongezeko la vitendo vya ukatili nchini pamoja na kutoa haki sawa kwa watoto wote bila ubaguzi wa aina yoyote.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE