July 4, 2017

TANZANIA KUTOA MAFUNZO MBALIMBALI SUDAN YA KUSINI


Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan amekubali ombi la kuisaidia serikali ya Sudani kusini katika utoaji wa mafunzo mbalimbali kwa wataalamu wake hasa wa sekta ya afya, kilimo pamoja na kupatiwa walimu wa lugha la Kiswahili.
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akifanya mazungumzo na Makamu wa Kwanza Rais wa serikali ya Sudan Kusini, Jenerali Taban Deng Gai
Mhe. Samia Suluhu amesema hayo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Kwanza Rais wa serikali ya Sudan Kusini, Jenerali Taban Deng Gai kando mwa Mkutano 29 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika Jijini Addis Ababa Ethiopia.
"Ili Tanzania iweze kushirikiana vizuri na serikali ya Sudani Kusini ni muhimu kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa za nchi hizi mbili kuandaa mfumo maalum wa ushirikiano na utekelezaji wake ambao utaainisha maeneo ya kushirikiana katika sekta mbalimbali kutokana na taifa hilo changa barani Afrika kuwa na changamoto nyingi hasa kwenye sekta za afya, elimu, kilimo, siasa, ulinzi na usalama", alisema Mhe. Samia.
Aidha, Makamu wa Rais ameziomba Wizara za Mambo ya Nje za Nchi zote mbili kuandaa mpango huo haraka kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa pande zote huku Mhe. Samia akionyesha  kuguswa sana na tatizo na vifo vinavyatokana na uzazi na ameshauri serikali ya Sudan Kusini, pamoja na changamoto zao za kiuchumi ijaribu kuboresha kadri itakavyoweza, miundombinu ya barabara, magari ya kusafirisha wangonjwa kwa haraka, vifaa tiba na kuimarisha vyumba vya dharura vya uzazi ili kukabiliana na tatizo hilo.
Kwa upande wake, Jenerali Taban Deng ameishukuru serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono serikali ya Sudan Kusini kupitia Jumuiya mbalimbali hususan Jumuiya ya Afrika Mashariki katika juhudi zake za kutafuta amani ya kudumu pamoja na kuwavumilia kadri inavyowezekana hasa wanapopitia changamoto mbalimbali kufikia amani hiyo.  
Vile vile, Jenerali Taban amesema serikali ya Tanzania ni mdau muhimu wa maendeleo kwa taifa lake ambalo ni changa barani Afrika hivyo kutaka kuendelea kusaidiwa ili waweze kuimarisha hali ya ulinzi na usalama pamoja na uimarishaji wa utoaji wa huduma za msingi kwa wananchi wake.

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE