July 16, 2017

TAMKO LA MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU KUHUSU KUKAMATWA KWA WENZAO

MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU TANZANIA

TAMKO KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KUKAMATWA KWA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU WILAYANI KISHAPU-MKOA WA SHINYANGA 
UTANGULIZI

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzanaia wenye wanachama zaidi ya 130 wanaofanya kazi katika maeneo tofauti ya haki za binadamu tunasikitishwa na kukamatwa kwa watetezi wawili wa haki za binadamu katika wilaya ya Kishapu; Mkoa wa Shinyanga. 


Bibiana Mushi na Nichodemus Ngelela walikamatwa wakati walipokuwa wakifanya semina ya kujenga uwezo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zinazopatikana karibu na maeneo yenye uwekezaji wa madini. Bibiana Mushi na Nicodemus Ngelela ni Watetezi wa Haki za Binadamu kutoka katika shirika la Actions for Democracy and Local Governance  ADLG  ambalo linapigania ushiriki wa wananchi, demokrasia na utawala bora katika mkoa wa Shinyanga hapa Tanzania. ADLG iliundwa ili kupambana na utawala mbovu na maamuzi ya kisiasa yanayoathiri ustawi wa Watanzania masikini kwa kuwajengea uwezo ili waweze kutetea haki zao. Kazi za shirika hilo zinalenga hasa jamii zinazojihusisha na madini, kilimo na uvuvi. 

ADLG imekuwa ikiendesha mpango wake wa utawala bora tangu mwaka 2011 na sehemu ya msingi ya programu hiyo ni warsha za mafunzo na kuendelea kushauriana na kutoa elimu ili kuhamasisha jamii iweze kuwa na sauti katika michakato ya kutunga sera katika hatua ya kitaifa na kimataifa.


Watuhumiwa walikamatwa tarehe 12 Julai 2017 kufuatia amri ya Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Nyabanga Taraba. 

Siku ya tukio, watetezi hao wa haki za binadamu walifika eneo ambalo semina ilitakiwa kufanyika na kuona Mkuu wa Wilaya amefika katika eneo hilo akiwa na Maofisa wa Jeshi la Polisi.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la ADLG Jimmy Luhende aliuambia Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu kwamba Shirika hilo limekuwa likifanya semina katika vijiji vilivyolengwa, kuanzia tarehe 11 Julai 2017 na walikuwa karibu kumaliza mpango huo  kwa kutembelea vijiji vitano vilivyo katika wilaya hiyo ya Kishapu.


 Makosa Wanayoshutumiwa Kufanya
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania umekuwa ukifuatilia kwa karibu kukamatwa kwa Watetezi hao wa Haki za Binadamu na hivyo uliajiri Wakili ili kutoa msaada wa kisheria kwa watuhumiwa. 

Wakili alipowauliza polisi juu ya kosa la watuhumiwa aliambiwa kuwa watuhumiwa wamekamatwa kwa kosa la kukusanyika kinyume cha sheria. 

Cha kushangaza, Hati ya Mashtaka, iliyosomwa mbele ya Mahakama ya Wilaya ya Kishapu, ni tofauti na madai hayo.

 Kosa lililopo kwenye hati ya mashtaka ni kutotii wajibu uliowekwa kisheria kinyume na kifungu cha 123 cha Kanuni ya Adhabu, CAP 16 ikisomwa kwa pamoja na kifungu cha 35 (1) cha Sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2002. 

Watuhumiwa hao wawili wameachiwa huru kwa dhamana ya mahakama baada ya kukaa kwa siku mbili mahabusu baada ya kunyimwa dhamana ya polisi. Kesi yao imepangwa tarehe 10 August 2017 kwa ajili ya kutajwa.

Inaonekana bila shaka yoyote kwamba mashtaka hayo dhidi ya watuhumiwa ni mabaya na yanalenga kuzuia kazi yao halali ya kutoa elimu kwa ajili ya ustawi wa jamii.


Ongezeko la Kuminywa kwa Nafasi ya Asasi za Kiraia / Watetezi  Nchini
Kumekuwa na ongezeko la tabia ya wakuu wa Mikoa na Wilaya kutumia nguvu pasipo busara kupitia nguvu walizopewa na Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997, (kifungu cha 7 na 15 kwa pamoja) katika kuzuia au kutoa amri ya kukamata watu pasipo kujali haki. 

Matukio kama hayo yameathiri kwa kiasi kikubwa kazi za watetezi wa haki za binadamu na hivyo kuminya nafasi ya Asasi za kiraia nchini Tanzania.

Yafuatayo ni baadhi ya matukio ya mwaka 2017 ambayo yanaonyesha jinsi viongozi wetu hasa Wakuu wa Mikoa na Wilaya walivyokuwa wakitumia nguvu kuminya nafasi ya AZAKi na wanakiuka haki za watetezi wa haki za binadamu. 

Mtandao umerekodi matukio ya aina hii takribani 20 kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari mpaka Julai 2017. 

Matukio hayo kwa uchache ni kama ifuatavyo:-
Mnamo Februari 2017, timu ya Asasi za Kiraia inayofanya kazi katika maeneo tofauti ya haki za binadamu ilikwenda Morogoro kwa lengo la kufanya utafiti ili kutambua chanzo cha migogoro inayotokana na rasilimali ardhi katika eneo hilo na kutoa majibu juu ya namna ya kukabiliana na hali hiyo. 

Asasi za Kiraia zilizopanga kufanya utafiti huo ni HAKIARDHI, TCRIP, CCWT, PINGOS Forum, PAICODEO, CHRAGG, TNRF, TPCF, ANSAF, MVIWATA, THRDC, LHRC, TAWLA, TAMWA and TGNP. 

Timu hiyo ilitoa taarifa katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kumjulisha kwamba, timu hiyo ilikuwa ikifanya utafiti katika eneo lake. 

Hata hivyo, timu ilishangazwa na majibu ya ofisi ya Mkuu wa mkoa kuhusu utafiti huo. 

Mkuu wa Mkoa aliandika barua ya kupiga marufuku utafiti huo kwa madai kwamba kulikuwa na zoezi la usajili wa mifugo na utambuzi, ambao ungeathiri utafiti huo. 

Timu ilijibu barua hiyo na kumwambia Mkuu wa Mkoa kwamba utafiti wetu hautaathiriwa na zoezi hilo wakati ambapo timu yetu tayari ilishakua imepata habari kutoka kwa chanzo cha kuaminika kwamba hakuna zoezi kama hilo lililokua likiendelea katika mkoa wa Morogoro.

Mnamo tarehe 17/03/2017, ofisi za Clouds Media Group zilivamiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda aliyefuatana na Maofisa wa Polisi. 

 Ilisemekana kuwa Bw. Makonda alitumia nguvu dhidi ya wafanyakazi wa Clouds Tv ambao walikataa kutangaza taarifa moja   dhidi ya mchungaji mmoja maarufu hapa Tanzania. 

 Mnamo 23 Machi 2017 Mkutano wa Waandishi wa Habari ulioandaliwa na Nape Nauye aliyekuwa Waziri wa Habari uliokuwa ufanyike katika  Hoteli ya Protea hapa Dar es Salaam ulidaiwa zuiliwa na Kamanda wa Polisi wa Kinondoni Susan Kaganda. 

Nape alifukuzwa mara moja kutoka katika nafasi yake ya uwaziri baada ya kulinda na kutetea uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania. 

 Mnamo 21 Aprili 2017, wavamizi walivamia mkutano wa chama cha Civic United Front (CUF) na waandishi wa habari wengine walipigwa kikatili. 

Tukio hilo lilivunja haki ya uhuru wa kukusanyika na kujieleza ambayo ni kinyume na Katiba yetu. 

 Mnamo 18 Mei 2017 kundi la waandishi wa habari walikamatwa na Maafisa wa Polisi huko Arusha wakati wakihudhuria tukio la kuwasilisha rambirambi kwa wazazi na jamaa za waathirika wa msiba wa shule ya  Lucky Vicent. 

Amri ya kukamatwa ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

 Mnamo tarehe 3 Juni 2017 mkutano wa ndani uliofanywa kwa mujibu wa sheria ulizuiwa na kusababisha kufunguliwa kwa mashtaka dhidi ya watetezi wawili wa haki za binadamu, Onesmo Olengurumwa na Baraka John Mbwambo. 

Mkutano huo ulikuwa wa uzinduzi wa kitabu kilichoandikwa na kijana Mtetezi wa Haki za Binadamu, Alfonce Lusako ambaye alifukuzwa kutoka masomo yake ya Chuo Kikuu. Amri ya kukamatwa ilidaiwa kuwa ilitoka kwa watu wasiojulikana ndani ya serikali. 

Mnamo Julai 4, 2017, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Salum Hapi, alitoa amri ya kukamatwa kwa Mbunge wa Kawe, Halima Mdee kwa madai kwamba mbunge huyo alitoa maneno yenye kuudhi dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Hata hivyo Mbunge huyo, alikuwa akitumia haki yake ya Kikatiba ya uhuru wa kujieleza lakini akajikuta kwenye mikono ya polisi kwa muda mrefu baada ya kukataliwa dhamana ya polisi. 

Mnamo Desemba 2016, Haki Madini, Shirika la Kiraia ambalo pamoja na mambo mengine, linahusika na utetezi wa haki za watu wanaofanya kazi katika sekta ya uchimbaji wa madini walikwenda wilaya ya Shinyanga kufanya utafiti juu ya haki ardhi kwa wanawake lakini walizuiliwa na Mkuu wa Wilaya ambaye aliwaomba barua ya kibali kutoka kwa Kamishna wa madini na Wizara ya Nishati na Madini. 

Hali ya watetezi wa haki za binadamu wanaofanya kazi katika sekta ya uchimbaji wa madini ni mbaya zaidi huko Tarime ambako watetezi wa haki za binadamu wamekuwa wakiteswa, kutishiwa, kushtakiwa kinyume cha sheria kwa sababu ya kazi zao za utetezi wa haki za binadamu. 

Waandishi zaidi ya 10 wamekuwa wakikamatwa katika maeneo mbalimbali nchini wanapofanya kazi zao kwa kudaiwa kuwa hawana kibali cha wakuu. 

Mfano wa Wilaya ambayo waadishi hadi leo wamezuiwa hata kuingia kwenye vikao vya wazi vya madiwani ni Arumeru Mkoani Arusha. 

Vyombo vya habari vimeendelea kujenga hofu kubwa na kuamua kuchagua vipindi au taarifa za kurusha kwa usalama wao au kuogopa kufungiwa kama vyombo vingine.

Mnamo tarehe 30 Julai 2017 Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu uliomba ulinzi wa askari polisi kuweza kufanya maandamano nchi nzima, kulaani mauaji ya askari polisi pamoja na raia yanayoendelea katika wilaya ya Kibiti mkoa wa Pwani.

 Hata hivyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo, walipiga marufuku maandamano hayo kwa kile walichodai kuwa yatavuruga operesheni inayoendelea nchi nzima ya kuwasaka wahalifu wa mauaji Kibiti.

Asasi za Kiraia na watetezi wa haki za binadamu wanaofanya kazi katika sekta ya madini wamekuwa lengo kuu la mashambulizi, vitisho, kukamatwa na mashtaka ya kutengenezwa kutokana na ukweli kwamba, wanaweka wazi ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanyika katika sekta ya madini. 

Utafiti na elimu kwa wadau mbalimbali katika sekta hii umekua mgumu kutokana na vikwazo vikali ambavyo vinawekwa kwa watafiti. 

Ni muhimu ikumbukwe kwamba, watetezi wa haki za binadamu na umma wanaunda sehemu muhimu katika maendeleo ya taifa lolote duniani. 

Kuzuia shughuli za AZAKi na kuweka hatua zisizohitajika dhidi ya AZAKi /watetezi wa haki za binadamu nchini hutengeneza chuki kati ya serikali na watu wake ambao ikiwa haitashughulikiwa vizuri, inaweza kusababisha machafuko katika siku zijazo. 

AZAKi zinafanya kazi za kijamii, kiuchumi na kiutamaduni, majukumu ambayo yanatakiwa kufanywa na serikali. 

Kupitia utafiti, elimu, utoaji huduma, kupanga, ufuatiliaji, tathmini, na kadhalika, AZAKi zinasaidia serikali kutekeleza mipango yake ya kimkakati. 

Ni kwa njia ya kazi za AZAKi serikali huweza kuweka bajeti nzuri na halisi ya utoaji wa huduma kwa wananchi kulingana na data na uchambuzi unaofanywa na AZAKi. 

Kwa hiyo, majukumu yao hayapaswi kupuuzwa kwa kuzingatia ukweli kwamba wanafanya kazi zao kwa mujibu wa sheria za nchi.

 Ni kwa sababu hizo serikali inaombwa kuacha watu wafurahie haki zao bila vikwazo vya aina yoyote. 

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Ibara ya 18 na 20 inatoa haki ya uhuru wa kujieleza na kusanyiko.

 Ibara ya 1, 5, 6, 7, 8, 9, 11, 12, 13 na 18 ya Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Watetezi wa Haki za Binadamu, 1998 zinatambua haki ya kutafuta ulinzi na utambuzi wa haki za binadamu katika ngazi za kitaifa na kimataifa; Kufanya kazi za haki za binadamu binafsi na kwa kushirikiana na wengine; Kuunda vyama na mashirika yasiyo ya kiserikali; Kukutana au kukusanyika kwa amani; Kutafuta, kupata, kupokea na kuhifadhi habari zinazohusiana na haki za binadamu na haki ya kulinda demokrasia, kukuza haki za binadamu na uhuru wa msingi na kuchangia kukuza jamii, taasisi na taratibu za kidemokrasia.

 Haki ya kujieleza pia inatambuliwa katika Ibara ya 19 cha Mkataba wa Kimataifa Juu ya Haki za Kiraia na Kisiasa wa mwaka 1966 pamoja na Ibara ya 22 cha Mkataba huo inayotoa haki ya uhuru wa kujiunga na vyama ambao Tanzania imeusaini. 

Kuzuia watu kufurahia haki zao ni kinyume na Katiba na mikataba mingine ya kimataifa ambayo Tanzania ni nchi mwanachama. 

Kama watetezi wa haki za binadamu hatuwezi kuacha ukiukwaji wa kutisha wa haki za binadamu uendelee bila kupingwa. 
Wito wetu: 

Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanapaswa kuacha mara moja kutumia mamlaka yao vibaya hasa pale ambapo hakuna uhalali wa kufanya hivyo. 

 Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 inapaswa kurekebishwa ili kuondoa kifungu kinachowapa Wakuu wa Wilaya nguvu nyingi ambazo sisi sote tunashuhudia zinatumiwa vibaya 
 Jamhuri inapaswa kuondoa mashtaka yote dhidi ya washitakiwa kwa sababu hayana msingi na yanahesabiwa kuwa yanavunja haki ya watuhumiwa na kuminya nafasi ya AZAKi nchini Tanzania
 Katiba yetu inapaswa kuweka njia za kuheshimu na kukuza nafasi ya Asasi za Kiraia na kuhakikisha ushiriki wa umma katika masuala yenye maslahi kwao. 

Hii ndiyo njia bora zaidi ambayo nchi ya jirani Kenya, imeweka katika Katiba yake na hivyo kufanya Asasi za Kiraia kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa lao. 

 Serikali inapaswa kuacha kuingilia kati kazi ya AZAKi nchini Tanzania kwa sababu wanafanya Kazi kulingana na sheria. AZAKi zinapaswa kuchukuliwa kama washirika wa serikali na sio adui kama ilivyo katika hali ya sasa. 

 AZAKi / Watetezi wa Haki za Binadamu wanapaswa kuendelea na kazi zao za haki za binadamu, kwa sababu wamesajiliwa kisheria na wanafanya kazi kulingana na sheria. 

Katika hali hii, tunatoa wito kwa AZAKi zote nchini Tanzania kuunganisha nguvu katika kupambana na kuminywa kwa nafasi ya Asasi za Kiraia, ambayo kwa kiasi kikubwa imechangia katika udhibiti na utendaji mbaya wa AZAKi nchini. 


 Mashirika ya Kikanda na Kimataifa yanapaswa kujiunga na juhudi zinazofanywa na AZAKi za ndani katika kurejesha nafasi ya AZAKi nchini Tanzania.

 Wanapaswa kupaza sauti zao dhidi ya ukiukwaji wa haki za Watetezi wa Haki za Binadamu na AZAKi katika nchi yetu 
 Jeshi la Polisi linapaswa kufanya kazi kulingana na sheria. 

Kukamata raia kwa kufuata amri kutoka kwa wakuu imeendelea kupunguza heshima ya Jeshi la Polisi ambayo inajenga chuki kati ya raia na polisi. 

Serikali ione AZAKI kama wadau wamuhimu kipindi hiki hasa katika utekelezaji wa malengo mbalimbali ya maendeleo kama SDGs na AU 2063 tukizingatia msemo usemao Leave No One Behind
Mashirika yanayotetea haki za kiraia na kisiasa nchini yanapaswa kuungana na kuwa mstari wa mbele kukemea uvunjifu wa haki mbali mbali za kisiasa unaondelea nchini.

Serikali iache kukataza na kutishia uhuru wa asasi za kiraia kufanya kazi zao kwani asasi hizo zimeanzishwa kwa mujibu wa sheria na zinafanya kazi zao kwa misingi ya Kisheria. Mijadala huru isiminywe na serikali kwani kupitia mijadala hiyo zinaibuka hoja na mawazo chanya ambayo yanaweza kuwa chachu ya Maendeleo katika nchi yetu.

Ni wakati muafaka sasa kama Taifa kuja na sheria au sera inayowatambua na kuwalinda watetezi wa haki pamoja asasi zao wanapokuwa wanafanya majukumu yao ya kisheria popote nchini. 

Imetolewa leo tarehe16 Julai 2017
....................................... 
Onesmo Olengurumwa 
Mratibu wa Kitaifa, 
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)

0 comments:

Post a Comment

AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 026299 Email . fgodwin94@gmail.com , ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA MWINGINE